Methali 27:1-27
Methali 27:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Usijisifie ya kesho, hujui nini kitatokea leo mpaka kesho. Acha watu wengine wakusifu, kuliko mdomo wako wewe mwenyewe. Jiwe ni zito na mchanga kadhalika, lakini usumbufu wa mpumbavu ni mzito zaidi. Ghadhabu ni katili na hasira huangamiza; lakini ni nani awezaye kuukabili wivu? Afadhali mtu anayekuonya waziwazi, kuliko yule afichaye upendo. Makaripio ya rafiki yaonesha uaminifu, lakini busu la adui ni udanganyifu. Aliyeshiba hata asali huikataa, lakini kwa mwenye njaa kila kichungu ni kitamu. Mtu aliyepotea mbali na kwake, ni kama ndege aliyepotea mbali na kiota chake. Mafuta na manukato huufurahisha moyo, lakini taabu hurarua roho. Usisahau rafiki zako wala wa baba yako. Ukipatwa na janga usikimbilie kwa nduguyo; afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Uwe na hekima mwanangu upate kunifurahisha moyo, nami sitakosa la kumjibu yeyote anayenilaumu. Mwenye busara huona hatari akajificha, lakini mjinga hujitokeza mbele akaumia. Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake; mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni. Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri, itaeleweka kwamba amemtakia laana. Mke mgomvi daima, ni sawa na tonatona ya maji siku ya mvua. Kumzuia ni sawa na kuzuia upepo, au kukamata mafuta kwa mkono. Chuma hunoa chuma, kadhalika mtu hufundishwa na wenzake. Anayeutunza mtini hula tini, anayemhudumia bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ujionavyo wenyewe majini, ndivyo ujijuavyo mwenyewe moyoni. Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi, kadhalika na macho ya watu hayashibi. Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto, na mtu hupimwa kutokana na sifa zake. Mtwange mpumbavu katika kinu pamoja na nafaka, lakini hutafaulu kumtenganisha na upumbavu wake. Angalia vizuri hali ya mifugo yako; tunza vizuri wanyama wako. Maana utajiri haudumu milele, wala taji haidumu vizazi vyote. Baada ya kukata nyasi na kuzihifadhi, kata majani toka milimani, huku nyasi zinachipua upya. Kondoo watakupatia sufu kwa mavazi, mbuzi nao utauza na kujinunulia mashamba; watakupa maziwa ya kukutosha wewe na jamaa yako, na kwa ajili ya watumishi wako wa kike.
Methali 27:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe. Jiwe ni zito, na mchanga hulemea; Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili. Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu. Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika. Majeraha utiwazo na rafiki ni ya kweli; Bali busu la adui ni udanganyifu. Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu. Kama ndege aendaye huku na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huku na huko mbali na mahali pake. Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye. Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya. Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake. Matone daima kudondoka siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa; Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kulia hukuta mafuta. Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake. Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi. Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake. Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka. Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe wako. Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Ladumu tangu kizazi hata kizazi? Manyasi hukatwa, na majani mabichi huchipua, Na mboga ya mlimani hukusanywa. Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba. Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.
Methali 27:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe. Jiwe ni zito, na mchanga hulemea; Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili. Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu. Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika. Jeraha utiwazo na rafiki ni amini; Bali kubusu kwa adui ni kwingi sana. Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu. Kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huko na huko mbali na mahali pake. Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye. Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya. Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake. Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa; Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta. Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake. Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi. Kalibu ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake. Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka. Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng’ombe zako. Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi? Manyasi huchukuliwa, na majani mabichi huonekana, Na maboga ya milimani hukusanyika. Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.
Methali 27:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Usijisifu kwa ajili ya kesho, kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja. Mwache mwingine akusifu, wala si kinywa chako mwenyewe; mtu mwingine afanye hivyo na si midomo yako mwenyewe. Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo, lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito kuliko vyote viwili. Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika, lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu? Afadhali karipio la wazi kuliko upendo uliofichika. Majeraha kutoka kwa rafiki yaonesha uaminifu, lakini adui huzidisha busu. Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali, bali kwa mwenye njaa hata kile kilicho kichungu kwake ni kitamu. Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake, ndivyo alivyo mtu atangatangaye mbali na nyumbani mwake. Manukato na uvumba huleta furaha moyoni, nao uzuri wa rafiki huchipuka katika ushauri wake wa uaminifu. Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako, tena usiende nyumbani mwa ndugu yako wakati umepatwa na maafa. Bora jirani wa karibu kuliko ndugu aliye mbali. Mwanangu, uwe na hekima, nawe ulete furaha moyoni mwangu, ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote anitendaye kwa dharau. Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha, bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara. Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie liwe dhamana kwa ajili ya mgeni. Mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu asubuhi na mapema, itahesabiwa kuwa ni laana. Mke mgomvi ni kama matone yasiyokoma siku ya mvua. Kumzuia ni kama kuuzuia upepo, au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono. Kama vile chuma kinoavyo chuma, ndivyo mtu amnoavyo mwenzake. Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake, naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso uonekanavyo kwenye maji, ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonesha alivyo. Kuzimu na Uharibifu havishibi, wala macho ya mwanadamu hayashibi. Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu, bali mtu hupimwa kwa sifa anazopewa na watu. Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu, ukimtwanga kama nafaka kwa mchi, hutauondoa upumbavu wake. Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako ya kondoo na mbuzi; angalia ngʼombe wako kwa makini. Kwa kuwa utajiri haudumu milele, nalo taji halidumu vizazi vyote. Wakati majani makavu yameondolewa na mapya yamechipua, nayo majani toka milimani yamekusanywa, wana-kondoo watakupatia mavazi na mbuzi thamani ya shamba. Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi kukulisha wewe na jamaa yako, na kuwalisha wajakazi wako.