Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 24:17-34

Methali 24:17-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo; wakati anapojikwaa, usiruhusu moyo wako ushangilie. BWANA asije akaona na kuchukia akaiondoa ghadhabu yake mbali naye. Usikasirike kwa sababu ya wapotovu, wala usiwaonee wivu waovu, kwa maana mpotovu hana tumaini la siku zijazo, nayo taa ya waovu itazimwa. Mwanangu, mche BWANA na mfalme, wala usijiunge na waasi, kwa maana hao wawili watatuma maangamizi ya ghafula juu yao, naye ni nani ajuaye maafa wawezayo kuleta? Hii pia ni misemo ya wenye hekima: Kuonesha upendeleo katika hukumu si vyema: Yeyote amwambiaye mwenye hatia, “Wewe huna hatia,” makabila ya watu watamlaani, na mataifa watamkana. Bali itakuwa vyema kwa wale watakaowatia hatiani wenye hatia, nazo baraka tele zitawajilia juu yao. Jawabu la uaminifu ni kama busu la mdomoni. Maliza kazi zako za nje, nawe uweke mashamba yako tayari, baada ya hayo, jenga nyumba yako. Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu, au kutumia midomo yako kudanganya. Usiseme, “Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; nitamlipiza mtu yule kwa kile alichonitendea.” Nilipita karibu na shamba la mvivu, karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili, miiba ilikuwa imeota kila mahali, ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka. Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona, nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona: Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika: na umaskini utakuja juu yako kama mnyangʼanyi, na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

Shirikisha
Soma Methali 24