Methali 20:1-30
Methali 20:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Divai huleta dhihaka na kileo huleta ugomvi; yeyote anayevutiwa navyo hana hekima. Ghadhabu kali ya mfalme ni kama simba angurumaye; anayemkasirisha anayahatarisha maisha yake. Ni jambo la heshima kuepa ugomvi; wapumbavu ndio wanaogombana. Mvivu halimi wakati wa kulima; wakati wa mavuno atatafuta asipate chochote. Fikira za mtu zimefichika kama kilindi cha maji; lakini mtu mwenye busara ajua kuzichota humo. Watu wengi hujivunia kuwa wema, lakini mwaminifu wa kweli apatikana wapi? Mtu mwadilifu akiishi kwa unyofu; watoto wake atakaowaacha watabarikiwa. Mfalme mwema aketipo kutoa hukumu, huupepeta uovu wote kwa macho yake. Nani athubutuye kusema: “Nimeutakasa moyo wangu; mimi nimetakasika dhambi yangu?” Mizani ya udanganyifu na vipimo vya udanganyifu, vyote ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni njema na aminifu. Sikio lisikialo na jicho lionalo, yote mawili kayafanya Mwenyezi-Mungu. Usipende kulala tu usije ukawa maskini; uwe macho nawe utakuwa na chakula kingi. “Hakifai, hakifai”, mnunuzi hulalamika, lakini akiondoka hujisifu amepunguziwa bei. Kuna dhahabu na wingi wa mawe ya thamani kubwa; lakini cha thamani kubwa zaidi ni maneno ya busara! Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake; mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni. Chakula kipatikanacho kwa udanganyifu ni kitamu, lakini baadaye huwa kama mchanga kinywani. Mipango mizuri hufanyika kwa kushauriana; ukitaka kuanza vita lazima kutafakari kwanza. Mpiga domo hafichi siri, kwa hiyo mwepe mtu wa kuropoka. Anayemlaani baba yake au mama yake, mwanga wa uhai wake utazimwa kama taa gizani. Mali iliyopatikana kwa haraka mwanzoni, haitakuwa ya heri mwishoni. Usiseme, “Nitalipiza ubaya niliotendewa.” Mtegemee Mwenyezi-Mungu naye atakusaidia. Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, na vipimo visivyo halali ni kitu kibaya. Hatua za mtu huongozwa na Mwenyezi-Mungu; awezaje binadamu kujua njia ya kwenda? Ni hatari kusema kwa mzaha “Usiahidi kumpa Mungu kitu bila kufikiri, la sivyo utaanza kusikitika baada ya nadhiri yako.” Mfalme mwenye busara huwapepeta waovu; huwaadhibu bila huruma. Dhamiri ya mtu ni taa ya Mwenyezi-Mungu; huchunguza nafsi yake mtu mpaka ndani kabisa. Wema na uaminifu humkinga mfalme; utawala wake huimarishwa kwa uadilifu. Fahari ya vijana ni nguvu zao, uzuri wa vikongwe ni mvi za uzee. Mapigo yanayoumiza ni dawa ya kuondoa uovu; viboko husafisha nafsi mpaka ndani kabisa.
Methali 20:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima. Utisho wa mfalme ni kama ngurumo ya simba; Amkasirishaye huitendea dhambi nafsi yake. Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana. Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu. Mashauri ya moyoni ni kama kilindi; Lakini mtu mwenye ufahamu atayateka. Wanadamu hutangaza kila mtu hisani yake mwenyewe; Bali mtu aliye mwaminifu, ni nani awezaye kumpata? Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake. Mfalme aketiye katika kiti cha hukumu, Huyapepeta mabaya yote kwa macho yake. Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; Nimetakasika dhambi yangu? Vipimo mbalimbali, na pishi mbalimbali, Vyote viwili ni chukizo kwa BWANA. Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili. Sikio lisikialo, na jicho lionalo, BWANA ndiye aliyeyafanya yote mawili. Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula. Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi; Lakini akiisha kwenda zake hujisifu. Dhahabu iko, na marijani tele; Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni. Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu; Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe. Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita. Mwenye udaku hufunua siri; Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana. Amlaaniye babaye au mamaye, Taa yake itazimika katika giza kuu. Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa. Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee BWANA, naye atakuokoa. Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa BWANA; Tena mizani ya hila si njema. Mwenendo wa mtu watoka kwa BWANA; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake? Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuulizauliza habari. Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki; Naye hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao. Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake. Fadhili na uaminifu humhifadhi mfalme, Na kiti chake cha enzi huthibitishwa kwa fadhili. Fahari ya vijana ni nguvu zao, Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi. Machubuko ya fimbo husafisha uovu, Na mapigo hufikia ndani ya mtima.
Methali 20:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima. Utisho wa mfalme ni kama ngurumo ya simba; Amkasirishaye huitendea dhambi nafsi yake. Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana. Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu. Mashauri ya moyoni ni kama kilindi; Lakini mtu mwenye ufahamu atayateka. Wanadamu hutangaza kila mtu hisani yake mwenyewe; Bali mtu aliye mwaminifu, ni nani awezaye kumpata? Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake. Mfalme aketiye katika kiti cha hukumu, Huyapepeta mabaya yote kwa macho yake. Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; Nimetakasika dhambi yangu? Vipimo mbalimbali, na pishi mbalimbali, Vyote viwili ni chukizo kwa BWANA. Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili. Sikio lisikialo, na jicho lionalo, BWANA ndiye aliyeyafanya yote mawili. Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula. Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi; Lakini akiisha kwenda zake hujisifu. Dhahabu iko, na marijani tele; Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni. Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu; Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe. Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana. Amlaaniye babaye au mamaye, Taa yake itazimika katika giza kuu. Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa. Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee BWANA, naye atakuokoa. Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa BWANA; Tena mizani ya hila si njema. Mwenendo wa mtu watoka kwa BWANA; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake? Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari. Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki; Naye hulipitisha gurudumo la kupuria juu yao. Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake. Fadhili na uaminifu humhifadhi mfalme, Na kiti chake cha enzi huthibitishwa kwa fadhili. Fahari ya vijana ni nguvu zao, Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi. Machubuko ya fimbo husafisha uovu, Na mapigo hufikilia ndani ya mtima.
Methali 20:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima. Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake. Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi, bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana. Mvivu halimi kwa majira; kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama lakini hapati chochote. Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina, lakini mtu mwenye ufahamu huyachota. Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma, bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata? Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake. Mfalme anapoketi kwenye kiti chake cha ufalme kuhukumu, hupepeta ubaya wote kwa macho yake. Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi; mimi ni safi na sina dhambi?” Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, BWANA huchukia vyote viwili. Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili. Masikio yasikiayo na macho yaonayo: BWANA ndiye alivifanya vyote viwili. Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba. “Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake. Kuna dhahabu, na marijani kwa wingi, lakini midomo inayonena maarifa ni kito cha thamani. Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie liwe dhamana kwa ajili ya mgeni. Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe. Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo. Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika, kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi. Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene. Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni. Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!” Mngojee BWANA, naye atakuokoa. BWANA anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi. Hatua za mtu huongozwa na BWANA. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe? Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake. Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu, hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao. Taa ya BWANA huchunguza roho ya mwanadamu, huchunguza utu wake wa ndani. Upendo na uaminifu humweka mfalme salama; kiti chake cha ufalme huwa salama kwa upendo. Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee. Mapigo na majeraha huusafisha ubaya, nayo michapo hutakasa utu wa ndani.