Methali 17:1-17
Methali 17:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Afadhali mkate mkavu kwa amani, kuliko karamu katika nyumba ya ugomvi. Mtumwa mwenye busara atachukua nafasi ya mwana mpumbavu, atapata sehemu ya urithi wa jamaa hiyo. Ubora wa dhahabu ama fedha hupimwa kwa moto, lakini Mwenyezi-Mungu ndiye apimaye mioyo ya watu. Mtenda maovu husikiliza maneno mabaya, mwongo hutegea sikio ulimi mdanganyifu. Anayemdhihaki maskini anamtukana Muumba wake; anayefurahia maafa hatakosa kuadhibiwa. Wazee huwaonea fahari wajukuu zao; watoto huwaonea fahari wazazi wao. Maneno mazuri si kawaida kinywani mwa mpumbavu, sembuse maneno ya uongo kinywani mwa kiongozi! Kwa mhongaji, hongo ni kama hirizi; kila afanyacho hufanikiwa. Anayesamehe makosa hujenga urafiki, lakini anayekumbusha makosa hutenga rafiki. Onyo kwa mwenye busara lina maana, kuliko mapigo mia kwa mpumbavu. Afanyalo mtu mwovu ni kuasi tu; mjumbe mkatili atatumwa dhidi yake. Afadhali kukutana na dubu jike aliyenyanganywa watoto wake, kuliko kukutana na mpumbavu katika upumbavu wake. Mwenye kulipiza mema kwa mabaya, mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Kuanzisha ugomvi ni kama kufanya ufa kwenye bwawa; achana na ugomvi kabla haujafurika. Kumsamehe mwenye hatia na kumwadhibu asiye na hatia yote mawili ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu. Ya nini mpumbavu kuwa na fedha mkononi kununulia hekima, wakati yeye mwenyewe hana akili? Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote, ndugu huzaliwa asaidie wakati wa taabu.
Methali 17:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi. Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu. Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu; Bali BWANA huijaribu mioyo. Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara. Amchekaye maskini humtukana Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu. Wana wa wana ndio taji la wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao. Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Sembuse midomo ya uongo kinywani mwa mkuu. Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa. Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye afichuaye siri hutenga rafiki. Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake. Afadhali mtu akutwe na dubu jike aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika. Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA. Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.
Methali 17:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi. Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu. Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Bali BWANA huijaribu mioyo. Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara. Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu. Wana wa wana ndio taji ya wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao. Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu. Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa. Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki. Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake. Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika. Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA. Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.
Methali 17:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi. Mtumishi mwenye hekima atamtawala mwana aaibishaye, naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu. Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu, bali BWANA huujaribu moyo. Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya; mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara. Yeye anaye mdhihaki maskini huonesha dharau kwa Muumba wake; yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa. Wana wa wana ni taji la wazee, nao wazazi ni fahari ya watoto wao. Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu: je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala! Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; kokote kigeukiapo, hufanikiwa. Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo, bali yeyote arudiaye jambo huwatenganisha rafiki wa karibu. Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua kuliko mapigo mia kwa mpumbavu. Mwovu hupenda kuasi tu; mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake. Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyangʼanywa watoto wake, kuliko mpumbavu katika upumbavu wake. Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema, kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake. Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji; kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza. Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki, naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki: BWANA huwachukia sana wote wawili. Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu, wakati yeye hana haja ya kupata hekima? Rafiki hupenda wakati wote naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.