Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Methali 14:1-17

Methali 14:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, bali mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe. Yeye ambaye njia zake ni nyofu humcha BWANA, bali yeye ambaye njia zake zimepotoka humdharau Mungu. Mazungumzo ya mpumbavu huleta fimbo mgongoni mwake, bali mwenye hekima hulindwa na maneno ya midomo yake. Pale ambapo hakuna mafahali, hori ni tupu, bali kutokana na nguvu za fahali huja mavuno mengi. Shahidi mwaminifu hadanganyi, bali shahidi wa uongo humimina uongo. Mwenye mzaha huitafuta hekima na haipati, bali maarifa huja kwa urahisi kwa anayepambanua. Kaa mbali na mtu mpumbavu, kwa maana hutapata maarifa katika midomo yake. Hekima ya mwenye busara ni kufikiria njia zake, bali upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu. Wapumbavu hudhihaki kujirekebisha kutoka dhambi, bali wema hupatikana miongoni mwa wanyofu. Kila moyo hujua uchungu wake wenyewe, wala hakuna yeyote awezaye kushiriki furaha yake. Nyumba ya mwovu itaangamizwa, bali hema la mnyofu litastawi. Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu, bali mwisho wake huelekeza mautini. Hata katika kicheko moyo unaweza kuuma, nayo furaha yaweza kuishia katika majonzi. Wasio na imani watapatilizwa kikamilifu kwa ajili ya njia zao, naye mtu mwema atapewa thawabu kwa ajili ya njia yake. Mtu mjinga huamini kila kitu, bali mwenye busara hufikiria hatua zake. Mtu mwenye hekima humcha BWANA na kuepuka mabaya, bali mpumbavu hukasirika kwa hamaki na uzembe. Mtu anayekasirika kwa haraka hufanya mambo ya upumbavu, naye mtu wa hila huchukiwa.

Shirikisha
Soma Methali 14