Wafilipi 3:7-16
Wafilipi 3:7-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo. Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani. Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake, nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu. Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu. Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa.
Wafilipi 3:7-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, niliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yoyote kuufikia ufufuo wa wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikie tuzo la thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuende katika lilo hilo.
Wafilipi 3:7-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo.
Wafilipi 3:7-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe inayopatikana kwa sheria, bali ile inayopatikana kwa imani katika Kristo, haki ile inayotoka kwa Mungu kupitia kwa imani. Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu. Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele. Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu. Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo. Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia.