Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wafilipi 3:4-14

Wafilipi 3:4-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Mimi pia ningeweza kuyathamini hayo mambo ya nje; na kama yupo mtu anayefikiri kwamba anaweza kuyathamini hayo mambo ya nje, mimi ninayo sababu kubwa zaidi ya kufikiri hivyo: Mimi nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kwangu; mimi ni wa taifa la Israeli, kabila la Benyamini, Mwebrania halisi. Kuhusu kuizingatia sheria mimi nilikuwa Mfarisayo, na nilikuwa na bidii sana hata nikalidhulumu kanisa. Kuhusu uadilifu unaopatikana kwa kuitii sheria, mimi nilikuwa bila hatia yoyote. Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo. Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani. Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake, nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu. Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu.

Shirikisha
Soma Wafilipi 3

Wafilipi 3:4-14 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)

ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili. Kama mtu yeyote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi. Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya Torati, ni Farisayo, kwa habari ya juhudi, nilikuwa nikitesa jumuiya ya waumini, kuhusu haki inayopatikana kwa Torati, sikuwa na hatia. Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Al-Masihi. Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi cha kumjua Al-Masihi Isa Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Al-Masihi. Nami nionekane mbele zake bila kuwa na haki yangu mwenyewe inayopatikana kwa sheria, bali ile inayopatikana kwa imani katika Al-Masihi, haki ile inayotoka kwa Mungu kupitia kwa imani. Nataka nimjue Al-Masihi na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, ili kwa njia yoyote niweze kufikia ufufuo wa wafu. Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Al-Masihi Isa. Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele. Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Al-Masihi Isa.

Shirikisha
Soma Wafilipi 3