Wafilipi 3:12-21
Wafilipi 3:12-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu. Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa. Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo. Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo. Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia. Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake.
Wafilipi 3:12-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikie tuzo la thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuende katika lilo hilo. Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi huenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao uko katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.
Wafilipi 3:12-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo. Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo; mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.
Wafilipi 3:12-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Al-Masihi Isa. Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele. Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Al-Masihi Isa. Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo. Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia. Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea. Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Al-Masihi. Mwisho wa watu hao ni maangamizi, mungu wao ni tumbo, na utukufu wao ni aibu, na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia. Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani Bwana Isa Al-Masihi, atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.