Wafilipi 1:12-26
Wafilipi 1:12-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mambo yote yaliyonipata yamesaidia sana kuieneza Injili. Kutokana na hayo, walinzi wote wa ikulu pamoja na wengine wote hapa wanafahamu kwamba niko kifungoni kwa sababu mimi namtumikia Kristo. Na huku kuweko kwangu kifungoni kumewafanya ndugu wengi kuwa na imani kwa Bwana, hata wanazidi kuwa hodari katika kuutangaza ujumbe wa Mungu bila hofu. Kweli, baadhi yao wanamhubiri Kristo kwa sababu wana wivu na ni watu wagomvi; lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia nzuri. Hawa wanafanya hivyo kwa upendo, kwani wanajua kwamba Mungu amenipa jukumu hili la kuitetea Injili. Hao wengine wanamtangaza Kristo kwa mashindano na si kwa moyo mnyofu, wakidhani kwamba wataniongezea mateso yangu kifungoni. Haidhuru! Mimi nafurahi ikiwa tu watu wanamhubiri Kristo kwa kila njia, iwe ni kwa nia nzuri au kwa nia mbaya. Tena nitaendelea kufurahi, kwani najua kwamba kwa sala zenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo, nitakombolewa. Hamu yangu kubwa na tumaini langu ni kwamba kwa vyovyote sitashindwa katika kutimiza wajibu wangu, bali nitakuwa na moyo thabiti kila wakati na hasa wakati huu, ili kwa maisha yangu yote, niwapo hai au nikifa, nimpatie Kristo heshima. Kwangu, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida zaidi. Lakini, kama kwa kuishi nitaweza kufanya kazi yenye faida zaidi, basi, sijui nichague lipi! Nakabiliwa na haya mawili yaliyo sawa. Natamani kuyaacha maisha haya nikakae pamoja na Kristo, jambo ambalo ni bora zaidi; lakini ni jambo la maana zaidi kwenu kama nikiendelea kuishi. Nina hakika ya jambo hili, na hivyo najua kwamba nitaendelea kuishi pamoja nanyi nyote, ili nipate kuongeza maendeleo yenu na furaha katika imani. Basi, nitakapokuwa nanyi tena mtakuwa na sababu ya kuona fahari juu yangu katika kuungana na Kristo Yesu.
Wafilipi 1:12-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili; hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia. Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu. Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema. Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili; bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu. Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi. Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo; kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa uthabiti wote, kama sikuzote na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani; hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena.
Wafilipi 1:12-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili; hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia. Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu. Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema. Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili; bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu. Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi. Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo; kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa uthabiti wote, kama sikuzote na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu. Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani; hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena.
Wafilipi 1:12-26 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili. Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Al-Masihi. Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana Isa wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga. Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Al-Masihi kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Al-Masihi kwa nia njema. Hawa wa mwisho wanamhubiri Al-Masihi kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili. Hao wa kwanza wanamtangaza Al-Masihi kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu. Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Al-Masihi anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi. Naam, nami nitaendelea kufurahi, kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Isa Al-Masihi, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu. Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Al-Masihi atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa. Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Al-Masihi, na kufa ni faida. Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini nichague lipi? Mimi sijui! Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Al-Masihi, jambo hilo ni bora zaidi. Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili. Nikiwa na hakika ya jambo hili, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani, ili kwa kuja kwangu kwenu tena, furaha yenu iwe nyingi katika Al-Masihi Isa kwa ajili yangu.