Filemoni 1:8-21
Filemoni 1:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia. Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe. Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili. Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika. Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: Yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana. Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe. Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi. Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako). Naam, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo. Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.
Filemoni 1:8-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa sababu hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ndimi, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa nikiwa kifungoni mwangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nilitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako, niwapo katika kifungo kwa ajili ya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lolote isipokuwa kwa ushauri wako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi ikiwa waniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama ambavyo ungenipokea mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamdai kitu, ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakudai hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nifaidi kwa hili katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo. Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo.
Filemoni 1:8-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo. Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo.
Filemoni 1:8-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningekuwa na ujasiri wa kukuagiza yale yakupasayo kutenda, lakini ninakuomba kwa upendo. Mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu, nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo. Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia. Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa. Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili. Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari. Huenda sababu ya Onesimo kutengwa nawe kwa muda ni ili uwe naye daima, si kama mtumwa sasa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana. Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika nawe, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe. Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi. Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa hilo deni. Kumbuka kwamba nakudai hata nafsi yako. Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, yaani uniburudishe moyo wangu katika Kristo. Huku nikiwa na hakika ya kutii kwako, nakuandikia nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.