Filemoni 1:4-12
Filemoni 1:4-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu, maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu. Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni. Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia. Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.
Filemoni 1:4-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; naomba ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nilikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa sababu hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ndimi, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa nikiwa kifungoni mwangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa
Filemoni 1:4-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa
Filemoni 1:4-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku zote ninamshukuru Mungu wangu ninapokukumbuka katika maombi yangu, kwa sababu ninasikia kuhusu imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. Naomba utiwe nguvu katika kushiriki imani yako na wengine, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu wa kila kitu chema tunachoshiriki kwa ajili ya Kristo. Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu. Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningekuwa na ujasiri wa kukuagiza yale yakupasayo kutenda, lakini ninakuomba kwa upendo. Mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu, nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo. Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia. Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.