Filemoni 1:1-10
Filemoni 1:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu, na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkipo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kila wakati ninaposali, nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu, maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu. Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo. Ndugu, upendo wako umeniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu. Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika kuungana na Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya. Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake. Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.
Filemoni 1:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi, na kwa Afia, dada yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; naomba ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nilikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa sababu hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ndimi, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa nikiwa kifungoni mwangu, yaani, Onesimo
Filemoni 1:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi, na kwa Afia, ndugu yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo
Filemoni 1:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu. Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu, kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako. Neema na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi. Siku zote ninamshukuru Mungu wangu ninapokukumbuka katika maombi yangu, kwa sababu ninasikia kuhusu imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. Naomba utiwe nguvu katika kushiriki imani yako na wengine, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu wa kila kitu chema tunachoshiriki kwa ajili ya Kristo. Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu. Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningekuwa na ujasiri wa kukuagiza yale yakupasayo kutenda, lakini ninakuomba kwa upendo. Mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu, nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.