Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 9:1-14

Hesabu 9:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mnamo mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri, Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose katika jangwa la Sinai. Alimwambia: “Waisraeli sharti waiadhimishe sikukuu ya Pasaka wakati uliopangwa. Hii itakuwa siku ya kumi na nne ya mwezi huu; wakati wa jioni watafanya hivyo kufuatana na masharti na maagizo yake yote.” Kwa hiyo, Mose akawaambia watu kwamba wanapaswa kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka. Basi, wakaiadhimisha Pasaka jioni, siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, katika jangwa la Sinai. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Lakini, baadhi ya watu waliokuwapo walikuwa hawawezi kuiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka kwa sababu walikuwa wamegusa maiti, wakawa najisi. Hao waliwaendea Mose na Aroni, wakawaambia, “Sisi tu najisi kwa kuwa tumegusa maiti, lakini kwa nini tukatazwe kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka zake kwa wakati uliopangwa pamoja na Waisraeli wengine?” Mose akawajibu, “Ngojeni mpaka hapo nitakapopata maagizo juu yenu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mmoja wenu au mmoja wa wazawa wenu akiwa najisi kwa sababu amegusa maiti au akiwa mbali safarini, lakini akiwa anataka kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu kama huyo anaruhusiwa kufanya hivyo mwezi mmoja baadaye, jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Ataiadhimisha kwa kula mikate isiyotiwa chachu na mboga chungu. Wasibakize chakula chochote hadi asubuhi, wala wasivunje hata mfupa mmoja wa wanyama wa Pasaka. Wataiadhimisha sikukuu hii ya Pasaka kulingana na kanuni zake zote. Lakini mtu yeyote ambaye ni safi au hayumo safarini, asipoiadhimisha sikukuu ya Pasaka, atatengwa na watu wake kwa kuwa hakunitolea sadaka kwa wakati uliopangwa. Ni lazima aadhibiwe kwa ajili ya dhambi yake. “Ikiwa kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi na anapenda kuiadhimisha sikukuu ya Pasaka, mtu huyo sharti afanye hivyo kulingana na masharti na maagizo yote ya Pasaka. Kila mtu atafuata masharti yaleyale, akiwa mgeni au mwenyeji.”

Shirikisha
Soma Hesabu 9

Hesabu 9:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha BWANA akanena na Musa katika bara ya Sinai, mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri, akamwambia, Tena, wana wa Israeli na waadhimishe sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa. Siku ya kumi na nne ya mwezi huu, wakati wa jioni, mtaiadhimisha kwa wakati wake ulioagizwa; kwa amri zake zote, na kama hukumu zake zote zilivyo, ndivyo mtakavyoisherehekea. Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli kwamba waadhimishe sikukuu hiyo ya Pasaka; Nao wakaiadhmisha Pasaka katika mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, katika bara ya Sinai vile vile kama hayo yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Basi walikuwako wanaume kadhaa waliokuwa na unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu, hata wasiweze kuishika Pasaka siku hiyo; nao wakaenda mbele ya Musa na Haruni, siku hiyo hao watu wakamwambia, Sisi tuko katika hali ya unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu; nasi tumezuiwa kwa nini hata tusipate kumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioagizwa, kati ya wana wa Israeli? Musa akawaambia, Ngojeni hapo; hata nipate sikiza BWANA atakaloagiza juu yenu. BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na wana wa Israeli, kuwaambia, Mtu wa kwenu, au wa vizazi vyenu, yeyote atakayekuwa na unajisi kwa ajili ya maiti, au akiwako mbali katika safari, na haya yote, ataishika Pasaka kwa BWANA; mwezi wa pili, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, wataishika; watamla pamoja na mikate isiyotiwa chachu na mboga za uchungu; wasisaze kitu chake chochote hadi asubuhi, wala wasimvunje mfupa wake; kama hiyo sheria yote ya Pasaka ilivyo ndivyo watakavyoishika. Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atatengwa na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake. Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa BWANA; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi.

Shirikisha
Soma Hesabu 9

Hesabu 9:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha BWANA akanena na Musa katika bara ya Sinai, mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri, akamwambia, Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa. Siku ya kumi na nne ya mwezi huu, wakati wa jioni, mtaishika kwa wakati wake ulioagizwa; kwa amri zake zote, na kama hukumu zake zote zilivyo, ndivyo mtakavyoishika. Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli kwamba waishike sikukuu hiyo ya Pasaka; Nao wakaishika Pasaka katika mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, katika bara ya Sinai vile vile kama hayo yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Basi walikuwako watu waume kadha wa kadha waliokuwa na unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu, hata wasiweze kuishika Pasaka siku hiyo; nao wakaenda mbele ya Musa na Haruni, siku hiyo hao watu wakamwambia, Sisi tu hali ya unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu; nasi tumezuiwa kwa nini hata tusipate kumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioagizwa, kati ya wana wa Israeli? Musa akawaambia, Ngojeni hapo; hata nipate sikiza BWANA atakaloagiza juu yenu. BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na wana wa Israeli, kuwaambia, Mtu wa kwenu, au wa vizazi vyenu, ye yote atakayekuwa na unajisi kwa ajili ya maiti, au akiwako mbali katika safari, na haya yote, ataishika Pasaka kwa BWANA; mwezi wa pili, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, wataishika; watamla pamoja na mikate isiyotiwa chachu na mboga za uchungu; wasisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, wala wasimvunje mfupa wake; kama hiyo sheria yote ya Pasaka ilivyo ndivyo watakavyoishika. Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea BWANA matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake. Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa BWANA; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi.

Shirikisha
Soma Hesabu 9

Hesabu 9:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA akasema na Musa katika Jangwa la Sinai katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka Misri. Akasema, “Waamuru Waisraeli waadhimishe Pasaka katika wakati ulioamriwa. Adhimisheni wakati ulioamriwa, yaani wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi huu, kulingana na desturi zake zote na masharti yake.” Hivyo Musa akawaambia Waisraeli waiadhimishe Pasaka, nao wakafanya hivyo kwenye Jangwa la Sinai wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. Waisraeli wakafanya kila kitu kama vile BWANA alivyomwamuru Musa. Lakini baadhi yao hawakuweza kuadhimisha Pasaka siku ile kwa sababu walikuwa najisi kwa ajili ya kugusa maiti. Kwa hiyo wakamwendea Musa na Haruni siku ile ile, wakamwambia Musa, “Tumekuwa najisi kwa sababu tumegusa maiti, lakini kwa nini tuzuiliwe kumtolea BWANA sadaka yake pamoja na Waisraeli wengine katika wakati ulioamriwa?” Musa akawajibu, “Ngojeni hadi nitafute kile BWANA anachoagiza kuwahusu ninyi.” Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Waambie Waisraeli: ‘Mmoja wenu au wazao wenu wanapokuwa najisi kwa sababu ya maiti au wakiwa safarini, hata hivyo wanaweza kuadhimisha Pasaka ya BWANA. Wataiadhimisha wakati wa kuzama jua siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Watamla mwana-kondoo, pamoja na mkate usiotiwa chachu, na mboga chungu. Wasibakize chochote hadi asubuhi wala wasivunje mifupa ya mwana-kondoo. Wanapoiadhimisha Pasaka, hawana budi kufuata masharti yote. Lakini mtu aliyetakasika na hayuko safarini asipoiadhimisha Pasaka, mtu huyo hana budi kukatiliwa mbali na watu wake kwa sababu hakutoa sadaka ya BWANA kwa wakati ulioamriwa. Mtu huyo atawajibika kubeba matokeo ya dhambi yake. “ ‘Mgeni anayeishi miongoni mwenu ambaye anataka kuiadhimisha Pasaka ya BWANA, lazima afanye hivyo kwa kufuata desturi na masharti. Lazima masharti yawe sawasawa kwa mgeni na mzawa.’ ”

Shirikisha
Soma Hesabu 9