Hesabu 36:1-13
Hesabu 36:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Viongozi wa jamaa katika ukoo wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, mwana wa Yosefu, walikwenda kuzungumza na Mose na viongozi wengine wa koo za Waisraeli. Wakasema, “Bwana wetu, Mwenyezi-Mungu alikuamuru kuwagawia watu wa Israeli nchi kwa kura, kuwa urithi wao; alikuamuru pia uwape binti za Selofehadi ndugu yetu urithi wa baba yao. Lakini wao wakiolewa na Waisraeli wa makabila mengine, urithi wao utatoka kwetu na kuwaendea watu wa kabila watakamoolewa; kwa hiyo urithi wetu sisi utapungua. Katika sikukuu ya ukumbusho urithi wao utahesabiwa pamoja na ule wa kabila watakamoolewa na hivyo kabila letu halitapata urithi huo tena.” Basi, Mose akawapa Waisraeli agizo lifuatalo kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, akawaambia, “Watu wa ukoo wa kabila la Yosefu, wamesema ukweli. Na hivi ndivyo anavyoamuru Mwenyezi-Mungu kuhusu binti za Selofehadi; wako huru kuolewa na mtu yeyote wampendaye, lakini waolewe katika kabila lao, ili urithi wa Waisraeli usihamishiwe kwa kabila lingine; kila Mwisraeli atazingatia urithi wa kabila lake. Mwanamke yeyote mwenye urithi katika kabila mojawapo la Israeli ni lazima aolewe na mtu wa kabila lake, ili kila Mwisraeli achukue urithi wa babu zake. Hivyo hapatakuwa na urithi wowote utakaohamishwa kutoka kabila moja hadi jingine. Kila kabila la Waisraeli litashikilia urithi wake.” Binti za Selofehadi walifanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Wote: Mala, Tirza, Hogla, Milka na Noa wakaolewa na binamu zao. Waliolewa katika jamaa za ukoo wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika kabila la baba yao. Hizo ndizo amri na maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli kwa njia ya Mose katika tambarare za Moabu, ngambo ya Mto Yordani karibu na mji wa Yeriko.
Hesabu 36:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wale wakuu wa nyumba za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli; wakasema, BWANA alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi wao; tena bwana wangu aliagizwa na BWANA awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo urithi wa baba yao. Wakiolewa na watu wa wana wa hayo makabila mengine ya wana wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba zetu, na hilo kabila watakalotiwa ndani yake litaongezewa urithi wao; basi urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu. Tena itakapokuwapo hiyo jubilii ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hilo kabila ambalo wamekuwa ndani yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa kabila la baba zetu. Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la BWANA lilivyokuwa, akasema, Kabila la wana wa Yusufu imenena yaliyo haki. BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila la baba zao. Hivyo hapana urithi wowote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hili kwenda kabila hili; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila la baba zake. Na kila binti atakayemiliki urithi katika kabila lolote katika wana wa Israeli, ataolewa katika jamaa moja ya kabila la baba yake, ili wana wa Israeli wapate kumiliki kila mtu urithi wa baba zake. Hivyo hapatakuwa na urithi wowote utakaotoka kabila hili kwenda kabila hili; kwa kuwa makabila ya wana wa Israeli yatashikamana kila mmoja na urithi wake mwenyewe. Basi hao binti za Selofehadi wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa; kwa kuwa Mala, na Tirza, na Hogla, na Milka, na Nuhu, binti za Selofehadi waliolewa na wanaume, wana wa ndugu za baba yao. Waliolewa katika jamaa za wana wa Manase, mwana wa Yusufu, na urithi wao ukakaa katika kabila la jamaa ya baba yao. Haya ndiyo maagizo na hukumu, ambayo BWANA aliwaagiza wana wa Israeli, kwa mkono wa Musa, hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko.
Hesabu 36:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wale wakuu wa nyumba za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli; wakasema, BWANA alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi wao; tena bwana wangu aliagizwa na BWANA awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo urithi wa baba yao. Wakiolewa na watu wa wana wa hizo kabila nyingine za wana wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba zetu, na hiyo kabila watakayotiwa ndani yake itaongezewa urithi wao; basi urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu. Tena itakapokuwapo hiyo yubile ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hiyo kabila ambayo wamekuwa ndani yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa kabila ya baba zetu. Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la BWANA lilivyokuwa, akasema, Kabila ya wana wa Yusufu imenena yaliyo haki. BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao. Hivyo hapana urithi wo wote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila ya baba zake. Na kila binti atakayemiliki urithi katika kabila yo yote katika wana wa Israeli, ataolewa katika jamaa moja ya kabila ya baba yake, ili wana wa Israeli wapate kumiliki kila mtu urithi wa baba zake. Hivyo hapatakuwa na urithi uwao wote utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa kabila za wana wa Israeli zitashikamana kila mmoja na urithi wake mwenyewe. Basi hao binti za Selofehadi wakafanya kama BWANA alivyomwagiza Musa; kwa kuwa Mala, na Tirsa, na Hogla, na Milka, na Noa, binti za Selofehadi waliolewa na waume, wana wa ndugu za baba yao. Waliolewa katika jamaa za wana wa Manase, mwana wa Yusufu, na urithi wao ukakaa katika kabila ya jamaa ya baba yao. Haya ndiyo maagizo na hukumu, ambayo BWANA aliwaagiza wana wa Israeli, kwa mkono wa Musa, hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko
Hesabu 36:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Viongozi wa jamaa ya ukoo wa Gileadi mwana wa Makiri, mwana wa Manase, waliokuwa wametoka katika koo za wazao wa Yusufu, walikuja na kuzungumza mbele ya Musa na viongozi, wakuu wa jamaa ya Waisraeli. Wakasema, “BWANA alipomwamuru bwana wangu kuwapa Waisraeli nchi kama urithi kwa kura, alikuamuru kutoa urithi wa ndugu yetu Selofehadi kwa binti zake. Sasa ikiwa wataolewa na wanaume wa makabila mengine ya Israeli, itakuwa kwamba urithi wao utaondolewa kutoka urithi wa mababu zetu na kuongezwa katika urithi wa kabila ambalo dada hao wameolewa. Kwa hiyo sehemu ya urithi tuliyogawiwa itachukuliwa kutoka kwetu. Mwaka wa Yubile kwa Waisraeli utakapofika, urithi wao utaongezwa kwa lile kabila ambalo wameolewa, na mali yao itaondolewa kutoka urithi wa kabila la mababu zetu.” Ndipo kwa agizo la BWANA Musa akatoa amri ifuatayo kwa Waisraeli: “Kile wazao wa kabila la Yusufu wanachosema ni kweli. Hivi ndivyo BWANA anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu yeyote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila la baba yao. Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake. Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lolote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake. Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.” Kwa hiyo binti za Selofehadi wakafanya kama BWANA alivyomwamuru Musa. Binti za Selofehadi, ambao ni Mahla, Tirsa, Hogla, Milka na Noa, wakaolewa na wana wa ndugu za baba yao. Waliolewa ndani ya koo za wazao wa Manase mwana wa Yusufu, na urithi wao ukabaki katika ukoo na kabila la baba yao. Haya ndio maagizo na masharti ambayo BWANA aliwapa Waisraeli kupitia Musa katika tambarare za Moabu, karibu na Yordani ngʼambo ya Yeriko.