Hesabu 35:9-34
Hesabu 35:9-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose, akamwambia, Waambie Waisraeli kwamba wakati mtakapovuka mto Yordani na kuingia nchini Kanaani, mtachagua miji itakayokuwa miji ya makimbilio ambamo kama mtu akimuua mwenzake bila kukusudia ataweza kukimbilia. Miji hiyo itakuwa mahali pa kukimbilia usalama ili huyo mwuaji asiuawe na mwenye kulipiza kisasi kabla ya kuhukumiwa na jumuiya. Mtajitengea miji sita kwa ajili ya makimbilio. Kati ya miji hiyo sita mtakayoitenga, mitatu iwe mashariki ya Yordani, na mitatu iwe katika nchi ya Kanaani. Miji hii itakuwa ya makimbilio kwa ajili ya Waisraeli na wageni wa kudumu au wa muda wanaokaa pamoja nao. Mtu yeyote akimuua mwingine bila kukusudia anaweza kukimbilia huko. “Lakini mtu akimpiga mwenzake kwa kitu cha chuma, akafa, mtu huyo ni mwuaji na ni lazima auawe. Mtu yeyote akimpiga mwenzake kwa jiwe, akifa, mtu huyo ni mwuaji, na lazima auawe. Kama akimpiga mwenzake kwa silaha ya mti ambayo yaweza kusababisha kifo, akafa, mtu huyo ni mwuaji, na ni lazima auawe. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi. Huyu atakapokutana na huyo mwuaji, atatekeleza hukumu ya kifo. “Hali kadhalika, kama mtu anamchukia mwenzake halafu, akamsukuma au kumtupia kitu kwa kumvizia, au kwa kumpiga ngumi akafa, basi mtu huyo aliyempiga mwenzake ni mwuaji na ni lazima auawe. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi atakapokutana naye. “Lakini kama mtu akimsukuma mwenzake kwa ghafla bila chuki au kumtupia kitu bila kumvizia au mtu akirusha jiwe linaloweza kusababisha kifo, akamuua mtu bila kukusudia, ingawa hakuwa adui yake wala hakutaka kumdhuru, basi, jumuiya itaamua kati ya huyo mwuaji na jamaa ya mtu aliyeuawa anayetaka kulipiza kisasi, kulingana na sheria hizi. Jumuiya itamwokoa mtu huyo aliyeua mikononi mwa jamaa ya mtu aliyeuawa, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alimokuwa amekimbilia. Atakaa huko mpaka kifo cha kuhani mkuu wa wakati huo aliyeteuliwa kwa kupakwa mafuta matakatifu. Lakini huyo aliyeua akitoka nje ya mji aliokimbilia wakati wowote ule, halafu jamaa ya mtu aliyeuawa akampata nje ya mipaka ya mji huo wa makimbilio akamuua, huyo hatakuwa na hatia ya kuua. Maana huyo aliyeua ni lazima akae ndani ya mji wa makimbilio mpaka kuhani mkuu atakapofariki; lakini baada ya kifo cha kuhani mkuu anaweza kurudi nyumbani. “Sheria hizi zitatumika katika vizazi vyenu vyote, mahali popote mtakapokaa. “Mtu yeyote atakayeua mtu, atahukumiwa kifo kutokana na ushahidi wa mashahidi wawili au zaidi; mtu yeyote hawezi kuhukumiwa kifo kutokana na ushahidi wa mtu mmoja. “Msipokee fidia yoyote kuokoa maisha ya mwuaji aliyepatikana na hatia, akahukumiwa kifo; mtu huyo lazima auawe. Msipokee wala msikubali fidia yoyote kutoka kwa mtu aliyekimbilia mji wa makimbilio ili kumruhusu arudi kukaa nyumbani kwake kabla ya kifo cha kuhani mkuu. Mkifanya hivyo mtakuwa mnaitia unajisi nchi ambayo mnakaa. Umwagaji damu huitia nchi unajisi, na hakuna sadaka iwezayo kuitakasa nchi iliyofanyiwa mauaji isipokuwa kwa kumuua mwuaji huyo. Msiitie unajisi nchi ambayo mnakaa, nchi ambayo mimi ninakaa; maana mimi Mwenyezi-Mungu ninakaa miongoni mwenu Waisraeli.”
Hesabu 35:9-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, Ndipo mtajiwekea miji itakayokuwa ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kulipiza kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya kukimbilia. Mtawapa miji mitatu ng'ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio. Miji hiyo sita itakuwa pa kukimbilia usalama kwa ajili ya wana wa Israeli, kwa ajili ya mgeni na kwa ajili ya aishiye nao kama mgeni; ili kila amwuaye mtu, bila kukusudia kuua, apate mahali pa kukimbilia. Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa. Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa. Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua. Tena kama alimsukuma kwa kumchukia au kama alimtupia kitu kwa kumvizia, hadi akafa; au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye. Lakini ikiwa alimsukuma ghafla pasipo kumchukia; au akamtupia kitu chochote pasipo kumvizia, au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, bila kumwona akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara; ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayelipiza kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo; nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu; tena mkutano utamrejesha katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta matakatifu. Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wowote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia; na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yuko nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu; kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hadi kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake. Mambo haya yatakuwa ni amri ya hukumu kwenu, katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu yote. Mtu yeyote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu akauliwa. Tena, msipokee fidia kwa ajili ya uhai wa mwuaji, ambaye amekuwa na hatia ya mauti; Lakini lazima atauawa. Tena hamtapokea fidia kwa ajili ya huyo aliyeukimbilia mji wake wa makimbilio, apate kwenda tena kukaa katika nchi, hata kifo cha kuhani mkuu. Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga. Kwa hiyo msiitie unajisi nchi mwishiyo ambayo nami nakaa kati yake; kwa kuwa mimi BWANA nakaa kati ya wana wa Israeli.
Hesabu 35:9-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio. Mtawapa miji mitatu ng’ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio. Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa. Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa. Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua. Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa; au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye. Lakini ikiwa alimsukuma ghafula pasipo kumchukia; au akamtupia kitu cho chote pasipo kumvizia, au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, asipomwona, akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara; ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayetwaa kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo; nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kutwaa kisasi cha damu; tena mkutano utamrejeza katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta kwa mafuta matakatifu. Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wo wote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia; na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yu nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu; kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hata kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake. Mambo haya yatakuwa ni amri ya hukumu kwenu, katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu yote. Mtu awaye yote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu hata akafa. Tena, msipokee fidia kwa ajili ya uhai wa mwuaji, ambaye amekuwa na hatia ya mauti; Lakini lazima atauawa. Tena hamtapokea fidia kwa ajili ya huyo aliyeukimbilia mji wake wa makimbilio, apate kwenda tena kuketi katika nchi, hata kifo cha kuhani mkuu. Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga. Kwa hiyo msiitie unajisi nchi muiketiyo, ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi BWANA nakaa kati ya wana wa Israeli.
Hesabu 35:9-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha BWANA akamwambia Musa: “Sema na Waisraeli, uwaambie: ‘Mtakapovuka Yordani kuingia Kanaani, chagueni baadhi ya miji iwe miji yenu ya makimbilio, ambayo mtu ambaye ameua mwenzake bila kukusudia aweza kukimbilia humo. Itakuwa mahali pa kukimbilia kutoka mlipiza kisasi, ili mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji asife kabla ya kujitetea mbele ya mkutano. Miji hii sita mtakayoitoa itakuwa miji yenu ya makimbilio. Mtatoa miji mitatu ngʼambo hii ya Yordani na miji mingine mitatu upande wa Kanaani kama miji ya makimbilio. Miji hii sita itakuwa mahali pa makimbilio kwa ajili ya Waisraeli, wageni na watu wengine wanaoishi kati yenu, ili mtu ambaye ameua mtu mwingine pasipo kukusudia aweze kukimbilia humo. “ ‘Kama mtu akimpiga mwenzake kwa chuma naye mtu huyo akafa, mtu huyo ni muuaji; muuaji sharti atauawa. Au kama mtu analo jiwe mkononi mwake, naye akampiga mwenzake nalo akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa. Au kama mtu ana chombo cha mti mkononi mwake ambacho chaweza kuua, naye akampiga mwenzake akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa. Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji; wakati akikutana naye, atamuua. Ikiwa mtu ana chuki ya siku nyingi na mwenzake akamsukuma au akamtupia kitu kwa kukusudia naye akafa, au ikiwa katika uadui akampiga ngumi naye akafa, mtu yule sharti atauawa; yeye ni muuaji. Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji atakapokutana naye. “ ‘Lakini kama mtu akimsukuma mwenziwe ghafula pasipo chuki, au kumtupia kitu pasipo kukusudia, au, pasipo kumwona, akimwangushia jiwe ambalo laweza kumuua naye akafa, basi kwa kuwa hakuwa adui yake naye hakukusudia kumuumiza, kusanyiko lazima waamue kati yake na mlipiza kisasi wa damu kufuatana na sheria hizi. Kusanyiko lazima wamlinde yule anayeshtakiwa kuua kutoka kwa mlipiza kisasi wa damu, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alikokuwa amekimbilia. Lazima akae humo hadi atakapokufa kuhani mkuu aliyekuwa amepakwa mafuta matakatifu. “ ‘Lakini kama mshtakiwa atatoka nje ya mipaka ya mji wa makimbilio ambao amekimbilia, na mlipiza kisasi wa damu akamkuta nje ya mji, mlipiza kisasi wa damu anaweza kumuua mshtakiwa huyo bila kuwa na hatia ya kuua. Mshtakiwa lazima akae katika mji wake wa makimbilio hadi atakapokufa kuhani mkuu; atarudi tu kwenye mali yake baada ya kifo cha kuhani mkuu. “ ‘Hizi ndizo kanuni za sheria zitakazohitajiwa kwenu na katika vizazi vyenu vijavyo, popote mtakapoishi. “ ‘Yeyote anayeua mtu atauawa kama muuaji ikiwa tu kuna ushuhuda wa mashahidi. Lakini hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu. “ ‘Usikubali fidia yoyote ya kuokoa uhai wa muuaji ambaye anastahili kufa. Mtu huyo hakika lazima auawe. “ ‘Usikubali fidia ya mtu ambaye amekimbilia katika mji wa makimbilio, na hivyo kumruhusu kurudi kuishi katika nchi yake kabla ya kifo cha kuhani mkuu. “ ‘Msiinajisi nchi mnayoishi. Umwagaji damu hunajisi nchi, na upatanisho hauwezekani kufanyika katika nchi ambayo damu imemwagwa, isipokuwa tu kwa damu ya yule aliyeimwaga damu. Msiinajisi nchi mnayoishi, ambayo nami ninakaa, kwa kuwa Mimi, BWANA, ninakaa katikati ya Waisraeli.’ ”