Hesabu 27:18-23
Hesabu 27:18-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono, na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo. Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii. Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.” Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alimtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote ya Waisraeli. Kisha akamwekea mikono kichwani na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu.
Hesabu 27:18-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu ambaye roho iko ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya jumuiya yote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili jumuiya yote ya wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama BWANA alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya jumuiya yote; kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama BWANA alivyosema kwa mkono wa Musa.
Hesabu 27:18-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama BWANA alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama BWANA alivyosema kwa mkono wa Musa.
Hesabu 27:18-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo BWANA akamwambia Musa, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho yuko ndani yake, uweke mkono juu yake. Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao. Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli wapate kumtii. Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za BWANA kwa Urimu. Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.” Musa akafanya kama BWANA alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote. Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile BWANA alivyoelekeza kupitia kwa Musa.