Hesabu 27:12-23
Hesabu 27:12-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda juu ya Mlima huu wa miinuko ya Abarimu uitazame nchi ambayo nimewapa Waisraeli. Ukisha iona, nawe pia utafariki kama ndugu yako Aroni alivyofariki, kwa sababu hamkuitii amri yangu kule jangwani Sini. Wakati jumuiya yote ya watu walipolalamika juu yangu kule Meriba, hamkuacha utukufu wangu uonekane mbele yao walipotaka wapewe maji.” (Meriba ni chemchemi ya maji ya Kadeshi katika jangwa la Sini). Naye Mose akamwomba Mwenyezi-Mungu, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu uliye asili ya uhai wote, nakuomba umteue mtu wa kuisimamia jumuiya hii, ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasio na mchungaji.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono, na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo. Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii. Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.” Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alimtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote ya Waisraeli. Kisha akamwekea mikono kichwani na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu.
Hesabu 27:12-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli. Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika; kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.) Musa akanena na BWANA akisema, BWANA, Mungu wa roho za watu wote, na aweke mtu juu ya kusanyiko, atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili watu wa BWANA wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu ambaye roho iko ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya jumuiya yote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili jumuiya yote ya wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama BWANA alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya jumuiya yote; kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama BWANA alivyosema kwa mkono wa Musa.
Hesabu 27:12-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli. Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika; kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.) Musa akanena na BWANA akisema, BWANA, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano, atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa BWANA wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za BWANA; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama BWANA alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama BWANA alivyosema kwa mkono wa Musa.
Hesabu 27:12-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Kwea mlima huu katika safu za Abarimu uione nchi ninayowapa Waisraeli. Baada ya kuiona, wewe pia utakusanywa pamoja na watu wako kama ndugu yako Haruni alivyokusanywa, kwa kuwa jumuiya ilipoasi amri yangu kwenye maji katika Jangwa la Sini, wakati jumuiya ilipogombana nami, nyote wawili mliacha kuitii amri yangu ya kuniheshimu kama mtakatifu mbele ya macho yao.” (Haya yalikuwa maji ya Meriba huko Kadeshi, katika Jangwa la Sini.) Musa akamwambia BWANA, “BWANA, Mungu wa roho zote za wanadamu, na amteue mtu juu ya jumuiya hii ili atoke na kuingia mbele yao, atakayewaongoza katika kutoka kwao na kuingia kwao, ili watu wa BWANA wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.” Kwa hiyo BWANA akamwambia Musa, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho yuko ndani yake, uweke mkono juu yake. Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao. Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli wapate kumtii. Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za BWANA kwa Urimu. Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.” Musa akafanya kama BWANA alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote. Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile BWANA alivyoelekeza kupitia kwa Musa.