Hesabu 24:1-25
Hesabu 24:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa Balaamu alitambua kwamba Mwenyezi-Mungu alipenda kuwabariki Waisraeli, kwa hiyo hakwenda kupiga bao tena, akawa anaangalia jangwani. Alitazama juu akawaona Waisraeli wamepiga kambi, kila kabila mahali pake. Kisha roho ya Mungu ikamjia, naye akatamka kauli hii ya kinabii: Kauli yangu mimi Balaamu mwana wa Peori kauli ya mtu aliyefumbuliwa macho; kauli ya mtu aliyesikia maneno ya Mungu mtu aliyeona maono ya Mungu Mwenye Nguvu, mtu anayesujudu na kuona wazi. Hema zako zapendeza namna gani enyi watu wa Yakobo; naam, kambi zenu enyi watu wa Israeli! Ni kama mabonde yanayotiririka maji, kama bustani kandokando ya mto, kama mishubiri aliyopanda Mwenyezi-Mungu, kama mierezi kandokando ya maji. Watakuwa na hazina ya kutosha ya maji, mbegu yao itapata maji mengi, mfalme wao atakuwa mkuu kuliko Agagi, na ufalme wake utatukuka sana. Mungu aliwachukua kutoka Misri, naye huwapigania kwa nguvu kama nyati. Atayateketeza mataifa yaliyo adui zao, atavunjavunja mifupa yao, atawachoma kwa mishale yake. Ataotea na kulala chini kama simba, nani atathubutu kumwamsha? Abarikiwe yeyote atakayewabariki nyinyi Waisraeli, alaaniwe yeyote atakayewalaani. Balaki akawaka hasira dhidi ya Balaamu, akakunja mikono kwa ghadhabu na kumwambia, “Nilikuita uwalaani adui zangu, lakini mara hizi zote tatu umewabariki! Sasa! Nenda zako. Nilikuwa nimekuahidi kukupa zawadi nyingi, lakini Mwenyezi-Mungu hakukujalia kupata zawadi hizo, amekunyima!” Balaamu akamjibu Balaki, “Je, sikuwaambia wajumbe uliowatuma kwangu kwamba hata kama ungenipa nyumba yako imejaa fedha na dhahabu, mimi sitaweza kukiuka agizo la Mwenyezi-Mungu, kwa kufanya jambo lolote, jema au baya kwa hiari yangu mwenyewe? Nilisema, atakachosema Mwenyezi-Mungu ndicho nitakachokisema. “Sasa ninarudi kwa watu wangu, lakini kabla sijaondoka, acha nikuambie mambo ambayo watu hao watawatendea watu wako siku zijazo.” Basi, Balaamu akatamka kauli hii: “Kauli yangu mimi Balaamu mwana wa Beori, kauli ya mtu aliyefumbuliwa macho, kauli ya mtu aliyesikia maneno ya Mungu, na mtu ajuaye maarifa ya Mungu Mkuu, mtu aonaye maono ya Mungu Mwenye Nguvu, mtu anayesujudu, macho wazi. Ninamwona, atakayekuja, lakini baadaye, namwona, lakini hayuko karibu. Nyota itatokea kwa wazawa wa Yakobo, atatokea mfalme miongoni mwa Waisraeli. Kwa fimbo yake atawachapa viongozi wa Wamoabu atawaangamiza wazawa wote wa Sethi. Edomu itamilikiwa naye, Seiri itakuwa mali yake, Israeli itapata ushindi mkubwa. Mmoja wa wazawa wa Yakobo atatawala naye atawaangamiza watakaonusurika wa Ari.” Kisha Balaamu akawaangalia Waamaleki, akatoa kauli hii: “Amaleki ni taifa lenye nguvu kuliko yote, lakini mwishoni litaangamia kabisa.” Kisha Balaamu akawaangalia Wakeni, akatoa kauli hii: “Makao yenu ni salama, enyi Wakeni, kama kiota juu kabisa mwambani. Lakini mtateketezwa, enyi Wakeni. Mtachukuliwa mateka na Ashuru mpaka lini?” Tena Balaamu akatoa kauli hii: “Lo! Nani ataishi, Mungu atakapofanya hayo? Meli zitafika kutoka Kitimu, wataishambulia Ashuru na Eberi, lakini nao pia wataangamia milele.” Basi, Balaamu akaondoka, akarudi nyumbani; Balaki pia akaenda zake.
Hesabu 24:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza BWANA kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo awali, ili kupiga bao, bali alielekeza uso wake jangwani. Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kwa kabila; Roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbuliwa macho asema; Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho; Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda BWANA, Mfano wa mierezi kando ya maji. Maji yatatiririka kutoka ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa. Mungu amemleta kutoka Misri, Ana nguvu mfano wa nguvu za nyati; Atawameza mataifa walio adui zake, Ataivunja mifupa yao vipande vipande. Atawachoma kwa mishale yake. Aliinama, akalala mfano wa simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemstusha? Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye. Hasira ya Balaki ikawaka juu ya Balaamu akayapiga makofi; Balaki akamwambia Balaamu, Nilikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi. Basi sasa kimbilia mahali pako; niliazimu kukuheshimu sana; lakini, tazama, BWANA amekuzuilia heshima. Balaamu akamwambia Balaki, Je! Sikuwaambia wajumbe wako ulionitumia, nikisema, Hata Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kukiuka neno la BWANA, kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; BWANA atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi. Basi sasa, tazama, ninakwenda kwa watu wangu; haya, nitakuarifu mambo ambayo watu hawa watakayowatenda watu wako siku za mwisho. Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema, Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipigapiga pembe za Moabu, Na kuwavunjavunja wana wote wa ghasia. Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa. Mwenye kutawala atakuja kutoka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini. Kisha akamwangalia Amaleki, akatunga mithali yake, akasema, Amaleki alikuwa ni wa kwanza wa mataifa; Lakini mwisho wake atapata uharibifu. Kisha akamwangalia Mkeni, akatunga mithali yake, akasema, Makao yako yana nguvu, Na kiota chako kimewekwa katika jabali. Pamoja na haya Wakeni wataangamizwa, Hadi Ashuru atakapokuchukua mateka. Akatunga mithali yake akasema, Ole wao! Ni nani atakayepona, Mungu atakapofanya haya? Lakini merikebu zitakuja kutoka pwani kwa Kitimu, Nazo zitamtaabisha Ashuru, na Eberi zitamtaabisha, Yeye naye atapata uharibifu. Basi Balaamu akainuka, akaondoka na kurudi mahali pake; Balaki naye akaenda zake.
Hesabu 24:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza BWANA kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani. Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia. Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho; Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli! Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda BWANA, Mfano wa mierezi kando ya maji. Maji yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa. Mungu amemleta kutoka Misri, Ana nguvu mfano wa nguvu za nyati; Atawameza mataifa walio adui zake, Ataivunja mifupa yao vipande vipande. Atawachoma kwa mishale yake. Aliinama, akalala mfano wa simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemstusha? Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye. Hasira ya Balaki ikawaka juu ya Balaamu akayapiga makofi; Balaki akamwambia Balaamu, Nalikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi. Basi sasa kimbilia mahali pako; naliazimu kukuheshimu sana; lakini, tazama, BWANA amekuzuilia heshima. Balaamu akamwambia Balaki, Je! Sikuwaambia wajumbe wako ulionipelekea, nikisema, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la BWANA, kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; BWANA atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi. Basi sasa, tazama, ninakwenda kwa watu wangu; haya, nitakuarifu mambo ambayo watu hawa watakayowatenda watu wako siku za mwisho. Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema, Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia. Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa. Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini. Kisha akamwangalia Amaleki, akatunga mithali yake, akasema, Amaleki alikuwa ni wa kwanza wa mataifa; Lakini mwisho wake atafikilia uharibifu. Kisha akamwangalia Mkeni, akatunga mithali yake, akasema, Makao yako yana nguvu, Na kitundu chako kimewekwa katika jabali. Pamoja na haya Wakeni wataangamizwa, Hata Ashuru atakapokuchukua mateka. Akatunga mithali yake akasema, Ole wao! Ni nani atakayepona, Mungu atakapofanya haya? Lakini merikebu zitakuja kutoka pwani kwa Kitimu, Nazo zitamtaabisha Ashuru, na Eberi zitamtaabisha, Yeye naye atafikilia uharibifu. Basi Balaamu akainuka, akaondoka na kurudi mahali pake; Balaki naye akaenda zake.
Hesabu 24:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Balaamu alipoona imempendeza BWANA kubariki Israeli, hakuendelea tena kutafuta uchawi kama nyakati nyingine, bali aligeuza uso wake kuelekea nyikani. Balaamu alipotazama nje na kuona Israeli amepiga kambi kabila kwa kabila, Roho wa Mungu akawa juu yake, naye akatoa ujumbe wake: “Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori, ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri; ujumbe wake yeye anayesikia maneno ya Mungu, anayeona maono kutoka kwa Mwenyezi, ambaye husujudu, na macho yake yamefunguka: “Tazama jinsi yalivyo mazuri mahema yako, ee Yakobo, maskani zako, ee Israeli! “Kama mabonde, yanaenea, kama bustani kando ya mto, kama miti ya udi iliyopandwa na BWANA, kama mierezi kando ya maji. Maji yatatiririka kutoka ndoo zake; mbegu yake itakuwa na maji tele. “Mfalme wake atakuwa mkuu kuliko Mfalme Agagi; ufalme wake utatukuka. “Mungu alimleta kutoka Misri; yeye ana nguvu kama nyati. Anayararua mataifa yaliyo adui zake, na kuvunja mifupa yao vipande vipande; huwachoma kwa mishale yake. Hujikunyata na kuvizia kama simba, kama simba jike; nani anayethubutu kumwamsha? “Abarikiwe kila akubarikiye, na alaaniwe kila akulaaniye!” Ndipo hasira ya Balaki ikawaka dhidi ya Balaamu. Akapiga mikono yake pamoja, akamwambia Balaamu, “Nilikuita uje kuwalaani adui zangu, lakini umewabariki mara hizi tatu. Sasa ondoka upesi uende nyumbani! Mimi nilisema nitakuzawadia vizuri sana, lakini BWANA amekuzuia usizawadiwe.” Balaamu akamwambia Balaki, “Je, hukumbuki jinsi nilivyowaambia wajumbe uliowatuma kwangu? Niliwaambia hivi, ‘Hata ikiwa Balaki angenipa jumba lake la kifalme likiwa limejazwa fedha na dhahabu, nisingeweza kufanya kitu chochote kwa matakwa yangu, kikiwa kizuri au kibaya, kwenda kinyume na agizo la BWANA, nami imenipasa kusema tu kile BWANA atakachosema’? Sasa ninarudi kwa watu wangu. Lakini njoo, nikuonye kuhusu kile watu hawa watakachowatenda watu wako siku zijazo.” Kisha Balaamu akatoa ujumbe wake: “Ujumbe wa Balaamu mwana wa Beori, ujumbe wake yeye ambaye jicho lake linaona vizuri; ujumbe wake yeye ambaye husikia maneno ya Mungu, mwenye maarifa kutoka kwa Aliye Juu Sana, aonaye maono kutoka kwa Mwenyezi, na kuanguka kifudifudi nayo macho yake yamefunguliwa: “Namwona yeye, lakini si sasa; namtazama yeye, lakini si karibu. Nyota itatoka kwa Yakobo, fimbo ya ufalme itainuka kutoka kwa Israeli. Atawaponda Wamoabu paji za nyuso, na mafuvu yote ya wana wa Shethi. Edomu itamilikiwa, Seiri, adui yake, itamilikiwa, lakini Israeli atakuwa na nguvu. Mtawala atakuja kutoka kwa Yakobo na kuangamiza walionusurika katika mji.” Kisha Balaamu akawaona watu wa Amaleki, na kutoa ujumbe wake: “Amaleki alikuwa ya kwanza miongoni mwa mataifa, lakini mwisho wake ataangamizwa milele.” Kisha akawaona Wakeni, akatoa ujumbe wake: “Makao yenu ni salama, kiota chenu kiko kwenye mwamba. Hata hivyo ninyi Wakeni mtaangamizwa Ashuru atakapowachukua mateka.” Ndipo akatoa ujumbe wake: “Ole wao! Ni nani ataweza kuishi Mungu atakapofanya hili? Meli zitakuja kutoka pwani za Kitimu, zitaitiisha Ashuru na Eberi, lakini nao pia wataangamizwa.” Kisha Balaamu akainuka na kurudi nyumbani mwake, naye Balaki akashika njia yake.