Hesabu 21:1-9
Hesabu 21:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme mmoja Mkanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu alipopata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, alikwenda kuwashambulia, akawateka baadhi yao. Hapo, Waisraeli wakamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri wakisema: “Kama utawatia watu hawa mikononi mwetu, basi tutaiangamiza kabisa miji yao.” Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi lao, akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Waisraeli wakawaangamiza kabisa Wakanaani pamoja na miji yao. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Horma. Waisraeli walifunga safari kutoka Mlima Hori wakapitia njia inayoelekea bahari ya Shamu ili waizunguke nchi ya Edomu. Lakini njiani watu walikufa moyo. Basi, wakaanza kumnungunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini mmetutoa Misri tuje tukafie humu jangwani? Humu hamna chakula wala maji; nasi tumechoshwa na chakula hiki duni.” Hapo Mwenyezi-Mungu akapeleka nyoka wenye sumu miongoni mwa watu, wakawauma hata Waisraeli wengi wakafa. Basi, watu wakamwendea Mose, wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa kumnungunikia Mwenyezi-Mungu na wewe pia. Mwombe Mwenyezi-Mungu atuondolee nyoka hawa.” Kwa hiyo, Mose akawaombea watu. Ndipo Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.” Basi, Mose akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama nyoka huyo wa shaba, alipona.
Hesabu 21:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeishi Negebu, akasikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, akawateka baadhi yao. Basi Israeli akaweka nadhiri kwa BWANA akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa. BWANA akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma. Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Hesabu 21:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeketi upande wa Negebu, alisikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, na watu kadha wa kadha miongoni mwao akawateka mateka. Basi Israeli akaweka nadhiri kwa BWANA akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa. BWANA akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma. Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Hesabu 21:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mfalme wa Aradi, aliyekuwa Mkanaani aliyeishi huko Negebu, aliposikia kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, aliwashambulia Waisraeli na kuwateka baadhi yao. Ndipo Israeli akaweka nadhiri hii kwa BWANA: “Ikiwa utawatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza kabisa miji yao.” BWANA akasikiliza ombi la Waisraeli, naye akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Wakawaangamiza kabisa na miji yao; hivyo mahali pale pakaitwa Horma. Waisraeli wakasafiri kutoka Mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani, wakamnungʼunikia Mungu na Musa, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!” Ndipo BWANA akapeleka nyoka wenye sumu kati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa. Watu wakamjia Musa na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi ya BWANA na dhidi yako. Mwombe BWANA ili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Musa akawaombea hao watu. BWANA akamwambia Musa, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; yeyote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.” Kwa hiyo Musa akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu yeyote aliumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.