Hesabu 20:2-11
Hesabu 20:2-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mahali hapo walipopiga kambi hapakuwa na maji. Kwa hiyo watu jumuiya yote, wakakusanyika kinyume cha Mose na Aroni. Waliwalalamikia wote wakisema, “Afadhali tungekufa pamoja na ndugu zetu mbele ya hema la Mwenyezi-Mungu! Kwa nini mlituleta sisi jumuiya ya Mwenyezi-Mungu huku jangwani? Je, mlituleta ili tufe pamoja na mifugo yetu? Na, kwa nini mlitutoa Misri na kutuleta mahali hapa pabaya hivi? Hapa si mahali pa nafaka, tini, zabibu wala makomamanga. Hata maji ya kunywa hakuna!” Hapo, Mose na Aroni waliondoka kwenye umati wa watu, wakaenda kusimama kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasujudu. Basi, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Twaa ile fimbo yako, kisha wewe na Aroni ndugu yako, muikusanye jumuiya yote ya watu. Halafu, mbele ya macho yao, uuambie mwamba ulio mbele ya macho yao utoe maji yake. Naam, utaufanya mwamba utoe maji, ili jumuiya nzima ya watu na mifugo yao waweze kunywa.” Mose akaenda kuichukua ile fimbo mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamriwa. Kisha Mose na Aroni wakaikusanya jumuiya yote ya watu mbele ya mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni sasa, enyi waasi: Je, tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” Kisha Mose akainua mkono wake, akaupiga ule mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika kwa wingi, watu wakanywa pamoja na mifugo yao.
Hesabu 20:2-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakakusanyika Juu ya Musa na juu ya Haruni. Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingekuwa heri kama tungekufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za BWANA! Mbona mmewaleta kusanyiko la BWANA hadi jangwani hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu? Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa. Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hadi mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa BWANA ukawatokea. BWANA akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za BWANA kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.
Hesabu 20:2-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni. Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za BWANA! Mbona mmewaleta kusanyiko la BWANA hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu? Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa. Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa BWANA ukawatokea. BWANA akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za BWANA kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.
Hesabu 20:2-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mahali hapo hapakuwa na maji kwa ajili ya jumuiya hiyo, nao wakakusanyika ili kumpinga Musa na Haruni. Watu wakagombana na Musa, na kusema, “Laiti tungekufa ndugu zetu walipokufa mbele za BWANA! Kwa nini mmewaleta jumuiya ya BWANA kwenye jangwa hili, ili tufe humu, sisi na mifugo yetu? Kwa nini mmetupandisha kutoka Misri hadi mahali hapa pa kutisha? Hapa hakuna nafaka wala tini, zabibu au makomamanga. Wala hapa hakuna maji ya kunywa!” Musa na Haruni wakaondoka pale kwenye kusanyiko hadi kwenye mlango wa Hema la Kukutania na kuanguka kifudifudi, nao utukufu wa BWANA ukawatokea. BWANA akamwambia Musa, “Chukua ile fimbo, na wewe na ndugu yako Haruni mkawakusanye watu wote. Nena na ule mwamba mbele ya macho yao, nao utatoa maji yake. Utatoa maji kutoka huo mwamba kwa ajili ya jumuiya ili wao na mifugo yao waweze kunywa.” Kwa hiyo Musa akaichukua hiyo fimbo kutoka pale ilipokuwa mbele za BWANA kama alivyomwagiza. Musa na Haruni wakakusanya kusanyiko pamoja mbele ya huo mwamba, naye Musa akawaambia, “Sikilizeni, enyi waasi. Je, ni lazima tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?” Ndipo Musa akainua mkono wake na kuupiga mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika, nayo jumuiya na mifugo yao wakanywa.