Hesabu 2:1-9
Hesabu 2:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu aliwapa Mose na Aroni, maagizo yafuatayo: “Waisraeli watapiga kambi zao, kila mmoja akikaa mahali penye bendera yake, penye alama za ukoo wake. Watapiga kambi zao kulizunguka hema la mkutano. “Wale watakaopiga kambi upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua watakuwa kikundi cha watu walio chini ya bendera ya Yuda na kiongozi wao atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 74600. Wale watakaofuata kupiga kambi baada ya watu wa Yuda watakuwa kabila la Isakari, kiongozi wao akiwa Nethaneli mwana wa Suari, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 54,400. Kisha kabila la Zebuluni, kiongozi wao akiwa Eliabu mwana wa Heloni, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 57,400. Jumla yote ya watu watakaokuwa katika kambi ya Yuda kulingana na makundi yao ni watu 186,400. Hao ndio watakaotangulia kusafiri.
Hesabu 2:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye bendera yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote. Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa bendera ya kambi ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu sabini na nne na mia sita. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na nne na mia nne; na kabila la Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na saba na mia nne. Hao wote waliohesabiwa katika kambi ya Yuda walikuwa elfu mia moja themanini na sita na mia nne, kwa makundi yao. Hao ndio watakaotangulia mbele.
Hesabu 2:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye beramu yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote. Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa beramu ya marago ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sabini na nne elfu na mia sita. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na nne elfu na mia nne; na kabila ya Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na saba elfu na mia nne. Hao wote waliohesabiwa katika marago ya Yuda walikuwa mia na themanini na sita elfu na mia nne, kwa majeshi yao. Hao ndio watakaosafiri mbele.
Hesabu 2:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA aliwaambia Musa na Haruni: “Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali kiasi, kila mwanaume akiwa chini ya beramu yake, pamoja na bendera ya jamaa yake.” Kwa upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua, kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu. Kundi lake lina watu elfu sabini na nne na mia sita. Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari. Kundi lake lina watu elfu hamsini na nne na mia nne. Kabila la Zabuloni litafuata. Kiongozi wa watu wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. Kundi lake lina watu elfu hamsini na saba na mia nne. Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja themanini na sita na mia nne. Wao watatangulia kuondoka.