Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 2:1-34

Hesabu 2:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu aliwapa Mose na Aroni, maagizo yafuatayo: “Waisraeli watapiga kambi zao, kila mmoja akikaa mahali penye bendera yake, penye alama za ukoo wake. Watapiga kambi zao kulizunguka hema la mkutano. “Wale watakaopiga kambi upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua watakuwa kikundi cha watu walio chini ya bendera ya Yuda na kiongozi wao atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 74600. Wale watakaofuata kupiga kambi baada ya watu wa Yuda watakuwa kabila la Isakari, kiongozi wao akiwa Nethaneli mwana wa Suari, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 54,400. Kisha kabila la Zebuluni, kiongozi wao akiwa Eliabu mwana wa Heloni, kikosi chake kulingana na hesabu ni wanaume 57,400. Jumla yote ya watu watakaokuwa katika kambi ya Yuda kulingana na makundi yao ni watu 186,400. Hao ndio watakaotangulia kusafiri. “Kwa upande wa kusini, wale walio chini ya bendera ya kundi la Reubeni kulingana na makundi yao, kiongozi wao akiwa Elisuri mwana wa Shedeuri, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 46,500. Kisha wale watakaopiga kambi kando ya watu wa Reubeni watakuwa ni watu wa kabila la Simeoni, kiongozi wao akiwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 59,300. Hatimaye kabila la Gadi, kiongozi wao akiwa Eliasafu mwana wa Reueli, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 45,650. Jumla ya wanaume watakaokuwa katika kambi ya Reubeni kulingana na makundi yao ni watu 151,450. Hawa ndio watakaokuwa katika msafara wa pili. “Halafu, kambi ya kabila la Walawi, ikiwa katikati ya kambi zote, na wakiwa wamebeba hilo hema la mkutano, wataondoka; kila kundi litasafiri kwa kufuata nafasi yake chini ya bendera yao. “Kwa upande wa magharibi, wale walio chini ya bendera ya kundi la Efraimu watapiga kambi kulingana na makundi yao, kiongozi wao akiwa Elishama mwana wa Amihudi, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 32,200. Mara tu baada ya Waefraimu litafuata kabila la Manase: Kiongozi wake akiwa Gamalieli, mwana wa Pedasuri, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa watu 32,000. Hatimaye kabila la Benyamini: Kiongozi wake ni Abidani, mwana wa Gideoni, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 35,400. Jumla ya watu watakaokuwa katika kambi ya Efraimu kulingana na makundi yao ni watu 108,100. Kundi hili la Efraimu litakuwa katika msafara wa tatu. “Kwa upande wa kaskazini, watapiga kambi katika makundi yao wale walio chini ya bendera ya Dani, kiongozi wao atakuwa Ahiezeri, mwana wa Amishadai, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 62,700. Kisha wale watakaopiga kambi baada yao watakuwa watu wa kabila la Asheri, kiongozi wao akiwa Pagieli mwana wa Okrani, kikosi chake kulingana na hesabu kitakuwa na watu 41,500. “Hatimaye watu wa kabila la Naftali, kiongozi wake akiwa Ahira mwana wa Enani, kikosi chake kulingana na hesabu, kitakuwa na watu 53,400. Jumla ya watu watakaokuwa katika kambi ya Dani kulingana na makundi yao ni watu 157,600. Kundi hili la Dani litakuwa katika msafara wa mwisho, bendera baada ya bendera.” Hao ndio Waisraeli waliohesabiwa kulingana na koo zao, katika kambi na vikosi vyao; wote walikuwa 603,550. Lakini Walawi hawakuhesabiwa miongoni mwa watu wa Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Hivyo ndivyo, Waisraeli walivyofanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Walipiga kambi zao, kufuata bendera zao na walisafiri kila mmoja akiandamana na jamaa yake kwa kufuata ukoo wake.

Shirikisha
Soma Hesabu 2

Hesabu 2:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye bendera yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote. Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa bendera ya kambi ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu sabini na nne na mia sita. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na nne na mia nne; na kabila la Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na saba na mia nne. Hao wote waliohesabiwa katika kambi ya Yuda walikuwa elfu mia moja themanini na sita na mia nne, kwa makundi yao. Hao ndio watakaotangulia mbele. Upande wa kusini kutakuwa na bendera ya kambi ya Reubeni kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Reubeni atakuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu arubaini na sita na mia tano. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Simeoni; na mkuu wa wana wa Simeoni atakuwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na tisa na mia tatu; na kabila la Gadi; na mkuu wa wana wa Gadi atakuwa Eliasafu mwana wa Deueli; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu arubaini na tano, mia sita na hamsini. Wote waliohesabiwa katika kambi za Reubeni walikuwa elfu mia moja hamsini na moja na mia nne na hamsini, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaofuata wakiwa kundi la pili. Ndipo hema ya kukutania itasafiri, pamoja na kambi za Walawi katikati ya kambi zote; kama wapangavyo kambi, watasafiri vivyo hivyo, kila mtu mahali pake, penye bendera zao. Upande wa magharibi kutakuwa na bendera ya kambi ya Efraimu kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Efraimu atakuwa Elishama mwana wa Amihudi. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao walikuwa elfu arubaini na mia tano. Na karibu naye itakuwa kabila la Manase; na mkuu wa wana wa Manase atakuwa Gamalieli mwana wa Pedasuri; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu thelathini na mbili na mia mbili; tena kabila la Benyamini; na mkuu wa wana wa Benyamini atakuwa Abidani mwana wa Gideoni; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu thelathini na tano na mia nne. Wote waliohesabiwa katika kambi ya Efraimu walikuwa elfu mia moja na nane na mia moja, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaoondoka wakiwa kundi la tatu. Upande wa kaskazini kutakuwa na bendera ya kambi ya Dani kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Dani atakuwa Ahiezeri mwana wa Amishadai. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu sitini na mbili na mia saba. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila la Asheri; na mkuu wa wana wa Asheri atakuwa Pagieli mwana wa Okrani; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu arubaini na moja na mia tano; kisha kabila la Naftali; na mkuu wa wana wa Naftali atakuwa Ahira mwana wa Enani; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu hamsini na tatu na mia nne. Wote waliohesabiwa katika kambi ya Dani walikuwa elfu mia moja hamsini na saba na mia sita. Hao ndio watakaoondoka mwisho kwa kufuata bendera yao. Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli kwa nyumba za baba zao; wote waliohesabiwa katika kambi kwa majeshi yao, walikuwa elfu mia sita na tatu na mia tano na hamsini. Lakini Walawi hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli; kama BWANA alivyomwagiza Musa. Hivyo ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama BWANA alivyomwamuru Musa; ndivyo walivyojipanga kufuata bendera zao, na ndivyo walivyosafiri, kila mtu kwa jamaa zao, kwa nyumba za baba zao.

Shirikisha
Soma Hesabu 2

Hesabu 2:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye beramu yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote. Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa beramu ya marago ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sabini na nne elfu na mia sita. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na nne elfu na mia nne; na kabila ya Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na saba elfu na mia nne. Hao wote waliohesabiwa katika marago ya Yuda walikuwa mia na themanini na sita elfu na mia nne, kwa majeshi yao. Hao ndio watakaosafiri mbele. Upande wa kusini kutakuwa na beramu ya marago ya Reubeni kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Reubeni atakuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na sita elfu na mia tano. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Simeoni; na mkuu wa wana wa Simeoni atakuwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na kenda elfu na mia tatu; na kabila ya Gadi; na mkuu wa wana wa Gadi atakuwa Eliasafu mwana wa Deueli; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na tano elfu na mia sita na hamsini. Wote waliohesabiwa katika marago ya Reubeni walikuwa mia na hamsini na moja elfu na mia nne na hamsini, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaosafiri mahali pa pili. Ndipo hema ya kukutania itasafiri, pamoja na marago ya Walawi katikati ya marago yote; kama wapangavyo marago, watasafiri vivyo, kila mtu mahali pake, penye beramu zao. Upande wa magharibi kutakuwa na beramu ya marago ya Efraimu kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Efraimu atakuwa Elishama mwana wa Amihudi. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini elfu na mia tano. Na karibu naye itakuwa kabila ya Manase; na mkuu wa wana wa Manase atakuwa Gamalieli mwana wa Pedasuri; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa thelathini na mbili elfu na mia mbili; tena kabila ya Benyamini; na mkuu wa wana wa Benyamini atakuwa Abidani mwana wa Gideoni; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa thelathini na tano elfu na mia nne. Wote waliohesabiwa katika marago ya Efraimu walikuwa mia na nane elfu na mia moja, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaosafiri katika mahali pa tatu. Upande wa kaskazini kutakuwa na beramu ya marago ya Dani kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Dani atakuwa Ahiezeri mwana wa Amishadai. Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sitini na mbili elfu na mia saba. Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Asheri; na mkuu wa wana wa Asheri atakuwa Pagieli mwana wa Okrani; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na moja elfu na mia tano; kisha kabila ya Naftali; na mkuu wa wana wa Naftali atakuwa Ahira mwana wa Enani; na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na tatu elfu na mia nne. Wote waliohesabiwa katika marago ya Dani walikuwa mia na hamsini na saba elfu na mia sita. Hao ndio watakaosafiri mwisho kwa kuandama beramu zao. Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli kwa nyumba za baba zao; wote waliohesabiwa katika marago kwa majeshi yao, walikuwa mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini. Lakini Walawi hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli; kama BWANA alivyomwagiza Musa. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote BWANA aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyopanga penye beramu zao, na ndivyo walivyosafiri, kila mtu kwa jamaa zao, kwa nyumba za baba zao.

Shirikisha
Soma Hesabu 2

Hesabu 2:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA aliwaambia Musa na Haruni: “Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali kiasi, kila mwanaume akiwa chini ya beramu yake, pamoja na bendera ya jamaa yake.” Kwa upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua, kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu. Kundi lake lina watu elfu sabini na nne na mia sita. Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari. Kundi lake lina watu elfu hamsini na nne na mia nne. Kabila la Zabuloni litafuata. Kiongozi wa watu wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. Kundi lake lina watu elfu hamsini na saba na mia nne. Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja themanini na sita na mia nne. Wao watatangulia kuondoka. Kwa upande wa kusini kutakuwa na kambi ya makundi ya Reubeni chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Reubeni ni Elisuri mwana wa Shedeuri. Kundi lake lina watu elfu arobaini na sita na mia tano. Kabila la Simeoni watapiga kambi karibu na Reubeni. Kiongozi wa watu wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Surishadai. Kundi lake lina watu elfu hamsini na tisa na mia tatu. Kabila la Gadi litafuata. Kiongozi wa watu wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. Kundi lake lina watu elfu arobaini na tano mia sita na hamsini. Wanaume wote walio katika kambi ya Reubeni, kufuatana na makundi yao, ni elfu mia moja hamsini na moja na mia nne na hamsini (151,450). Nao watakuwa nafasi ya pili kuondoka. Kisha Hema la Kukutania na kambi ya Walawi vitakuwa katikati ya kambi zote. Wao watasafiri kwa utaratibu ule ule kama walivyopiga kambi, kila mmoja mahali pake mwenyewe chini ya beramu yake. Upande wa magharibi kutakuwa na kambi ya makundi ya Efraimu chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Efraimu ni Elishama mwana wa Amihudi. Kundi lake lina watu elfu arobaini na mia tano. Kabila la Manase litafuata baada ya Efraimu. Kiongozi wa watu wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. Kundi lake lina watu elfu thelathini na mbili na mia mbili. Kabila la Benyamini litafuata baada ya Manase. Kiongozi wa watu wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. Kundi lake lina watu elfu thelathini na tano na mia nne. Wanaume wote walio katika kambi ya Efraimu kufuatana na makundi yao ni elfu mia moja na nane na mia moja. Nao watakuwa nafasi ya tatu kuondoka. Upande wa kaskazini kutakuwa na makundi ya kambi ya Dani, chini ya beramu yao. Kiongozi wa watu wa Dani ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. Kundi lake lina watu elfu sitini na mbili na mia saba. Kabila la Asheri watapiga kambi karibu na Dani. Kiongozi wa watu wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani. Kundi lake lina watu elfu arobaini na moja na mia tano. Kabila la Naftali litafuata. Kiongozi wa watu wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. Kundi lake lina watu elfu hamsini na tatu na mia nne. Wanaume wote walio katika kambi ya Dani ni elfu mia moja hamsini na saba na mia sita. Wao watakuwa wa mwisho kuondoka chini ya beramu yao. Hawa ndio Waisraeli, wakiwa wamehesabiwa kufuatana na jamaa zao. Wote walio kambini kwa makundi yao ni watu elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550). Hata hivyo, Walawi hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine, kama BWANA alivyomwagiza Musa. Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kila kitu BWANA alichomwamuru Musa. Hivyo ndivyo walivyopiga kambi chini ya beramu zao. Pia hivyo ndivyo walivyoondoka, kila mmoja akiwa na ukoo wake na jamaa yake.

Shirikisha
Soma Hesabu 2