Hesabu 19:11-16
Hesabu 19:11-16 Biblia Habari Njema (BHN)
“Mtu akigusa maiti ya mtu yeyote, atakuwa najisi kwa siku saba. Siku ya tatu na ya saba mtu huyo atajiosha kwa yale maji ya utakaso, naye atakuwa safi. Lakini akiacha kujitakasa katika siku ya tatu na ya saba, mtu huyo atabaki kuwa najisi. Agusaye maiti, yaani mwili wa mtu aliyekufa, asipojitakasa, analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu, naye atatengwa na wana wa Israeli. Mtu huyo atabaki najisi kwa sababu hakunyunyiziwa yale maji ya utakaso. “Na hii ndiyo sheria ya kufuatwa kama mtu akifia hemani: Kila mtu atakayeingia ndani ya hema hilo, au aliye ndani ya hema hilo, atakuwa najisi kwa siku saba. Kila chombo kilicho wazi ambacho hakina kifuniko juu yake kitakuwa najisi. Mtu yeyote akigusa mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida nje ya nyumba, au akigusa mfupa wa mtu au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.
Hesabu 19:11-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu agusaye maiti yeyote atakuwa najisi muda wa siku saba; naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi. Mtu yeyote yule agusaye maiti ya mtu aliyekufa, asijitakase, analitia unajisi maskani ya BWANA; na mtu huyo atatupiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ungali upo juu yake. Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba. Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi. Kisha mtu yeyote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba.
Hesabu 19:11-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu agusaye maiti ye yote atakuwa najisi muda wa siku saba; naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi. Mtu awaye yote agusaye maiti wa mtu aliyekufa, asijitakase, yuatia unajisi maskani ya BWANA; na mtu huyo atakatiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ukali juu yake bado. Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba. Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi. Kisha mtu ye yote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba.
Hesabu 19:11-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote atakuwa najisi kwa siku saba. Ni lazima ajitakase mwenyewe kwa maji katika siku ya tatu na siku ya saba, ndipo atakuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu na ya saba, hatakuwa safi. Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote na kushindwa kujitakasa mwenyewe hunajisi Maskani ya BWANA. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na Israeli. Kwa sababu hajanyunyiziwa maji ya utakaso, yeye ni najisi; unajisi wake unabaki juu yake. “Hii ndiyo sheria itumikayo wakati mtu amekufa ndani ya hema: Yeyote aingiaye ndani ya hema hilo na yeyote aliye ndani yake watakuwa najisi kwa muda wa siku saba, nacho kila chombo kisicho na kifuniko juu yake kitakuwa najisi. “Mtu yeyote aliye nje mahali pa wazi agusaye mtu aliyeuawa kwa upanga au mtu aliyekufa kwa kifo cha kawaida, au mtu yeyote agusaye mfupa wa mtu aliyekufa au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba.