Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 19:1-22 - Compare All Versions

Hesabu 19:1-22 BHN (Biblia Habari Njema)

Mwenyezi-Mungu aliendelea kuwaambia Mose na Aroni, “Haya ni masharti ya sheria ambayo mimi Mwenyezi-Mungu ninatoa. Waambieni Waisraeli wawaletee ng'ombe jike mwekundu asiye na dosari wala kasoro yoyote, na ambaye hajapata kufungwa nira. Nyinyi mtampa kuhani Eleazari ng'ombe huyo. Atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele ya kuhani huyo. “Kisha kuhani Eleazari atachukua kiasi cha damu na kuinyunyiza kwa kidole mara saba, kuelekea upande wa mbele wa hema la mkutano. Ngombe huyo mzima atateketezwa kwa moto mbele ya kuhani. Kila kitu chake kitateketezwa; ngozi, nyama, damu na utumbo wake. Halafu kuhani atachukua mti wa mwerezi, husopo na sufu nyekundu na kuvitia katika moto huo. Baada ya hayo, kuhani atazifua nguo zake na kuoga mwili kwa maji, halafu anaweza kuingia kambini; atakuwa najisi hadi jioni. Mtu atakayemteketeza ng'ombe huyo pia atazifua nguo zake kwa maji na kuoga mwili kwa maji, lakini naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Mtu aliye safi atayazoa majivu ya ng'ombe huyo na kuyapeleka mahali safi nje ya kambi. Yatahifadhiwa na kutumiwa na jumuiya nzima ya Israeli kutengeneza maji ya kuondoa najisi, ili kuondoa dhambi. Mtu atakayeyazoa majivu ya ng'ombe huyo lazima azifue nguo zake, lakini atakuwa najisi hadi jioni. Sharti hili ni la kudumu, na litawahusu Waisraeli na watu wengine watakaoishi pamoja nao. “Mtu akigusa maiti ya mtu yeyote, atakuwa najisi kwa siku saba. Siku ya tatu na ya saba mtu huyo atajiosha kwa yale maji ya utakaso, naye atakuwa safi. Lakini akiacha kujitakasa katika siku ya tatu na ya saba, mtu huyo atabaki kuwa najisi. Agusaye maiti, yaani mwili wa mtu aliyekufa, asipojitakasa, analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu, naye atatengwa na wana wa Israeli. Mtu huyo atabaki najisi kwa sababu hakunyunyiziwa yale maji ya utakaso. “Na hii ndiyo sheria ya kufuatwa kama mtu akifia hemani: Kila mtu atakayeingia ndani ya hema hilo, au aliye ndani ya hema hilo, atakuwa najisi kwa siku saba. Kila chombo kilicho wazi ambacho hakina kifuniko juu yake kitakuwa najisi. Mtu yeyote akigusa mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida nje ya nyumba, au akigusa mfupa wa mtu au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba. “Kwa ajili ya wale waliojitia najisi watachukua majivu ya sadaka ya kuondoa dhambi iliyoteketezwa, majivu hayo yatachanganywa na maji ya mtoni katika chungu. Mtu aliye safi atachukua husopo, halafu ataichovya katika maji hayo, kisha atainyunyizia hema, vyombo vyote vilivyomo ndani ya hema na watu waliokuwamo ndani. Atamnyunyizia pia mtu aliyegusa mfupa wa mtu, au mwili wa mtu aliyeuawa au aliyekufa kifo cha kawaida, au aliyegusa kaburi. Katika siku ya tatu na ya saba, mtu aliye safi atamnyunyizia mtu aliye najisi maji hayo; hivyo katika siku ya saba, atamtakasa mtu huyo aliye najisi, naye atazifua nguo zake na kuoga, na jioni atakuwa safi. “Lakini mtu akiwa najisi asipojitakasa, mtu huyo atakataliwa mbali na jumuiya, kwa kuwa analitia najisi hema la Mwenyezi-Mungu. Kwa vile hakunyunyiziwa maji ya utakaso, yu unajisi. Watu watalishika sharti hili daima. Mtu atakayenyunyiza maji ya kutakasia ataosha nguo zake; naye anayegusa maji hayo ya najisi atakuwa najisi hadi jioni. Chochote atakachogusa mtu najisi kitakuwa najisi, na yeyote atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi mpaka jioni.”

Shirikisha
Hesabu 19 BHN

Hesabu 19:1-22 SRUV (Swahili Revised Union Version)

BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Hii ndiyo amri ya sheria BWANA aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng'ombe jike mwekundu asiye na doa, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado; nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake; kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba; kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng'ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto; kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng'ombe. Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hadi jioni. Na huyo aliyemchoma moto ng'ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hadi jioni. Kisha mtu mmoja aliye safi atayazoa majivu ya huyo ng'ombe, na kuyaweka yawe akiba katika mahali safi nje ya kambi, nayo yatatunzwa kwa ajili ya mkutano wa wana wa Israeli, kuwa ndiyo maji ya farakano; ni sadaka ya dhambi. Na yeye ayazoaye majivu ya huyo ng'ombe atazifua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; na jambo hili litakuwa amri ya milele, kwa wana wa Israeli, na wa mgeni akaaye kati yao. Mtu agusaye maiti yeyote atakuwa najisi muda wa siku saba; naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi. Mtu yeyote yule agusaye maiti ya mtu aliyekufa, asijitakase, analitia unajisi maskani ya BWANA; na mtu huyo atatupiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ungali upo juu yake. Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba. Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi. Kisha mtu yeyote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba. Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo; kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi; na yule aliye safi atamnyunyizia huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni. Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa BWANA; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yuko najisi. Nayo itakuwa amri ya siku zote kwao; na yeye anyunyizaye maji ya farakano atazifua nguo zake; naye ayagusaye hayo maji ya farakano atakuwa najisi hadi jioni. Na kitu chochote atakachokigusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi; na mtu atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi hadi jioni.

Shirikisha
Hesabu 19 SRUV

Hesabu 19:1-22 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Hii ndiyo amri ya sheria BWANA aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng’ombe mke mwekundu asiye na kipaku, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado; nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake; kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba; kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng’ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto; kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng’ombe. Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hata jioni. Na huyo aliyemchoma moto ng’ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni. Kisha mtu mmoja aliye safi atayazoa majivu ya huyo ng’ombe, na kuyaweka yawe akiba katika mahali safi nje ya kambi, nayo yatatunzwa kwa ajili ya mkutano wa wana wa israeli, kuwa ndiyo maji ya farakano; ni sadaka ya dhambi. Na yeye ayazoaye majivu ya huyo ng’ombe atazifua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; na jambo hili litakuwa amri ya milele, kwa wana wa Israeli, na wa mgeni akaaye kati yao. Mtu agusaye maiti ye yote atakuwa najisi muda wa siku saba; naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi. Mtu awaye yote agusaye maiti wa mtu aliyekufa, asijitakase, yuatia unajisi maskani ya BWANA; na mtu huyo atakatiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ukali juu yake bado. Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba. Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi. Kisha mtu ye yote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba. Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo; kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi; na yule aliye safi atamnyunyiza huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni. Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa BWANA; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yu najisi. Nayo itakuwa amri ya sikuzote kwao; na yeye anyunyizaye maji ya farakano atazifua nguo zake; naye ayagusaye hayo maji ya farakano atakuwa najisi hata jioni. Na kitu cho chote atakachokigusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi; na mtu atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi hata jioni.

Shirikisha
Hesabu 19 SUV

Hesabu 19:1-22 NEN (Neno)

BWANA akamwambia Musa na Haruni: “Hivi ndivyo sheria ambayo BWANA ameagiza itakavyo: Waambie Waisraeli wakuletee mtamba mwekundu asiye na dosari wala waa, na ambaye hajapata kufungwa nira. Mpeni kuhani Eleazari huyo mtamba; naye atatolewa nje ya kambi na kuchinjwa mbele yake huyo kuhani. Kisha kuhani Eleazari atachukua sehemu ya damu yake kwenye kidole chake, na kuinyunyiza mara saba kuelekea upande wa mbele ya Hema la Kukutania. Wakati angali akitazama, mtamba huyo atateketezwa: ngozi yake, nyama yake, damu na sehemu zake za ndani. Kuhani atachukua kuni za mti wa mwerezi, hisopo na sufu nyekundu, na kuvitupa kwenye huyo mtamba anayeungua. Baada ya hayo, kuhani lazima afue nguo zake, na aoge mwili wake kwa maji. Kisha anaweza kurudi kambini, lakini atakuwa najisi hadi jioni. Mtu amchomaye huyo mtamba lazima naye pia afue nguo zake na kuoga kwa maji, naye pia atakuwa najisi hadi jioni. “Mtu ambaye ametakaswa atakusanya majivu ya mtamba huyo na kuyaweka mahali nje ya kambi palipo safi. Yatahifadhiwa na jumuiya ya Waisraeli kwa matumizi katika maji ya utakaso; ni kwa ajili ya kutakasa kutoka dhambini. Mtu akusanyaye majivu ya huyo mtamba ni lazima pia afue nguo zake, kadhalika naye pia atakuwa najisi hadi jioni. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa Waisraeli na kwa wageni wanaoishi miongoni mwao. “Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote atakuwa najisi kwa siku saba. Ni lazima ajitakase mwenyewe kwa maji katika siku ya tatu na siku ya saba, ndipo atakuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu na ya saba, hatakuwa safi. Mtu yeyote agusaye maiti ya mtu yeyote na kushindwa kujitakasa mwenyewe hunajisi Maskani ya BWANA. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na Israeli. Kwa sababu hajanyunyiziwa maji ya utakaso, yeye ni najisi; unajisi wake unabaki juu yake. “Hii ndiyo sheria itumikayo wakati mtu amekufa ndani ya hema: Yeyote aingiaye ndani ya hema hilo na yeyote aliye ndani yake watakuwa najisi kwa muda wa siku saba, nacho kila chombo kisicho na kifuniko juu yake kitakuwa najisi. “Mtu yeyote aliye nje mahali pa wazi agusaye mtu aliyeuawa kwa upanga au mtu aliyekufa kwa kifo cha kawaida, au mtu yeyote agusaye mfupa wa mtu aliyekufa au kaburi, atakuwa najisi kwa siku saba. “Kwa mtu aliye najisi, weka majivu ya sadaka ya utakaso wa dhambi ndani ya chombo, umimine maji safi juu yao. Kisha mtu aliyetakasika atachukua hisopo, achovye ndani ya maji, na kunyunyizia hema na vifaa vyote pamoja na watu ambao walikuwamo. Pia ni lazima amnyunyizie mtu yeyote ambaye amegusa mfupa wa mtu aliyekufa, au kaburi, au mtu aliyeuawa, au mtu ambaye amekufa kifo cha kawaida. Mtu ambaye ni safi ndiye atakayemnyunyizia yeyote ambaye ni najisi siku ya tatu na siku ya saba, na katika siku ya saba atamtakasa mtu huyo. Mtu ambaye ametakaswa lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji, na jioni ile atakuwa safi. Lakini ikiwa mtu ambaye ni najisi hakujitakasa mwenyewe, ni lazima akatiliwe mbali na jumuiya, kwa sababu ameinajisi Maskani ya BWANA. Maji ya utakaso hayajanyunyizwa juu yake, naye ni najisi. Hili ni agizo la kudumu kwao. “Mtu anayenyunyiza yale maji ya utakaso lazima pia afue nguo zake, na yeyote anayegusa maji ya utakaso atakuwa najisi hadi jioni. Kitu chochote anachogusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi, na yeyote akigusaye huwa najisi hadi jioni.”

Shirikisha
Hesabu 19 NEN