Hesabu 18:1-7
Hesabu 18:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Lawama zote kuhusu huduma ya hema takatifu, zitakuwa juu yako, wanao na ukoo wako; kadhalika makosa yanayoambatana na ukuhani wako wewe mwenyewe na wanao mtahusika. Wewe, wanao na wazawa wako wote mtahudumu kama makuhani; jamaa zako wengine wa kabila lako watafanya kazi pamoja nawe mbele ya hema la maamuzi. Wao watafanya kazi utakazowapa na kutimiza wajibu wao kuhusu hema. Lakini hawana ruhusa kuvigusa vyombo vya hema, wala kuikaribia madhabahu, wasije wakafa, nawe pia ukafa. Wao watajiunga nawe kazini na kutimiza wajibu wao kikamilifu kuhusu huduma zote za hema, na wala pasiwe na mtu mwingine atakayekukaribia humo. Nyinyi mtafanya huduma za mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu yangu isije ikawatokea tena Waisraeli. Ni mimi niliyewachagua ndugu zenu Walawi miongoni mwa Waisraeli kama toleo kwenu. Wao wametengwa kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, ili watoe huduma katika hema la mkutano. Lakini wewe peke yako na wanao mtatoa huduma zote za kikuhani kwa ajili ya madhabahu na vyote vilivyomo katika mahali patakatifu. Huo ni wajibu wenu, kwa sababu ninawapeni kipawa cha ukuhani. Mtu yeyote asiyestahili atakayevikaribia vyombo vya hema, atauawa.”
Hesabu 18:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu. Na ndugu zako nao, kabila la Lawi, kabila la baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungane nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi. Nao watahudumu kwa kufuata amri yako, na kuhudumu hemani pote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi. Nao watataambatana nawe, na kuhudumu katika hema ya kukutania, kwa ajili ya huduma yote ya hema; na mgeni asiwakaribie ninyi. Nanyi mtahudumu katika patakatifu na huduma ya madhabahuni, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena. Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa BWANA, wahudumu katika hema ya kukutania. Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa.
Hesabu 18:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu. Na ndugu zako nao, kabila ya Lawi, kabila ya baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungwe nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi. Nao watashika ulinzi kwa amri yako, na ulinzi wa Hema yote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi. Nao wataungwa nawe, na kuushika ulinzi wa hema ya kukutania, kwa ajili ya utumishi wote wa hema; na mgeni asiwakaribie ninyi. Nanyi mtashika ulinzi wa patakatifu, na ulinzi wa madhabahu, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena. Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa BWANA, waufanye utumishi wa hema ya kukutania. Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa.
Hesabu 18:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Haruni, “Wewe, wanao na jamaa ya baba yako mtawajibika kwa makosa dhidi ya mahali patakatifu, na wewe na wanao peke yenu ndio mtakaowajibika kwa makosa dhidi ya ukuhani. Walete Walawi wenzako kutoka kabila la baba zako ili waungane nanyi na kuwasaidia wakati wewe na wanao mnapohudumu mbele ya Hema la Ushuhuda. Watawajibika kwenu na watafanya kazi zote za Hema, lakini kamwe wasisogelee vifaa vya patakatifu au madhabahu, la sivyo wao na ninyi mtakufa. Watajiunga nanyi na watawajibika kwa utunzaji wa Hema la Kukutania, yaani kazi zote kwenye Hema, wala hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kusogea karibu hapo mlipo. “Mtawajibika katika utunzaji wa mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu isiwaangukie Waisraeli tena. Mimi mwenyewe nimewachagua Walawi wenzenu kutoka miongoni mwa Waisraeli kama zawadi kwenu, waliowekwa wakfu kwa BWANA ili kufanya kazi katika Hema la Kukutania. Lakini ni wewe tu na wanao mtakaoweza kutumika kama makuhani kuhusiana na kila kitu kwenye madhabahu na ndani ya pazia. Ninawapa utumishi wa ukuhani kama zawadi. Mtu mwingine yeyote atakayekaribia mahali patakatifu ni lazima auawe.”