Hesabu 18:1-32
Hesabu 18:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Lawama zote kuhusu huduma ya hema takatifu, zitakuwa juu yako, wanao na ukoo wako; kadhalika makosa yanayoambatana na ukuhani wako wewe mwenyewe na wanao mtahusika. Wewe, wanao na wazawa wako wote mtahudumu kama makuhani; jamaa zako wengine wa kabila lako watafanya kazi pamoja nawe mbele ya hema la maamuzi. Wao watafanya kazi utakazowapa na kutimiza wajibu wao kuhusu hema. Lakini hawana ruhusa kuvigusa vyombo vya hema, wala kuikaribia madhabahu, wasije wakafa, nawe pia ukafa. Wao watajiunga nawe kazini na kutimiza wajibu wao kikamilifu kuhusu huduma zote za hema, na wala pasiwe na mtu mwingine atakayekukaribia humo. Nyinyi mtafanya huduma za mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu yangu isije ikawatokea tena Waisraeli. Ni mimi niliyewachagua ndugu zenu Walawi miongoni mwa Waisraeli kama toleo kwenu. Wao wametengwa kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, ili watoe huduma katika hema la mkutano. Lakini wewe peke yako na wanao mtatoa huduma zote za kikuhani kwa ajili ya madhabahu na vyote vilivyomo katika mahali patakatifu. Huo ni wajibu wenu, kwa sababu ninawapeni kipawa cha ukuhani. Mtu yeyote asiyestahili atakayevikaribia vyombo vya hema, atauawa.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Ninakukabidhi matoleo waliyonipa Waisraeli, vitu vyote vitakatifu walivyonipa: Vitu vyote vilivyowekwa wakfu na Waisraeli. Ninakupa vitu vyote wewe na wazawa wako kuwa fungu lenu, na hiyo ni haki yenu milele. Kati ya vitu vitakatifu kabisa ambavyo haviteketezwi motoni, hivi vitakuwa vyenu: Sadaka za nafaka, sadaka za kuondoa dhambi na sadaka za hatia. Kila kitu watu watakachonitolea kama tambiko takatifu kitakuwa chako na wanao. Mtavila vitu hivyo kama vitu vitakatifu kabisa, na ni wanaume tu ndio watakaovila; vitu hivyo ni vitakatifu kwenu. “Pia, vitu vingine vyote watakavyonitolea Waisraeli kama sadaka za kutikisa, vitakuwa vyako. Ninakupa wewe, wanao na binti zako kuwa haki yenu milele. Mtu yeyote katika jamaa yako asiye najisi anaweza kula vitu hivyo. “Ninakupa vitu vyote vizuri vinavyotokana na malimbuko ambayo Waisraeli hunitolea: Mafuta safi, divai na nafaka. Mazao yote ya kwanza ya matunda mabivu ya mashamba yao ambayo wataniletea mimi, yatakuwa yako. Kila mtu asiye najisi katika jamaa yako anaweza kula. Kila kitu kilichowekwa wakfu nchini Israeli kitakuwa chenu. “Kila mzaliwa wa kwanza ambaye Waisraeli watanitolea, akiwa mzaliwa wa kwanza wa binadamu, au wa mnyama, atakuwa wako. Walakini huna budi kuwakomboa wazaliwa wa kwanza wote wa binadamu, na kila mzaliwa wa kwanza wa mnyama aliye najisi ni lazima akombolewe. Wazaliwa hao wa kwanza watakombolewa wakiwa wenye umri wa mwezi mmoja kwa kulipiwa fedha shekeli tano, kulingana na vipimo vya hema takatifu. Lakini wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe, kondoo au mbuzi wasikombolewe; hao ni watakatifu. Damu yao utainyunyizia madhabahu na mafuta yao utayateketeza kuwa sadaka ya kuteketezwa ambayo ni harufu nzuri inipendezayo mimi Mwenyezi-Mungu. Nyama yao unaweza kuila, kama vile kidari na mguu wa nyuma wa kulia vinavyotolewa kama sadaka ya kutikisa. “Ninakupa wewe, wanao na binti zako, vitu vyote ambavyo watu wa Israeli hunitolea; hivyo ni haki yenu daima. Hili ni agano la milele mbele yangu ambalo ni kwa ajili yako na wazawa wako.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Wewe hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala kuwa na fungu lako miongoni mwao; mimi ndimi fungu lako na urithi wako kati ya Waisraeli.” “Kuhusu Walawi, hao nimewapa zaka zote ambazo Waisraeli hunitolea kuwa urithi wao. Haya yatakuwa malipo yao kwa huduma wanayotoa katika kulitunza hema langu la mkutano. Na tangu sasa, watu wengine wa Israeli wasilikaribie hema la mkutano wasije wakatenda dhambi na kujiletea kifo. Lakini Walawi peke yao ndio watakaohudumu katika hema la mkutano; na kuwajibika kikamilifu juu yake. Hili ni sharti la kudumu katika vizazi vyenu vyote. Walawi hawatakuwa na mali ya kurithi nchini Israeli, kwa sababu zaka wanazonitolea Waisraeli nimewapa kuwa urithi wao. Ndio maana nimesema kwamba wao hawatakuwa na urithi kati ya Waisraeli.” Kisha, Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Tena utawaambia Walawi maagizo yafuatayo: Wakati mtakapopokea zaka ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa kutoka kwa Waisraeli iwe urithi wenu, mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sehemu moja ya kumi ya zaka hiyo. Sadaka hii yenu itakubaliwa kuwa kama malimbuko ya nafaka au kama zabibu anazonitolea mkulima. Basi, ndivyo mtakavyonitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za zaka mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Zaka hiyo mtakayonitolea mimi Mwenyezi-Mungu mtampa kuhani Aroni. Kutokana na matoleo yote mtakayopokea, mtamtolea Mwenyezi-Mungu zaka ya sehemu iliyo bora kuliko zote na takatifu. Kwa hiyo utawaambia: Mkishanitolea sehemu bora kuliko zote, sehemu itakayobakia itakuwa yenu, kama ilivyo kwa mkulima ambaye huchukua kinachobakia baada ya kutoa sadaka zake za mazao ya kwanza ya nafaka na zabibu. Nanyi mtakula kilichotolewa mkiwa mahali popote pale pamoja na jamaa zenu maana ni ujira wenu kwa sababu ya huduma yenu katika hema la mkutano. Hamtakuwa na hatia yoyote mkila vitu hivyo, iwapo kama mmemtolea Mwenyezi-Mungu sehemu bora kuliko zote, nanyi hamtavikufuru vitu vitakatifu vya Waisraeli na kufa.”
Hesabu 18:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu. Na ndugu zako nao, kabila la Lawi, kabila la baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungane nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi. Nao watahudumu kwa kufuata amri yako, na kuhudumu hemani pote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi. Nao watataambatana nawe, na kuhudumu katika hema ya kukutania, kwa ajili ya huduma yote ya hema; na mgeni asiwakaribie ninyi. Nanyi mtahudumu katika patakatifu na huduma ya madhabahuni, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena. Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa BWANA, wahudumu katika hema ya kukutania. Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa. Kisha BWANA akamwambia Haruni, Tazama, nimekupa wewe ulinzi wa sadaka zangu za kuinuliwa, maana, vitu vyote vya hao wana wa Israeli vilivyowekwa wakfu; nimekupa wewe na wanao vitu hivyo kwa ajili ya kule kutiwa mafuta kwenu, kuwa haki yenu milele. Vitu hivi vitakuwa vyako katika vile vilivyo vitakatifu sana, visiteketezwe motoni; matoleo yao yote, maana, kila sadaka yao ya unga, na kila sadaka yao ya dhambi, na kila sadaka yao ya hatia watakayonitolea, vitakuwa vitakatifu sana kwa ajili yako wewe na kwa wanao. Utakula vitu hivyo kuwa ni vitu vitakatifu sana; kila mwanamume atakula vitu hivyo; vitakuwa vitakatifu kwako wewe. Tena kitu hiki ni chako; ile sadaka ya kuinuliwa ya kipawa chao, maana, sadaka za kutikiswa zote za wana wa Israeli; hizi nimekupa wewe, na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu milele; kila mtu katika nyumba yako aliye safi atakula katika hizo. Yaliyo mazuri katika mafuta, na yaliyo mazuri ya mavuno ya zabibu, na ya mavuno ya nafaka, malimbuko yake watakayompa BWANA, hayo nimekupa wewe. Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea BWANA, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo. Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako. Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsogezea BWANA cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa. Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini). Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, iwe harufu ya kupendeza. Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kulia, itakuwa yako. Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa BWANA, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za BWANA kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe. Kisha BWANA akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lolote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli. Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania. Mwanzo wa sasa wana wa Israeli wasikaribie hema ya kukutania, wasije wakachukua dhambi, nao wakafa. Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi. Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi wowote. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka. Na sadaka yenu ya kuinuliwa itahesabiwa kwenu, kama ndiyo nafaka ya sakafu ya kupuria, na kama kujaa kwake kinu cha kusindikia zabibu. Hivyo ninyi nanyi mtasongeza sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA katika zaka zenu zote, mpokeazo mikononi mwa wana wa Israeli; kwa hiyo mtampa Haruni kuhani hiyo sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA. Katika vipawa vyenu vyote mtasongeza kila sadaka ya kuinuliwa ya BWANA, ya wema wake wote, hiyo sehemu yake iliyowekwa takatifu. Kwa ajili ya hayo utawaambia, Mtakapoinua humo hayo yaliyo mema, ndipo yatahesabiwa kuwa ya Walawi, kama mavuno ya sakafu ya kupuria nafaka, na kama mavuno ya kinu cha kusindikia zabibu. Nanyi mtakula hayo kila mahali, ninyi na watu wa nyumbani mwenu; kwa kuwa ni thawabu yenu badala ya utumishi wenu katika hema ya kukutania. Nanyi hamtachukua dhambi kwa ajili yake, hapo mtakapokwisha kuinua humo hayo mema yake; lakini msivitie unajisi vile vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, ili msife.
Hesabu 18:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu. Na ndugu zako nao, kabila ya Lawi, kabila ya baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungwe nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi. Nao watashika ulinzi kwa amri yako, na ulinzi wa Hema yote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi. Nao wataungwa nawe, na kuushika ulinzi wa hema ya kukutania, kwa ajili ya utumishi wote wa hema; na mgeni asiwakaribie ninyi. Nanyi mtashika ulinzi wa patakatifu, na ulinzi wa madhabahu, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena. Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa BWANA, waufanye utumishi wa hema ya kukutania. Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa. Kisha BWANA akamwambia Haruni, Tazama, nimekupa wewe ulinzi wa sadaka zangu za kuinuliwa, maana, vitu vyote vya hao wana wa Israeli vilivyowekwa wakfu; nimekupa wewe na wanao vitu hivyo kwa ajili ya kule kutiwa mafuta kwenu, kuwa haki yenu milele. Vitu hivi vitakuwa vyako katika vile vilivyo vitakatifu sana, visiteketezwe motoni; matoleo yao yote, maana, kila sadaka yao ya unga, na kila sadaka yao ya dhambi, na kila sadaka yao ya hatia watakayonitolea, vitakuwa vitakatifu sana kwa ajili yako wewe na kwa wanao. Utakula vitu hivyo kuwa ni vitu vitakatifu sana; kila mume atakula vitu hivyo; vitakuwa vitakatifu kwako wewe. Tena kitu hiki ni chako; ile sadaka ya kuinuliwa ya kipawa chao, maana, sadaka za kutikiswa zote za wana wa Israeli; hizi nimekupa wewe, na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu milele; kila mtu katika nyumba yako aliye safi atakula katika hizo. Yaliyo mazuri katika mafuta, na yaliyo mazuri ya mavuno ya zabibu, na ya mavuno ya nafaka, malimbuko yake watakayompa BWANA, amekupa wewe hayo. Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea BWANA, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo. Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako. Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsongezea BWANA cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa. Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini). Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng’ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, iwe harufu ya kupendeza. Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kuume, itakuwa yako. Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa BWANA, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za BWANA kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe. Kisha BWANA akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lo lote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli. Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania. Mwanzo wa sasa wana wa Israeli wasikaribie hema ya kukutania, wasije wakachukua dhambi, nao wakafa. Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi. Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka. Na sadaka yenu ya kuinuliwa itahesabiwa kwenu, kama ndiyo nafaka ya sakafu ya kupuria, na kama kujaa kwake kinu cha kushindikia zabibu. Hivyo ninyi nanyi mtasongeza sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA katika zaka zenu zote, mpokeazo mikononi mwa wana wa Israeli; kwa hiyo mtampa Haruni kuhani hiyo sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA. Katika vipawa vyenu vyote mtasongeza kila sadaka ya kuinuliwa ya BWANA, ya wema wake wote, hiyo sehemu yake iliyowekwa takatifu. Kwa ajili ya hayo utawaambia, Mtakapoinua humo hayo yaliyo mema, ndipo yatahesabiwa kuwa ya Walawi, kama kuongea kwake sakafu ya kupuria nafaka, na kama maongeo ya kinu cha kushindikia zabibu. Nanyi mtakula hayo kila mahali, ninyi na watu wa nyumbani mwenu; kwa kuwa ni thawabu yenu badala ya utumishi wenu katika hema ya kukutania. Nanyi hamtachukua dhambi kwa ajili yake, hapo mtakapokwisha kuinua humo hayo mema yake; lakini msivitie unajisi vile vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, ili msife.
Hesabu 18:1-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Haruni, “Wewe, wanao na jamaa ya baba yako mtawajibika kwa makosa dhidi ya mahali patakatifu, na wewe na wanao peke yenu ndio mtakaowajibika kwa makosa dhidi ya ukuhani. Walete Walawi wenzako kutoka kabila la baba zako ili waungane nanyi na kuwasaidia wakati wewe na wanao mnapohudumu mbele ya Hema la Ushuhuda. Watawajibika kwenu na watafanya kazi zote za Hema, lakini kamwe wasisogelee vifaa vya patakatifu au madhabahu, la sivyo wao na ninyi mtakufa. Watajiunga nanyi na watawajibika kwa utunzaji wa Hema la Kukutania, yaani kazi zote kwenye Hema, wala hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kusogea karibu hapo mlipo. “Mtawajibika katika utunzaji wa mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu isiwaangukie Waisraeli tena. Mimi mwenyewe nimewachagua Walawi wenzenu kutoka miongoni mwa Waisraeli kama zawadi kwenu, waliowekwa wakfu kwa BWANA ili kufanya kazi katika Hema la Kukutania. Lakini ni wewe tu na wanao mtakaoweza kutumika kama makuhani kuhusiana na kila kitu kwenye madhabahu na ndani ya pazia. Ninawapa utumishi wa ukuhani kama zawadi. Mtu mwingine yeyote atakayekaribia mahali patakatifu ni lazima auawe.” Kisha BWANA akamwambia Haruni, “Mimi mwenyewe nimekuweka kuwa mwangalizi wa sadaka zote zitakazotolewa kwangu; matoleo yote matakatifu Waisraeli wanayonipa ninakupa wewe na wanao kuwa sehemu yenu na fungu lenu la milele. Mtachukua sehemu ya yale matoleo matakatifu sana ambayo hayateketezwi kwa moto. Kutoka kwa matoleo yote wanayoniletea kama sadaka takatifu sana, ziwe za nafaka, au za dhambi, au za makosa, sehemu ile itakuwa yako na wanao. Mtaila kama kitu kilicho kitakatifu sana; kila mwanaume ataila. Ni lazima mtaiheshimu kama takatifu. “Hiki pia ni chako: chochote kilichotengwa kutoka matoleo yote ya sadaka za kuinuliwa za Waisraeli. Haya ninakupa wewe, na wanao wa kiume na wa kike kuwa sehemu yenu ya milele. Kila mmoja wa nyumba yako ambaye ametakasika anaweza kuyala. “Ninawapa mafuta ya zeituni yaliyo bora kuliko yote, na divai mpya iliyo bora kuliko zote na nafaka wanazompa BWANA kama malimbuko katika mavuno yao. Malimbuko yote ya nchi ambayo wanamletea BWANA yatakuwa yenu. Kila mmoja nyumbani mwako ambaye ametakasika anaweza kula. “Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwa BWANA ni chenu. Kila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwa BWANA ni wenu. Lakini ni lazima mtamkomboa kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi. Watakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tano za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini. “Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kuwa sadaka inayotolewa kwa moto, harufu nzuri inayompendeza BWANA. Nyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kuinuliwa na paja la mguu wa kulia. Chochote kitakachotengwa kutoka sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtolea BWANA, ninakupa wewe, na wanao wa kiume na wa kike kuwa fungu lenu la milele. Ni agano la milele la chumvi mbele za BWANA, kwako na wazao wako.” BWANA akamwambia Haruni, “Hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli. “Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania. Kuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa. Ni Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wowote miongoni mwa Waisraeli. Badala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwa BWANA kuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuwahusu: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ” BWANA akamwambia Musa, “Sema na Walawi na uwaambie: ‘Mtakapopokea zaka kutoka kwa Waisraeli ninayowapa kama urithi wenu kutoka kwao, ni lazima mtoe sehemu ya kumi ya hiyo zaka kuwa sadaka kwa BWANA, iwe zaka ya hiyo zaka. Sadaka yenu itahesabiwa kwenu kama nafaka kutoka sakafu ya kupuria, au divai kutoka shinikizo la kukamulia zabibu. Kwa njia hii, ninyi pia mtatoa sadaka kwa BWANA kutoka zaka zote mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Kutoka kwa zaka hizi, ni lazima mtoe sehemu ya BWANA kwa Haruni, kuhani. Ni lazima mtoe kama sehemu ya BWANA iliyo nzuri sana tena ile sehemu iliyo takatifu sana kuliko zote ya kile kitu mlichopewa.’ “Waambie Walawi: ‘Mtakapotoa sehemu zilizo bora sana, itahesabiwa kwenu kama mazao ya sakafu ya kupuria nafaka, au ya shinikizo la kukamulia zabibu. Ninyi na watu wa nyumbani mwenu mnaweza kula sehemu iliyobaki mahali popote, kwani ndio ujira wenu kwa ajili ya kazi yenu katika Hema la Kukutania. Kwa kutoa sehemu zake zilizo bora sana, hamtakuwa na hatia katika jambo hili; ndipo hamtatia unajisi sadaka takatifu za Waisraeli, nanyi hamtakufa.’ ”