Hesabu 16:26-35
Hesabu 16:26-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Alipofika, akawaambia watu, “Tafadhalini ondokeni kwenye hema za watu hawa waovu na msiguse kitu chao chochote, msije mkaangamizwa pamoja nao kwa sababu ya dhambi zao zote.” Watu wakaondoka kwenye makao ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu wakatoka mahemani mwao na kusimama mlangoni wakiandamana na wake zao na watoto wao wote hata wale wanaonyonya. Hapo Mose akawaambia watu, “Hivi ndivyo mtakavyotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyenituma kufanya mambo haya yote, wala siyo kwa matakwa yangu mwenyewe. Watu hawa wakifa kifo cha kawaida, au wakipatwa na maafa kama watu wengine, basi jueni kuwa Mwenyezi-Mungu hakunituma. Lakini Mwenyezi-Mungu akifanya jambo ambalo halijapata kutendeka, ardhi ikafunuka na kuwameza watu hawa pamoja na kila kitu chao, wakaenda kuzimu wakiwa hai, basi mtajua kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi-Mungu.” Mara tu alipomaliza kusema maneno hayo yote, ardhi chini ya Dathani na Abiramu ikafunuka kuwameza watu hao, jamaa zao, pamoja na wafuasi wote wa Kora na mali zao zote. Basi, wao, pamoja na vyote vilivyokuwa vyao wakashuka kuzimu hali wangali hai. Ardhi ikawafunika, wote wakatoweka. Waisraeli wote wengine waliokuwa karibu waliposikia vilio vyao walikimbia wakisema, “Tukimbie, ardhi isije ikatumeza na sisi pia.” Kisha Mwenyezi-Mungu akapeleka moto ukawateketeza wale watu 250 waliokwenda kufukiza ubani.
Hesabu 16:26-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao chochote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha kawaida, kama watu wote wafavyo, au kama wataadhibiwa kwa adhabu ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao wakashuka shimoni wakiwa hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wakiwa hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kandokando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.
Hesabu 16:26-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.
Hesabu 16:26-35 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Musa akawaonya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.” Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao. Ndipo Musa akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa BWANA amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu. Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi BWANA hakunituma mimi. Lakini ikiwa BWANA ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau BWANA.” Mara Musa alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka, nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali yao yote. Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kwa kusanyiko. Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!” Moto ukaja kutoka kwa BWANA, ukawateketeza wale watu mia mbili na hamsini waliokuwa wakifukiza uvumba.