Hesabu 16:1-7
Hesabu 16:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu pamoja na watu watatu wa ukoo wa Reubeni: Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, hao wote waliungwa mkono na viongozi mashuhuri 250 waliochaguliwa na jumuiya yote, wakamwasi Mose. Walikusanyika mbele ya Mose na Aroni, wakawaambia, “Nyinyi mmepita kikomo! Jumuiya yote ni takatifu na kila mtu katika jumuiya hii ni mtakatifu, na Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi sote. Mbona sasa nyinyi mnajifanya wakuu wa jumuiya ya Mwenyezi-Mungu?” Mose aliposikia hayo, alijitupa chini kifudifudi. Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake, “Kesho asubuhi, Mwenyezi-Mungu ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, naye atakayemchagua, atamwezesha kukaribia madhabahuni. Basi, fanyeni hivi: Asubuhi, wewe pamoja na wafuasi wako, mtachukua vyetezo, mweke makaa ya moto ndani na kutia ubani juu yake, kisha mtavipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Halafu tutaona ni nani aliyechaguliwa na Mwenyezi-Mungu. Nyinyi Walawi mmepita kikomo!”
Hesabu 16:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadhaa wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yuko kati yao; ya nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA? Musa aliposikia maneno haya, akaanguka kifudifudi; kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu atakayechaguliwa na BWANA, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.
Hesabu 16:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yu kati yao; n’nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA? Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu BWANA atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.
Hesabu 16:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Pelethi, wakachukua baadhi ya watu, wakainuka dhidi ya Musa. Pamoja nao walikuwa wanaume Waisraeli mia mbili na hamsini, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko. Wakaja kama kikundi kuwapinga Musa na Haruni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili wote ni watakatifu, kila mmoja wao, naye BWANA yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la BWANA?” Musa aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi. Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi BWANA ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye. Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo, kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za BWANA. Mtu ambaye BWANA atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”