Hesabu 16:1-40
Hesabu 16:1-40 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu pamoja na watu watatu wa ukoo wa Reubeni: Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, hao wote waliungwa mkono na viongozi mashuhuri 250 waliochaguliwa na jumuiya yote, wakamwasi Mose. Walikusanyika mbele ya Mose na Aroni, wakawaambia, “Nyinyi mmepita kikomo! Jumuiya yote ni takatifu na kila mtu katika jumuiya hii ni mtakatifu, na Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi sote. Mbona sasa nyinyi mnajifanya wakuu wa jumuiya ya Mwenyezi-Mungu?” Mose aliposikia hayo, alijitupa chini kifudifudi. Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake, “Kesho asubuhi, Mwenyezi-Mungu ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, naye atakayemchagua, atamwezesha kukaribia madhabahuni. Basi, fanyeni hivi: Asubuhi, wewe pamoja na wafuasi wako, mtachukua vyetezo, mweke makaa ya moto ndani na kutia ubani juu yake, kisha mtavipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Halafu tutaona ni nani aliyechaguliwa na Mwenyezi-Mungu. Nyinyi Walawi mmepita kikomo!” Mose akaendelea kumwambia Kora, “Sikilizeni, enyi Walawi! Je, mnaona ni jambo dogo kwenu kwamba Mungu wa Israeli amewateua nyinyi miongoni mwa jumuiya ya Israeli, ili muweze kumkaribia, mhudumie katika hema la Mwenyezi-Mungu na kuihudumia na kuitumikia jamii yote? Amewatunukia heshima ya kuwa karibu naye, nyinyi pamoja na Walawi wenzenu wote. Sasa mnataka kunyakua hata ukuhani? Kwa hiyo wewe na kundi lako mnamshambulia Mwenyezi-Mungu. Nyinyi mnamnungunikia Aroni, lakini ukweli ni kwamba mnanungunika dhidi ya Mungu.” Mose alituma ujumbe kwa Dathani na Abiramu wana wa Eliabu ili waitwe, lakini wao wakasema, “Hatutakuja! Je, ni jambo dogo kwamba umetutoa Misri, nchi inayotiririka maziwa na asali, ili uje kutuua humu jangwani? Tena, unajifanya mkuu wetu! Zaidi ya hayo, hukutuleta kwenye nchi inayotiririka maziwa na asali, wala kutupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Unafikiri utawafanya hawa watu kuwa vipofu? Hatutakuja!” Mose alikasirika mno, akamwambia Mwenyezi-Mungu “Usizikubali sadaka za watu hawa. Mimi sijachukua punda wa mtu yeyote, wala sijamdhuru mtu!” Mose akamwambia Kora, “Kesho usikose kuja pamoja na wafuasi wako mbele ya Mwenyezi-Mungu. Aroni pia atakuwapo. Kila mmoja wenu achukue chetezo chake, na kutia ubani, kisha atakipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu; kwa jumla vitakuwa vyetezo 250; wewe pia na Aroni, kila mmoja atakuwa na chetezo chake.” Basi, kila mmoja wao akachukua chetezo chake, akatia makaa ya moto na ubani, kisha wakaenda na kusimama mlangoni mwa hema la mkutano, pamoja na Mose na Aroni. Naye Kora akawakusanya watu wote pamoja, wakasimama mbele ya Mose na Aroni ambao walikuwa mlangoni mwa hema la mkutano. Ndipo utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea watu wote! Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Jitengeni na watu hawa, niwaangamize sasa hivi.” Lakini Mose na Aroni wakajitupa chini kifudifudi na kusema, “Ee Mwenyezi-Mungu uliye asili ya uhai wa binadamu wote. Je, mtu mmoja akikukosea, utaikasirikia jumuiya nzima?” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Waambie watu waondoke karibu na makao ya hema ya Kora, Dathani na Abiramu.” Basi, Mose akaenda kwa Dathani na Abiramu, akifuatwa na wazee wa Israeli. Alipofika, akawaambia watu, “Tafadhalini ondokeni kwenye hema za watu hawa waovu na msiguse kitu chao chochote, msije mkaangamizwa pamoja nao kwa sababu ya dhambi zao zote.” Watu wakaondoka kwenye makao ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu wakatoka mahemani mwao na kusimama mlangoni wakiandamana na wake zao na watoto wao wote hata wale wanaonyonya. Hapo Mose akawaambia watu, “Hivi ndivyo mtakavyotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyenituma kufanya mambo haya yote, wala siyo kwa matakwa yangu mwenyewe. Watu hawa wakifa kifo cha kawaida, au wakipatwa na maafa kama watu wengine, basi jueni kuwa Mwenyezi-Mungu hakunituma. Lakini Mwenyezi-Mungu akifanya jambo ambalo halijapata kutendeka, ardhi ikafunuka na kuwameza watu hawa pamoja na kila kitu chao, wakaenda kuzimu wakiwa hai, basi mtajua kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi-Mungu.” Mara tu alipomaliza kusema maneno hayo yote, ardhi chini ya Dathani na Abiramu ikafunuka kuwameza watu hao, jamaa zao, pamoja na wafuasi wote wa Kora na mali zao zote. Basi, wao, pamoja na vyote vilivyokuwa vyao wakashuka kuzimu hali wangali hai. Ardhi ikawafunika, wote wakatoweka. Waisraeli wote wengine waliokuwa karibu waliposikia vilio vyao walikimbia wakisema, “Tukimbie, ardhi isije ikatumeza na sisi pia.” Kisha Mwenyezi-Mungu akapeleka moto ukawateketeza wale watu 250 waliokwenda kufukiza ubani. Baada ya hayo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni avitoe hivyo vyetezo penye moto, akautapanye mbali moto uliomo ndani, maana vyetezo hivyo ni vitakatifu. Vimekuwa vitakatifu kwa sababu watu hawa walivileta madhabahuni pa Mwenyezi-Mungu. Basi, vichukue vyetezo vya watu hao waliouawa kwa sababu ya dhambi zao, vifuliwe kuwa vyembamba ili viwe kifuniko cha madhabahu. Hili litakuwa onyo kwa Waisraeli wote.” Basi, kuhani Eleazari alivichukua vyetezo hivyo vya shaba ambavyo vililetwa mbele ya Mwenyezi-Mungu na wale watu walioteketezwa vikafuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu. Hili lilikuwa onyo kwa Waisraeli kwamba mtu yeyote ambaye si kuhani, yaani asiye wa ukoo wa Aroni asiende madhabahuni kumfukizia Mwenyezi-Mungu ubani. La sivyo ataangamizwa kama Kora na wafuasi wake. Haya yote yalitendeka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Eleazari kwa njia ya Mose.
Hesabu 16:1-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadhaa wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yuko kati yao; ya nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA? Musa aliposikia maneno haya, akaanguka kifudifudi; kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu atakayechaguliwa na BWANA, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi. Musa akamwambia Kora, Sikilizeni basi, enyi Wana wa Lawi; Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mhudumu katika maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha BWANA; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia? Kisha Musa akatuma ujumbe wa kuwaita Dathani na Abiramu wana wa Eliabu; nao wakasema, “Hatuji sisi”; je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyobubujika na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. Musa akakasirika sana, akamwambia BWANA. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote kuweni hapa mbele ya BWANA kesho, wewe, na wao, na Haruni; mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za BWANA, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja. Nao wakaanguka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote? BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu. Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakafuatana naye. Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao chochote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha kawaida, kama watu wote wafavyo, au kama wataadhibiwa kwa adhabu ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao wakashuka shimoni wakiwa hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wakiwa hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kandokando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu; vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuziumiza nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za BWANA, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli. Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu; viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni yeyote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za BWANA; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama BWANA alivyonena naye, kwa kupitia kwa Musa.
Hesabu 16:1-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yu kati yao; n’nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA? Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi BWANA ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za BWANA kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu BWANA atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi. Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha BWANA; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung’unikia? Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. Musa akakasirika sana, akamwambia BWANA. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya BWANA kesho, wewe, na wao, na Haruni; mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za BWANA, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa BWANA ukatokea mbele ya mkutano wote. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja. Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote? BWANA akasema na Musa, na kumwambia, Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu. Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye. Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba BWANA amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi BWANA hakunituma mimi. Lakini BWANA akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau BWANA Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. Kisha moto ukatoka kwa BWANA, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu; vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuzihasiri nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za BWANA, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli. Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu; viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni awaye yote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za BWANA; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama BWANA alivyonena naye, kwa mkono wa Musa.
Hesabu 16:1-40 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Pelethi, wakachukua baadhi ya watu, wakainuka dhidi ya Musa. Pamoja nao walikuwa wanaume Waisraeli mia mbili na hamsini, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko. Wakaja kama kikundi kuwapinga Musa na Haruni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili wote ni watakatifu, kila mmoja wao, naye BWANA yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la BWANA?” Musa aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi. Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi BWANA ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye. Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo, kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za BWANA. Mtu ambaye BWANA atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!” Pia Musa akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni. Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka kusanyiko lote la Israeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia? Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye; lakini sasa unajaribu kuchukua ukuhani pia. Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume cha BWANA. Haruni ni nani kwamba ninyi mnungʼunike dhidi yake?” Kisha Musa akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji! Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi inayotiririka maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu? Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayangʼoa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!” Ndipo Musa akakasirika sana na kumwambia BWANA, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua chochote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.” Musa akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele za BWANA: wewe na hao wenzako, pamoja na Haruni. Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani, vyetezo mia mbili na hamsini kwa jumla, na kukileta mbele za BWANA. Wewe na Haruni mtaleta vyetezo vyenu pia.” Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani, na kusimama pamoja na Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania. Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Musa na Haruni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa BWANA ukatokea kwa kusanyiko lote. BWANA akamwambia Musa na Haruni, “Jitengeni na kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.” Lakini Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?” Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Waambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ” Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye. Musa akawaonya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu chochote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.” Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao. Ndipo Musa akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa BWANA amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu. Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi BWANA hakunituma mimi. Lakini ikiwa BWANA ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau BWANA.” Mara Musa alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka, nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali yao yote. Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka kwa kusanyiko. Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!” Moto ukaja kutoka kwa BWANA, ukawateketeza wale watu mia mbili na hamsini waliokuwa wakifukiza uvumba. BWANA akamwambia Musa, “Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Haruni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu: vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele za BWANA na vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.” Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu, kama vile BWANA alivyomwelekeza kupitia Musa. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Haruni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele za BWANA, la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.