Hesabu 14:5-10
Hesabu 14:5-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo, Mose na Aroni wakaanguka kifudifudi mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli. Yoshua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ambao walikuwa miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi, wakazirarua nguo zao na kuiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Nchi tuliyokwenda kuipeleleza ni nzuri kupita kiasi. Ikiwa Mwenyezi-Mungu amependezwa nasi, atatupeleka huko na kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali. Mradi tu msimwasi Mwenyezi-Mungu, wala msiwaogope wenyeji wa nchi hiyo. Maana wao ni mboga tu kwetu; kinga yao imekwisha ondolewa kwao, naye Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi; msiwaogope!” Lakini jumuiya yote ikatishia kuwapiga mawe. Ghafla, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatokea juu ya hema la mkutano, mbele ya Waisraeli wote.
Hesabu 14:5-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; kinga iliyokuwa juu yao imeondolewa, naye BWANA yuko pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.
Hesabu 14:5-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.
Hesabu 14:5-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli waliokusanyika hapo. Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale walioenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao, wakasema na kusanyiko lote la Waisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita kati yake kuipeleleza ni nzuri sana. Ikiwa BWANA anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi inayotiririka maziwa na asali, naye atatupatia nchi hiyo. Ila tu msimwasi BWANA. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini BWANA yupo pamoja nasi. Msiwaogope.” Lakini kusanyiko lote wakazungumza kuhusu kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika Hema la Kukutania kwa Waisraeli wote.