Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hesabu 14:1-45

Hesabu 14:1-45 Biblia Habari Njema (BHN)

Jumuiya yote ya Waisraeli ikaangua kilio kikubwa, watu wakalia usiku ule. Waliwalalamikia Mose na Aroni wakisema, “Afadhali tungefia Misri! Afadhali tungefia papa hapa jangwani! Kwa nini Mwenyezi-Mungu anatupeleka katika nchi hiyo? Tutauawa vitani, na wake zetu na watoto wetu watachukuliwa mateka! Si afadhali turudi Misri?” Basi wakaanza kuambiana, “Na tuchague kiongozi, turudi Misri.” Hapo, Mose na Aroni wakaanguka kifudifudi mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli. Yoshua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ambao walikuwa miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi, wakazirarua nguo zao na kuiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Nchi tuliyokwenda kuipeleleza ni nzuri kupita kiasi. Ikiwa Mwenyezi-Mungu amependezwa nasi, atatupeleka huko na kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali. Mradi tu msimwasi Mwenyezi-Mungu, wala msiwaogope wenyeji wa nchi hiyo. Maana wao ni mboga tu kwetu; kinga yao imekwisha ondolewa kwao, naye Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi; msiwaogope!” Lakini jumuiya yote ikatishia kuwapiga mawe. Ghafla, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatokea juu ya hema la mkutano, mbele ya Waisraeli wote. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Watu hawa watanidharau mpaka lini? Na, mpaka lini wataendelea kutoniamini, hata pamoja na miujiza yote niliyotenda kati yao? Nitawapiga kwa maradhi mabaya na kuwatupilia mbali; lakini, kutokana nawe, nitaunda taifa lingine kubwa, lenye nguvu kuliko wao.” Lakini Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Uliwatoa watu hawa nchini Misri kwa nguvu yako. Wamisri watakaposikia kwamba umewatenda hivyo watu wako, watawapasha habari wakazi wa nchi hii. Maana watu hawa wamekwisha pata habari kwamba wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u pamoja nasi; maana wewe, ee Mwenyezi-Mungu, unaonekana waziwazi wingu lako linaposimama juu yetu, na kwamba wewe hututangulia mchana kwa nguzo ya wingu na usiku kwa nguzo ya moto. Sasa basi, ukiwaua watu wako wote kwa mara moja, mataifa ambayo yamekwisha sikia sifa zako yatasema, ‘Mwenyezi-Mungu aliwaua watu wake jangwani kwa sababu alishindwa kuwapeleka katika nchi aliyoahidi kuwapa.’ Basi, sasa nakusihi, ee Mwenyezi-Mungu, utuoneshe uwezo wako kwa kufanya kama ulivyotuahidi uliposema, ‘Mimi Mwenyezi-Mungu si mwepesi wa hasira, ni mwenye fadhili nyingi, na ni mwenye kusamehe uovu na makosa. Lakini kwa vyovyote vile sitakosa kuwaadhibu watoto na wajukuu hadi kizazi cha tatu na cha nne kwa dhambi za wazazi wao.’ Nakusihi uwasamehe watu hawa dhambi zao, kadiri ya fadhili zako nyingi kama vile ulivyowasamehe tangu watoke Misri hadi sasa.” Mwenyezi-Mungu akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba. Lakini kwa kweli, kama niishivyo na kadiri dunia itakavyojaa utukufu wangu, hakuna hata mmoja wao ambaye amewahi kuuona utukufu wangu na miujiza yangu niliyoifanya Misri na jangwani kisha akazidi kunijaribu mara hizi zote bila ya kutii sauti yangu, ataiona nchi ile niliyoapa kuwapatia babu zao; kadhalika hata wale wanaonidharau pia hawataiona. Bali kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ni tofauti, na amenitii kikamilifu, nitamfikisha kwenye nchi hiyo aliyoingia na wazawa wake wataimiliki. Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanakaa katika mabonde ya nchi hiyo, kesho geukeni nyuma mwende jangwani kuelekea bahari ya Shamu.” Kisha Mwenyezi-Mungu akamwuliza Mose na Aroni, “Kundi hili la watu waovu litaendelea kuninungunikia mpaka lini? Nimechoka na haya manunguniko ya Waisraeli juu yangu! Sasa wajibu hivi: Kama niishivyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, nitawatendeeni yaleyale niliyosikia mkiyasema: Mtakufa na miili yenu itatupwa humuhumu jangwani, kwa sababu mmenungunika dhidi yangu, hakuna hata mmoja wenu mwenye umri wa kuanzia miaka ishirini na zaidi, atakayeingia katika nchi hiyo ambayo niliapa kuwapa iwe yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Nyinyi mlisema kuwa watoto wenu watatekwa nyara, lakini mimi nitawafikisha watoto wenu kwenye nchi mliyoidharau, ili waijue na iwe makao yao. Lakini nyinyi, mtafia humuhumu jangwani. Watoto wenu watatangatanga na kutaabika humu jangwani kwa muda wa miaka arubaini kwa ajili ya ukosefu wenu wa imani mpaka mtu wenu wa mwisho atakapofia jangwani. Kutokana na makosa yenu, mtataabika kwa muda wa miaka arubaini, sawa na zile siku arubaini mlizopeleleza ile nchi, mwaka mmoja kwa kila siku moja; mtatambua kwamba mimi nimechukizwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema: Hakika nitawatenda hivyo nyinyi nyote mliokusanyika hapa kunipinga. Wote wataishia humuhumu jangwani na ni humu watakamofia.” Wale watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza ile nchi waliorudi na kusababisha watu wamnungunikie Mwenyezi-Mungu kwa kuleta taarifa mbaya dhidi ya nchi, watu hao waliotoa taarifa ya uovu kuhusu hiyo nchi, walikufa kwa pigo mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, walibaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi. Naye Mose aliwaambia Waisraeli wote nao walilia kwa uchungu mwingi. Kesho yake, waliamka alfajiri na mapema wakaenda sehemu za milimani, wakisema, “Sasa tuko tayari kabisa kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alituahidi. Tunakiri kwamba tulitenda dhambi.” Lakini Mose akasema, “Sasa mbona mnavunja agizo la Mwenyezi-Mungu? Hivyo hamtafaulu! Msiende huko milimani msije mkapigwa bure na adui zenu, maana, Mwenyezi-Mungu hayuko pamoja nanyi. Mkiwakabili Waamaleki na Wakanaani, mtafia vitani; kwa kuwa mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu, yeye hatakuwa pamoja nanyi.” Hata hivyo, wao walisisitiza kwenda juu milimani, ingawa sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wala Mose hakuondoka kambini. Ndipo Waamaleki na Wakanaani, waliokuwa wakiishi katika nchi hiyo ya milima, wakashuka, wakawashambulia na kuwashinda. Wakawafukuza mpaka mji wa Horma.

Shirikisha
Soma Hesabu 14

Hesabu 14:1-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe kiongozi, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; kinga iliyokuwa juu yao imeondolewa, naye BWANA yuko pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote. BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hadi lini? Wasiniamini hadi lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao. Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao. Basi Musa akamwambia BWANA, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao; kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe BWANA u kati ya watu hawa; maana, wewe BWANA waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku. Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema, Ni kwa sababu yeye BWANA hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani. Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema, BWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yoyote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne. Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa; lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA; kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye amenifuata kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na wazao wake wataimiliki. Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Je! Nivumilie na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hadi lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo. Waambieni, Kama niishivyo, asema BWANA, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia, hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliapa kwa kuinua mkono wangu, kwamba nitawafanyia makao humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi mliyoikataa ninyi. Lakini katika habari zenu, maiti zenu zitaanguka katika jangwa hili. Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arubaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hadi maiti zenu zitakapoangamia jangwani. Kwa jumla ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arubaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arubaini, nanyi mtakujua kuchukizwa kwangu. Mimi BWANA nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko watakakokufa. Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi, watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya BWANA. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi. Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaomboleza sana. Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali BWANA alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi. Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyakaidi maagizo ya BWANA? Maana halitafanikiwa jambo hilo. Msikwee, kwa kuwa BWANA hayumo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu. Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimfuate BWANA, kwa hiyo BWANA hatakuwa pamoja nanyi. Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la Agano la BWANA halikutoka humo kambini, wala Musa hakutoka. Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakateremka, wakawapiga na kuwaangusha, hadi wakafika Horma.

Shirikisha
Soma Hesabu 14

Hesabu 14:1-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote. BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao. Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao. Basi Musa akamwambia BWANA, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao; kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe BWANA u kati ya watu hawa; maana, wewe BWANA waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku. Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema, Ni kwa sababu yeye BWANA hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani. Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema, BWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne. Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa; lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa BWANA; kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki. Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo. Waambieni, Kama niishivyo, asema BWANA, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung’unikia, hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa. Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili. Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani. Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu. Mimi BWANA nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko Watakakokufa. Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung’unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi, watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya BWANA. Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi. Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaombolea sana. Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali BWANA alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi. Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyahalifu maagizo ya BWANA? Maana halitafanikiwa jambo hilo. Msikwee, kwa kuwa BWANA hamo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu. Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimwandame BWANA, kwa hiyo BWANA hatakuwa pamoja nanyi. Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la agano la BWANA halikutoka humo maragoni, wala Musa hakutoka. Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakatelemka, wakawapiga na kuwaangusha, hata kufikilia Horma.

Shirikisha
Soma Hesabu 14

Hesabu 14:1-45 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Usiku ule watu wote wa jumuiya walipaza sauti zao na kulia kwa sauti kuu. Waisraeli wote wakanungʼunika dhidi ya Musa na Haruni, na kusanyiko lote wakawaambia, “Laiti tungekuwa tumefia humo nchi ya Misri! Au humu kwenye hili jangwa! Kwa nini BWANA anatuleta katika nchi hii ili tufe kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watachukuliwa kama nyara. Je, isingekuwa bora kwetu kurudi Misri?” Wakasemezana wao kwa wao, “Inatupasa kumchagua kiongozi na kurudi Misri.” Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli waliokusanyika hapo. Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale walioenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao, wakasema na kusanyiko lote la Waisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita kati yake kuipeleleza ni nzuri sana. Ikiwa BWANA anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi inayotiririka maziwa na asali, naye atatupatia nchi hiyo. Ila tu msimwasi BWANA. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini BWANA yupo pamoja nasi. Msiwaogope.” Lakini kusanyiko lote wakazungumza kuhusu kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika Hema la Kukutania kwa Waisraeli wote. BWANA akamwambia Musa, “Watu hawa watanidharau hadi lini? Wataendelea kukataa kuniamini mimi hadi lini, ingawa nimetenda ishara za miujiza miongoni mwao? Nitawapiga kwa tauni na kuwaangamiza, lakini nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa lenye nguvu kuliko wao.” Musa akamwambia BWANA, “Ndipo Wamisri watasikia juu ya jambo hili! Kwa uweza wako uliwapandisha watu hawa kutoka miongoni mwao. Nao watawaambia wenyeji wa nchi hii jambo hili. Wao tayari wameshasikia kwamba wewe, Ee BWANA, upo pamoja na watu hawa, na kuwa wewe, Ee BWANA, umeonekana uso kwa uso, nalo wingu lako hukaa juu yao. Tena wewe unawatangulia kwa nguzo ya wingu mchana na kwa nguzo ya moto usiku. Ikiwa utawaua watu hawa wote mara moja, mataifa ambayo yamesikia taarifa hii kukuhusu wewe watasema, ‘BWANA alishindwa kuwaingiza watu hawa katika nchi aliyowaahidi kwa kiapo; hivyo akawaua jangwani.’ “Basi sasa nguvu za Bwana na zionekane, sawasawa na ulivyosema: ‘BWANA si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo na mwenye kusamehe dhambi na uasi. Lakini haachi kumwadhibu mwenye hatia, huadhibu watoto kwa ajili ya dhambi ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne.’ Kwa kadiri ya upendo wako mkuu, usamehe dhambi ya watu hawa, kama vile ulivyowasamehe tangu walipotoka Misri hadi sasa.” BWANA akajibu, “Nimewasamehe kama ulivyoomba. Hata hivyo, kwa hakika kama niishivyo, na kwa hakika kama utukufu wa BWANA uijazavyo dunia yote, hakuna hata mmoja wa watu hawa ambao waliuona utukufu wangu na ishara za miujiza niliyotenda huko Misri na huko jangwani, lakini ambaye hakunitii na akanijaribu mara hizi kumi, hakuna hata mmoja wao atakayeona nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo. Hakuna hata mmoja ambaye amenidharau atakayeiona. Lakini kwa sababu mtumishi wangu Kalebu ana roho ya tofauti na ananifuata kwa moyo wote, nitamwingiza katika nchi aliyoiendea, nao wazao wake watairithi. Kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani wanaishi katika mabonde, kesho geukeni mwelekee jangwani kwa kufuata njia iendayo Bahari ya Shamu.” BWANA akamwambia Musa na Haruni: “Jumuiya hii ovu itanungʼunika dhidi yangu hadi lini? Nimesikia malalamiko ya hawa Waisraeli wanaonungʼunika. Hivyo waambie, ‘Hakika kama niishivyo, asema BWANA, nitawafanyia vitu vilevile nilivyosikia mkisema: Kila mmoja wenu mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi ambaye alihesabiwa na amenungʼunika dhidi yangu, miili yenu itaanguka katika jangwa hili. Hakuna hata mmoja wenu atakayeingia katika nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kuwa makao yenu, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini watoto wenu ambao mlisema watachukuliwa mateka, nitawaingiza humo ili waifurahie nchi ambayo ninyi mmeikataa. Bali ninyi, miili yenu itaanguka katika jangwa hili. Watoto wenu watakuwa wachungaji wa mifugo hapa kwa miaka arobaini, wakiteseka kwa ajili ya kukosa uaminifu kwenu, hadi mwili wa mtu wenu wa mwisho ulale katika jangwa hili. Kwa miaka arobaini, mwaka mmoja kwa kila siku katika zile siku arobaini mlizoipeleleza nchi, mtateseka kwa ajili ya dhambi zenu, na kujua jinsi ilivyo vibaya kunifanya mimi kuwa adui yenu.’ Mimi BWANA nimesema, na hakika nitafanya mambo haya kwa jumuiya hii yote ovu, ambayo imefungamana pamoja dhidi yangu. Watakutana na mwisho wao katika jangwa hili; hapa ndipo watafia.” Hivyo watu wale ambao Musa alikuwa amewatuma kuipeleleza nchi, waliorudi na kuifanya jumuiya nzima kunungʼunika dhidi ya Musa kwa kueneza taarifa mbaya kuhusu hiyo nchi: watu hawa waliohusika kueneza taarifa mbaya kuhusu hiyo nchi walipigwa na kuanguka kwa tauni mbele za BWANA. Miongoni mwa watu walioenda kuipeleleza hiyo nchi, ni Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune peke yao waliosalia. Musa alipotoa taarifa hii kwa Waisraeli wote, waliomboleza kwa uchungu. Asubuhi na mapema siku iliyofuata, walipanda kilele kirefu cha nchi ya vilima, wakasema, “Tumetenda dhambi. Tutakwea hadi mahali BWANA alipotuahidi.” Lakini Musa akasema, “Kwa nini hamtii amri ya BWANA? Jambo hili halitafanikiwa! Msipande juu, kwa kuwa BWANA hayupo pamoja nanyi. Mtashindwa na adui zenu, kwa kuwa Waamaleki na Wakanaani watapambana nanyi huko. Kwa sababu mmemwacha BWANA, hatakuwa pamoja nanyi, ninyi mtaanguka kwa upanga.” Hata hivyo, kwa kiburi chao walipanda juu kuelekea nchi ya vilima virefu, ijapokuwa Musa hakutoka kambini wala Sanduku la Agano la BWANA. Ndipo Waamaleki na Wakanaani walioishi katika hiyo nchi ya vilima wakateremka na kuwashambulia, wakawapiga njia yote hadi Horma.

Shirikisha
Soma Hesabu 14