Hesabu 14:1-10
Hesabu 14:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Jumuiya yote ya Waisraeli ikaangua kilio kikubwa, watu wakalia usiku ule. Waliwalalamikia Mose na Aroni wakisema, “Afadhali tungefia Misri! Afadhali tungefia papa hapa jangwani! Kwa nini Mwenyezi-Mungu anatupeleka katika nchi hiyo? Tutauawa vitani, na wake zetu na watoto wetu watachukuliwa mateka! Si afadhali turudi Misri?” Basi wakaanza kuambiana, “Na tuchague kiongozi, turudi Misri.” Hapo, Mose na Aroni wakaanguka kifudifudi mbele ya jumuiya yote ya Waisraeli. Yoshua, mwana wa Nuni, na Kalebu, mwana wa Yefune, ambao walikuwa miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi, wakazirarua nguo zao na kuiambia jumuiya yote ya Waisraeli, “Nchi tuliyokwenda kuipeleleza ni nzuri kupita kiasi. Ikiwa Mwenyezi-Mungu amependezwa nasi, atatupeleka huko na kutupa nchi inayotiririka maziwa na asali. Mradi tu msimwasi Mwenyezi-Mungu, wala msiwaogope wenyeji wa nchi hiyo. Maana wao ni mboga tu kwetu; kinga yao imekwisha ondolewa kwao, naye Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi; msiwaogope!” Lakini jumuiya yote ikatishia kuwapiga mawe. Ghafla, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatokea juu ya hema la mkutano, mbele ya Waisraeli wote.
Hesabu 14:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe kiongozi, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; kinga iliyokuwa juu yao imeondolewa, naye BWANA yuko pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.
Hesabu 14:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope. Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.
Hesabu 14:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Usiku ule watu wote wa jumuiya walipaza sauti zao na kulia kwa sauti kuu. Waisraeli wote wakanungʼunika dhidi ya Musa na Haruni, na kusanyiko lote wakawaambia, “Laiti tungekuwa tumefia humo nchi ya Misri! Au humu kwenye hili jangwa! Kwa nini BWANA anatuleta katika nchi hii ili tufe kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watachukuliwa kama nyara. Je, isingekuwa bora kwetu kurudi Misri?” Wakasemezana wao kwa wao, “Inatupasa kumchagua kiongozi na kurudi Misri.” Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli waliokusanyika hapo. Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale walioenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao, wakasema na kusanyiko lote la Waisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita kati yake kuipeleleza ni nzuri sana. Ikiwa BWANA anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi inayotiririka maziwa na asali, naye atatupatia nchi hiyo. Ila tu msimwasi BWANA. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini BWANA yupo pamoja nasi. Msiwaogope.” Lakini kusanyiko lote wakazungumza kuhusu kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa BWANA ukaonekana katika Hema la Kukutania kwa Waisraeli wote.