Hesabu 13:1-33
Hesabu 13:1-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tuma watu waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani ambayo ninawapa wana wa Israeli. Utatuma mtu mmoja kutoka katika kila kabila, na mtu huyo lazima awe kiongozi katika kabila lake.” Basi, kwa mujibu wa agizo la Mwenyezi-Mungu, Mose akatuma watu kutoka jangwa la Parani. Watu wote waliotumwa walikuwa viongozi wa makabila mbalimbali ya wana wa Israeli. Ifuatayo ndiyo orodha ya majina ya watu hao: Kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri. Kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Kabila la Isakari, Igali mwana wa Yosefu. Kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni. Kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Kabila la Zebuluni, Gadieli mwana wa Sodi. Kabila la Yosefu (yaani kabila la Manase), Gadi mwana wa Susi. Kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali. Kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani. Mose alimpa Hoshea mwana wa Nuni jina jipya, akamwita Yoshua. Alipowatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, Mose aliwaambia: “Nendeni juu kule Negebu, hadi kwenye nchi ya milima, mkaipeleleze nchi ilivyo. Chunguzeni pia kama watu wanaoishi humo ni wenye nguvu au dhaifu, wengi au wachache. Pelelezeni kama nchi hiyo ni nzuri au mbaya, na kama miji wanamoishi ni kambi au ni nyumba zilizozungukwa na ngome. Chunguzeni pia kama nchi yenyewe ni tajiri au maskini, ina miti au haina. Muwe na mioyo ya ujasiri na mnaporudi chukueni baadhi ya matunda ya nchi hiyo.” Hayo yalikuwa majira ya zabibu zianzapo kuiva. Basi, watu hao wakaenda na kuipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, karibu na njia ya kuingilia Hamathi. Walikwenda hadi Negebu wakapita mpaka mji wa Hebroni. Humo waliwakuta Waahimani, Washeshai na Watalmai, wazawa wa Anaki. (Mji wa Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko nchini Misri). Walipofika katika Bonde la Eshkoli, watu hao walikata shada la mzabibu lililokuwa na matunda mengi nalo lilibebwa na watu wawili juu ya mti. Walichukua pia makomamanga kadhaa na tini. Mahali hapo paliitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya shada ambalo watu hao wa Israeli walikata kutoka mahali hapo. Baada ya kuipeleleza nchi kwa muda wa siku arubaini, watu hao walirudi. Waliwaendea Mose, Aroni na jumuiya ya Waisraeli huko Kadeshi, katika jangwa la Parani, wakatoa taarifa ya mambo waliyoyaona na kuwaonesha matunda ya nchi. Walimwambia Mose, “Tuliifikia nchi uliyotutuma tuipeleleze; hiyo ni nchi inayotiririka maziwa na asali, na hili ni tunda lake. Lakini wenyeji wake ni wenye nguvu sana, na miji yao ni imara na mikubwa sana. Zaidi ya hayo, huko tuliona wazawa wa Anaki. Waamaleki wanakaa katika eneo la Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanakaa katika eneo la milima, na Wakanaani wanakaa karibu na bahari ya Mediteranea na karibu na kingo za mto Yordani.” Lakini Kalebu aliwanyamazisha watu mbele ya Mose, akasema, “Twende mara moja tukaimiliki nchi hiyo. Kwa kuwa tunao uwezo sana wa kushinda.” Lakini watu walioandamana naye kuipeleleza nchi wakasema, “Hatutaweza kupigana na watu hao; wao wana nguvu kuliko sisi.” Kwa hiyo wakaeneza mambo ya uongo kati ya wana wa Israeli kuhusu nchi waliyoipeleleza, wakisema, “Nchi hiyo inawaua watu wake. Pia watu wote tuliowaona huko ni wakubwa sana. Tuliona majitu huko, wazawa wa Anaki. Sisi tulijiona kuwa kama panzi mbele yao, na ndivyo walivyotuona sisi.”
Hesabu 13:1-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila la baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na BWANA; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli. Na majina yao ni haya; katika kabila la Reubeni, Shamua mwana Zakuri. Katika kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Katika kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Katika kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu. Katika kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni Katika kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Katika kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi. Katika kabila la Yusufu, yaani, katika kabila la Manase, Gadi mwana wa Susi. Katika kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali. Katika kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Katika kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Katika kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. Musa akawatuma ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kama ni wenye nguvu au dhaifu, kama ni wengi au wachache; na nchi wanayoikaa kama ni nzuri au mbaya na kama wanakaa katika kambi au katika ngome; nayo nchi ni ya namna gani, kama ni nchi ya utajiri au ya umaskini; kama ina misitu au haina. Kuweni na mioyo ujasiri, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza. Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arubaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, kwa hakika, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, uthibitisho, haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni wenye nguvu, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara moja tukaimiliki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala wakazi wake; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu wakubwa mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.
Hesabu 13:1-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, akamwambia, Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na BWANA; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli. Na majina yao ni haya; katika kabila ya Reubeni, Shamua mwana Zakuri. Katika kabila ya Simeoni, Shafati mwana wa Hori. Katika kabila ya Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. Katika kabila ya Isakari, Igali mwana wa Yusufu. Katika kabila ya Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni Katika kabila ya Benyamini, Palti mwana wa Rafu. Katika kabila ya Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi. Katika kabila ya Yusufu, yaani, katika kabila ya Manase, Gadi mwana wa Susi. Katika kabila ya Dani, Amieli mwana wa Gemali. Katika kabila ya Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. Katika kabila ya Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. Katika kabila ya Gadi, Geueli mwana wa Maki. Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi; na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome; nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza. Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.
Hesabu 13:1-33 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa, “Watume baadhi ya watu wakaipeleleze nchi ya Kanaani, ninayowapa Waisraeli. Kutoka kwa kila kabila la baba zao, tuma mwanaume aliye mmoja wa viongozi wao.” Hivyo kwa agizo la BWANA Musa akawatuma kutoka Jangwa la Parani. Wote walikuwa viongozi wa Waisraeli. Haya ndiyo majina yao: kutoka kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri; kutoka kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori; kutoka kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune; kutoka kabila la Isakari, Igali mwana wa Yusufu; kutoka kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni; kutoka kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu; kutoka kabila la Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi, kutoka kabila la Manase (kabila la Yusufu), Gadi mwana wa Susi; kutoka kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali; kutoka kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli; kutoka kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi; kutoka kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki. Haya ndiyo majina ya watu ambao Musa aliwatuma kuipeleleza nchi. (Musa akampa Hoshea mwana wa Nuni jina Yoshua.) Musa alipowatuma wakaipeleleze Kanaani, alisema, “Pandeni kupitia Negebu, mwende hadi nchi ya vilima. Mwone nchi ni ya namna gani, na kama watu wanaoishi humo wana nguvu au ni wadhaifu, iwapo ni wachache au wengi. Wanaishi katika nchi ya namna gani? Je, ni nzuri au mbaya? Wanaishi katika miji ya namna gani? Je, haina kuta au ngome? Ardhi ikoje? Ina rutuba au la? Je, kuna miti ndani yake au la? Jitahidini kadiri mnavyoweza kuleta baadhi ya matunda ya nchi.” (Ulikuwa msimu wa kuiva zabibu za kwanza.) Hivyo wakapanda na kuipeleleza nchi kutoka Jangwa la Sini hadi Rehobu, kuelekea Lebo-Hamathi. Wakapanda kupitia Negebu hadi wakafika Hebroni, mahali ambapo Ahimani, Sheshai na Talmai, wazao wa Anaki, waliishi. (Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko Misri.) Walipofika katika Bonde la Eshkoli, walikata tawi lililokuwa na kishada kimoja cha zabibu. Wawili wao wakalichukua lile tawi kwenye mti, pamoja na komamanga na tini. Eneo lile likaitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya kile kishada cha zabibu ambacho Waisraeli walikikata huko. Baada ya siku arobaini, wakarudi kutoka kuipeleleza nchi. Wakarudi kwa Musa, Haruni na jumuiya yote ya Waisraeli huko Kadeshi kwenye Jangwa la Parani. Hapo ndipo walipotoa habari kwao na kwa kusanyiko lote na kuwaonesha matunda ya hiyo nchi. Wakampa Musa taarifa hii: “Tuliingia katika nchi uliyotutuma, nayo inatiririka maziwa na asali! Hili hapa tunda lake. Lakini watu wanaoishi huko ni wenye nguvu, na miji yao ina ngome na ni mikubwa sana. Huko tuliona hata wazao wa Anaki. Waamaleki wanaishi Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanaishi katika nchi ya vilima; nao Wakanaani wanaishi karibu na bahari na kando ya Yordani.” Kisha Kalebu akawanyamazisha watu mbele ya Musa na kusema, “Imetupasa kupanda na kuimiliki nchi, kwa maana hakika tunaweza kufanya hivyo.” Lakini watu waliokuwa wamepanda pamoja naye wakasema, “Hatuwezi kuwashambulia wale watu; wana nguvu kuliko sisi.” Wakaeneza taarifa mbaya miongoni mwa Waisraeli kuhusu nchi waliyoipeleleza. Wakasema, “Nchi tuliyoipeleleza hula watu wanaoishi ndani yake. Watu wote tuliowaona huko ni majitu. Tuliwaona Wanefili huko (wazao wa Anaki wanatokana na Wanefili). Tulijiona kama panzi machoni petu wenyewe, nao ndivyo walivyotuona.”