Hesabu 11:24-30
Hesabu 11:24-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mose akaenda na kuwajulisha watu yale aliyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha, akakusanya wazee sabini kutoka miongoni mwa wazee viongozi nao akawaweka kandokando kuizunguka hema. Hapo, Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu na kuzungumza naye. Halafu akatwaa sehemu ya roho aliyokuwa amempa Mose, akawapa kila mmoja wa wale wazee sabini. Walipoingiwa na roho hiyo, wazee hao walianza kutoa unabii, lakini hawakurudia kufanya hivyo. Wazee wawili kati ya wale sabini waliochaguliwa, Eldadi na Medadi, walikuwa wamebaki kambini wenzao walipokwenda kwenye hema. Roho iliwajia humohumo kambini, wakaanza kutoa unabii mahali walipokuwa. Kijana mmoja alitoka mbio na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.” Hapo, Yoshua, mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akamwambia Mose, “Bwana wangu, wakataze!” Lakini Mose akamjibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Laiti Mwenyezi-Mungu angewapa watu wake wote roho yake nao wakawa manabii!” Kisha Mose alirudi kambini pamoja na wale wazee sabini wa Israeli.
Hesabu 11:24-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya BWANA; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema. Ndipo BWANA akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake. Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli.
Hesabu 11:24-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Hesabu 11:24-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo Musa akatoka na kuwaambia watu lile ambalo BWANA alikuwa amesema. Akawakusanya wazee wao sabini, akawasimamisha kuzunguka Hema. Kisha BWANA akashuka katika wingu na kunena na Musa, naye akachukua sehemu ya Roho iliyokuwa juu ya Musa na kuiweka juu ya wale wazee sabini. Roho aliposhuka juu yao, wakatoa unabii, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili, ambao majina yao ni Eldadi na Medadi, walibaki kambini. Walikuwa wameorodheshwa miongoni mwa wale wazee sabini, lakini hawakutoka kwenda kwenye Hema. Lakini Roho pia alishuka juu yao, nao wakatabiri huko kambini. Mwanaume mmoja kijana alikimbia na kumwambia Musa, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.” Yoshua mwana wa Nuni, aliyekuwa msaidizi wa Musa tangu ujana wake, akajibu, akasema, “Musa bwana wangu, wanyamazishe!” Lakini Musa akajibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Ningetamani watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kwamba BWANA angeweka Roho yake juu yao!” Ndipo Musa na wale wazee wa Israeli wakarudi kambini.