Hesabu 11:11-15
Hesabu 11:11-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Mose alipomwambia, Mwenyezi-Mungu “Kwa nini unanitendea vibaya mimi mtumishi wako? Mbona hupendezwi nami, kwa nini umenitwika mzigo wa kuwatunza watu wote hawa? Je, ni mimi niliyewazaa, hata ukaniambia niwabebe kifuani pangu kama mlezi abebavyo mtoto mchanga, na kuwapeleka mpaka nchi uliyoapa kuwapa babu zao? Nitapata wapi nyama ya kuwalisha watu hawa wote? Maana wanalia mbele yangu wakisema: ‘Tupe nyama tule!’ Siwezi kuwatunza watu wote hawa peke yangu; hilo ni jukumu kubwa mno kwangu! Ikiwa hivi ndivyo utakavyonitenda, afadhali uniue mara moja! Kama ninapata kibali mbele yako, usiniache niikabili taabu yangu.”
Hesabu 11:11-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Musa akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwa nini wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwawaongoza watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, ikiwa nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.
Hesabu 11:11-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Musa akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.
Hesabu 11:11-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Akamuuliza BWANA, “Kwa nini umeleta taabu hii juu ya mtumishi wako? Nimekufanyia nini cha kukuchukiza hata ukaweka mzigo huu wa watu hawa wote juu yangu? Je, watu hawa wote mimi ndiye niliyewatungisha mimba? Je, ni mimi niliyewazaa? Kwa nini unaniambia niwachukue mikononi mwangu, kama vile mlezi abebavyo mtoto mchanga, hadi kwenye nchi uliyowaahidi baba zao? Nitapata wapi nyama kwa ajili ya watu wote hawa? Wanaendelea kunililia wakisema, ‘Tupe nyama tule!’ Mimi siwezi kuwabeba watu hawa wote peke yangu, mzigo ni mzito sana kwangu. Kama hivi ndivyo unavyonitendea, uniue sasa hivi, yaani kama nimepata kibali machoni pako, wala usiniache nione maangamizi yangu mwenyewe.”