Hesabu 11:1-9
Hesabu 11:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu walianza kumlalamikia Mwenyezi-Mungu juu ya taabu zao. Mwenyezi-Mungu aliposikia, alishikwa na hasira, akawapelekea moto. Moto huo uliwaka kati yao na kuchoma upande mmoja wa kambi. Watu wakamlilia Mose, naye akamwomba Mwenyezi-Mungu na moto huo ukazimika. Kwa hiyo, mahali hapo pakaitwa Tabera, kwa sababu hapo moto wa Mwenyezi-Mungu uliwaka kati ya watu. Miongoni mwa Waisraeli kulikuwa na kundi fulani lililoandamana nao ambalo lilikuwa na hamu kubwa. Waisraeli kwa mara nyingine walilia, wakisema. “Laiti kama tungeweza kupata nyama ya kula! Tunakumbuka, samaki tuliokula kule Misri bila malipo, matango, matikiti, mboga, vitunguu na vitunguu saumu! Lakini sasa nguvu zimetuishia na hakuna chakula kingine isipokuwa hii mana tu!” Mana ilikuwa kama punje za mtama, rangi yake ilikuwa kama ya bedoza. Watu walizungukazunguka na kuikusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia au waliitwanga kwa vinu, halafu waliitokosa vyunguni na kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama ya maandazi yaliyokaangwa kwa mafuta. (Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, mana pia ilianguka pamoja na huo umande).
Hesabu 11:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza hadi viunga vya kambi. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao. Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, Ni nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hakuna kitu chochote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na rangi yake ilikuwa kama ya Bedola. Watu wakazungukazunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa vyunguni na kuandaa mikate; na ladha yake ilikuwa kama ladha ya mafuta mapya. Umande ulipoiangukia kambi wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.
Hesabu 11:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao. Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.
Hesabu 11:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi watu wakalalamika kwa habari ya taabu zao masikioni mwa BWANA, naye alipowasikia, hasira yake ikawaka. Ndipo moto kutoka kwa BWANA ukawaka miongoni mwao na kuteketeza baadhi ya viunga vya kambi. Watu walipomlilia Musa, akamwomba BWANA, nao moto ukazimika. Hivyo mahali pale pakaitwa Tabera, kwa sababu moto kutoka kwa BWANA uliwaka miongoni mwao. BWANA Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu. Lakini sasa tumepoteza hamu ya chakula; hatuoni kitu kingine chochote isipokuwa hii mana!” Mana ilifanana kama mbegu za giligilani, nayo ilikuwa na rangi ya manjano iliyopauka. Hao watu walienda kukusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia ya mkono au kuitwanga kwenye vinu. Waliipika vyunguni au kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama kitu kilichotengenezwa kwa mafuta ya zeituni. Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, pia mana ilianguka pamoja nao.