Hesabu 11:1-35
Hesabu 11:1-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu walianza kumlalamikia Mwenyezi-Mungu juu ya taabu zao. Mwenyezi-Mungu aliposikia, alishikwa na hasira, akawapelekea moto. Moto huo uliwaka kati yao na kuchoma upande mmoja wa kambi. Watu wakamlilia Mose, naye akamwomba Mwenyezi-Mungu na moto huo ukazimika. Kwa hiyo, mahali hapo pakaitwa Tabera, kwa sababu hapo moto wa Mwenyezi-Mungu uliwaka kati ya watu. Miongoni mwa Waisraeli kulikuwa na kundi fulani lililoandamana nao ambalo lilikuwa na hamu kubwa. Waisraeli kwa mara nyingine walilia, wakisema. “Laiti kama tungeweza kupata nyama ya kula! Tunakumbuka, samaki tuliokula kule Misri bila malipo, matango, matikiti, mboga, vitunguu na vitunguu saumu! Lakini sasa nguvu zimetuishia na hakuna chakula kingine isipokuwa hii mana tu!” Mana ilikuwa kama punje za mtama, rangi yake ilikuwa kama ya bedoza. Watu walizungukazunguka na kuikusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia au waliitwanga kwa vinu, halafu waliitokosa vyunguni na kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama ya maandazi yaliyokaangwa kwa mafuta. (Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, mana pia ilianguka pamoja na huo umande). Mose alisikia watu wakilia katika familia zote, kila mtu penye lango la hema lake. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka sana; naye Mose alichukizwa. Ndipo Mose alipomwambia, Mwenyezi-Mungu “Kwa nini unanitendea vibaya mimi mtumishi wako? Mbona hupendezwi nami, kwa nini umenitwika mzigo wa kuwatunza watu wote hawa? Je, ni mimi niliyewazaa, hata ukaniambia niwabebe kifuani pangu kama mlezi abebavyo mtoto mchanga, na kuwapeleka mpaka nchi uliyoapa kuwapa babu zao? Nitapata wapi nyama ya kuwalisha watu hawa wote? Maana wanalia mbele yangu wakisema: ‘Tupe nyama tule!’ Siwezi kuwatunza watu wote hawa peke yangu; hilo ni jukumu kubwa mno kwangu! Ikiwa hivi ndivyo utakavyonitenda, afadhali uniue mara moja! Kama ninapata kibali mbele yako, usiniache niikabili taabu yangu.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wakusanyeni wazee sabini wa Israeli, ambao wewe unajua wanaheshimiwa na kukubaliwa na watu kuwa viongozi, uwalete kwenye hema la mkutano, wasimame karibu nawe. Nitashuka huko na kuzungumza nawe; nitachukua sehemu ya roho niliyokupa, niwape watu hao. Nao watabeba jukumu la kuwatunza watu hawa pamoja nawe, usije ukaubeba mzigo huo peke yako. Sasa waambie watu hivi: Jitakaseni kwa ajili ya kesho; mtakula nyama. Mwenyezi-Mungu amesikia mkilia na kusema kuwa hakuna wa kuwapeni nyama, na kwamba hali yenu ilikuwa nzuri zaidi mlipokuwa Misri. Sasa Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama, nanyi sharti muile. Mtakula nyama si kwa muda wa siku moja tu, au mbili, au tano, au kumi au ishirini, bali kwa muda wa mwezi mzima! Mtaila hadi iwatoke puani, mpaka muikinai. Yote hayo ni kwa sababu mmemkataa Mwenyezi-Mungu aliye hapahapa miongoni mwenu, na kulia mbele yake mkisema, ‘Kwa nini tulitoka Misri?’” Lakini Mose alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Idadi ya watu ninaowaongoza hapa ni 600,000 waendao kwa miguu, nawe wasema, ‘Nitawapa nyama ya kuwatosha mwezi mzima!’ Je, panaweza kuchinjwa kondoo na ng'ombe wa kuwatosheleza? Je, samaki wote baharini wavuliwe kwa ajili yao?” Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Je, uwezo wangu umepungua? Utaona basi kama neno langu litakuwa la kweli kwako au la.” Basi, Mose akaenda na kuwajulisha watu yale aliyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha, akakusanya wazee sabini kutoka miongoni mwa wazee viongozi nao akawaweka kandokando kuizunguka hema. Hapo, Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu na kuzungumza naye. Halafu akatwaa sehemu ya roho aliyokuwa amempa Mose, akawapa kila mmoja wa wale wazee sabini. Walipoingiwa na roho hiyo, wazee hao walianza kutoa unabii, lakini hawakurudia kufanya hivyo. Wazee wawili kati ya wale sabini waliochaguliwa, Eldadi na Medadi, walikuwa wamebaki kambini wenzao walipokwenda kwenye hema. Roho iliwajia humohumo kambini, wakaanza kutoa unabii mahali walipokuwa. Kijana mmoja alitoka mbio na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.” Hapo, Yoshua, mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akamwambia Mose, “Bwana wangu, wakataze!” Lakini Mose akamjibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Laiti Mwenyezi-Mungu angewapa watu wake wote roho yake nao wakawa manabii!” Kisha Mose alirudi kambini pamoja na wale wazee sabini wa Israeli. Baadaye Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo kwa ghafla, ukaleta kware kutoka baharini na kuwafanya watue kando ya kambi, mwendo wa siku moja hivi kila upande kuizunguka kambi, wakarundikana chini karibu kimo cha mita moja hivi. Basi, siku hiyo yote, kutwa kucha, na siku iliyofuata watu walishughulika kukusanya kware; hakuna mtu aliyekusanya chini ya kilo 1,000. Wakawaanika kila mahali kandokando ya kambi ili wawakaushe. Kulipokuwa bado kuna nyama kwa wingi na kabla watu hawajawamaliza kuila, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia watu, akawapiga watu kwa pigo kubwa sana. Kwa hiyo mahali hapo palipewa jina Kibroth-hataava; kwa sababu huko ndiko walikowazika watu waliokuwa walafi. Kutoka hapo Kibroth-hataava watu walisafiri mpaka Haserothi, wakapiga kambi yao na kukaa huko.
Hesabu 11:1-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza hadi viunga vya kambi. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao. Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, Ni nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hakuna kitu chochote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na rangi yake ilikuwa kama ya Bedola. Watu wakazungukazunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa vyunguni na kuandaa mikate; na ladha yake ilikuwa kama ladha ya mafuta mapya. Umande ulipoiangukia kambi wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za BWANA zikawaka sana; Musa naye akakasirika. Musa akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwa nini wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwawaongoza watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, ikiwa nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu. Kisha BWANA akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa Israeli, ambao wewe unawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na viongozi juu yao; ukawalete katika hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako. Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa BWANA, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo BWANA atawapa nyama, nanyi mtakula. Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini; lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hadi hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa BWANA aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani? Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu elfu mia sita waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima. Je! Makundi ya kondoo na ng'ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha? BWANA akamwambia Musa, Je! Mkono wa BWANA umepungua urefu wake? Sasa utaona kama neno langu litatimizwa kwako, au la. Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya BWANA; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema. Ndipo BWANA akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake. Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli. Kisha upepo ukavuma kutoka kwa BWANA, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande ule, kuizunguka, nao wakafikia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi. Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kandokando ya kambi kuizunguka pande zote. Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za BWANA ziliwaka juu ya watu, BWANA akawapiga watu kwa pigo kuu mno. Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani. Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi.
Hesabu 11:1-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao. Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za BWANA zikawaka sana; Musa naye akakasirika. Musa akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu. Kisha BWANA akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako. Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa BWANA, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo BWANA atawapa nyama, nanyi mtakula. Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini; lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa BWANA aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani? Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima. Je! Makundi ya kondoo na ng’ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha? BWANA akamwambia Musa, Je! Mkono wa BWANA umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo. Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya BWANA; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema. Ndipo BWANA akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini. Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake. Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli. Kisha upepo ukavuma kutoka kwa BWANA, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi. Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote. Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za BWANA ziliwaka juu ya watu, BWANA akawapiga watu kwa pigo kuu mno. Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani. Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi.
Hesabu 11:1-35 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi watu wakalalamika kwa habari ya taabu zao masikioni mwa BWANA, naye alipowasikia, hasira yake ikawaka. Ndipo moto kutoka kwa BWANA ukawaka miongoni mwao na kuteketeza baadhi ya viunga vya kambi. Watu walipomlilia Musa, akamwomba BWANA, nao moto ukazimika. Hivyo mahali pale pakaitwa Tabera, kwa sababu moto kutoka kwa BWANA uliwaka miongoni mwao. BWANA Umati wa watu wenye zogo waliokuwa miongoni mwao walitamani sana chakula kingine, Waisraeli wakaanza kulia tena na kusema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tunakumbuka wale samaki tuliokula huko Misri bila gharama, pia yale matango, matikitimaji, mboga, vitunguu, na vitunguu saumu. Lakini sasa tumepoteza hamu ya chakula; hatuoni kitu kingine chochote isipokuwa hii mana!” Mana ilifanana kama mbegu za giligilani, nayo ilikuwa na rangi ya manjano iliyopauka. Hao watu walienda kukusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia ya mkono au kuitwanga kwenye vinu. Waliipika vyunguni au kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama kitu kilichotengenezwa kwa mafuta ya zeituni. Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, pia mana ilianguka pamoja nao. Musa akasikia watu wa kila jamaa wakilia, kila mmoja kwenye mlango wa hema lake. BWANA akakasirika mno, naye Musa akafadhaika. Akamuuliza BWANA, “Kwa nini umeleta taabu hii juu ya mtumishi wako? Nimekufanyia nini cha kukuchukiza hata ukaweka mzigo huu wa watu hawa wote juu yangu? Je, watu hawa wote mimi ndiye niliyewatungisha mimba? Je, ni mimi niliyewazaa? Kwa nini unaniambia niwachukue mikononi mwangu, kama vile mlezi abebavyo mtoto mchanga, hadi kwenye nchi uliyowaahidi baba zao? Nitapata wapi nyama kwa ajili ya watu wote hawa? Wanaendelea kunililia wakisema, ‘Tupe nyama tule!’ Mimi siwezi kuwabeba watu hawa wote peke yangu, mzigo ni mzito sana kwangu. Kama hivi ndivyo unavyonitendea, uniue sasa hivi, yaani kama nimepata kibali machoni pako, wala usiniache nione maangamizi yangu mwenyewe.” BWANA akamwambia Musa: “Niletee wazee sabini wa Israeli, unaowafahamu kama viongozi na maafisa miongoni mwa watu. Walete katika Hema la Kukutania, ili waweze kusimama huko pamoja nawe. Nami nitashuka na kusema nawe huko. Nami nitachukua sehemu ya Roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao. Watakusaidia kubeba mzigo wa watu hao ili usije ukaubeba peke yako. “Waambie hao watu: ‘Jiwekeni wakfu wenyewe kwa ajili ya kesho, wakati mtakapokula nyama. BWANA aliwasikia mlipolia, mkisema, “Laiti tungekuwa na nyama tule! Tulikuwa na hali nzuri zaidi katika nchi ya Misri!” Sasa BWANA atawapa nyama, nanyi mtaila. Hamtaila kwa siku moja tu, au siku mbili, au tano, kumi au siku ishirini, bali kwa mwezi mzima hadi iwatokee puani, nanyi mtaichukia kabisa, kwa kuwa mmemkataa BWANA, ambaye yupo miongoni mwenu, nanyi mmelia mbele zake, mkisema, “Hivi kwa nini tulitoka Misri?” ’ ” Lakini Musa alisema, “Mimi niko hapa miongoni mwa watu elfu mia sita wanaotembea kwa miguu, nawe umesema, ‘Nitawapa nyama ya kula kwa mwezi mzima!’ Je, wangeweza kupata nyama ya kuwatosha hata kama makundi ya kondoo na ya ngʼombe yangechinjwa kwa ajili yao? Je, wangetosheka hata kama samaki wote wa baharini wangevuliwa kwa ajili yao?” BWANA akamjibu Musa, “Je, mkono wa BWANA ni mfupi sana? Sasa utaona kama jambo nililolisema litatimizwa kwa ajili yako au la.” Kwa hiyo Musa akatoka na kuwaambia watu lile ambalo BWANA alikuwa amesema. Akawakusanya wazee wao sabini, akawasimamisha kuzunguka Hema. Kisha BWANA akashuka katika wingu na kunena na Musa, naye akachukua sehemu ya Roho iliyokuwa juu ya Musa na kuiweka juu ya wale wazee sabini. Roho aliposhuka juu yao, wakatoa unabii, lakini hawakufanya hivyo tena. Lakini watu wawili, ambao majina yao ni Eldadi na Medadi, walibaki kambini. Walikuwa wameorodheshwa miongoni mwa wale wazee sabini, lakini hawakutoka kwenda kwenye Hema. Lakini Roho pia alishuka juu yao, nao wakatabiri huko kambini. Mwanaume mmoja kijana alikimbia na kumwambia Musa, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.” Yoshua mwana wa Nuni, aliyekuwa msaidizi wa Musa tangu ujana wake, akajibu, akasema, “Musa bwana wangu, wanyamazishe!” Lakini Musa akajibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Ningetamani watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kwamba BWANA angeweka Roho yake juu yao!” Ndipo Musa na wale wazee wa Israeli wakarudi kambini. Kisha ukatokea upepo kutoka kwa BWANA, nao ukawaletea kware kutoka baharini. Ukawaangusha kwenye eneo lote linalozunguka kambi na kujaa ardhini kimo cha mita moja hivi kutoka ardhini kwenye eneo la umbali wa mwendo wa siku moja kila upande. Mchana kutwa na usiku kucha pamoja na siku nzima iliyofuata watu walitoka kwenda kuokota kware. Hakuna mtu yeyote aliyekusanya chini ya homeri kumi. Kisha wakazianika kuzunguka kambi yote. Lakini walipokuwa wakila nyama, ilipokuwa ingali kati ya meno yao na kabla hawajamaliza kula, hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya watu, naye akawapiga kwa tauni. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Kibroth-Hataava, kwa sababu huko ndiko walipowazika watu ambao walitamani sana chakula kingine. Kutoka Kibroth-Hataava watu wakasafiri hadi Haserothi na kukaa huko.