Nehemia 7:1-4
Nehemia 7:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya ukuta kukamilika, malango yote kuwa tayari, na kuteuliwa kwa walinzi, waimbaji na Walawi, nilimteua ndugu yangu Hanani kuwa mwangalizi wa Yerusalemu akishirikiana na Hanania aliyekuwa mkuu wa ngome katika Yerusalemu; kwa sababu alikuwa mtu wa kutegemewa na anayemcha sana Mungu, hapakuwapo mwingine aliyelingana naye, nikawaagiza, “Malango yasifunguliwe usiku kucha hadi jua linapokuwa limepanda. Kabla hawajaondoka walinzi ni lazima kufunga milango yote kwa makomeo yake. Teueni walinzi miongoni mwa wakazi wa mji wa Yerusalemu, kila mmoja awe mahali pake kukabiliana na nyumba yake.” Mji wa Yerusalemu ulikuwa mpana na mkubwa, lakini wakazi wake walikuwa wachache na nyumba zilikuwa hazijajengwa.
Nehemia 7:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, baada ya ukuta kujengwa, na milango kuisimamishwa na kuweka mabawabu, waimbaji na Walawi, ndipo nilimteua ndugu yangu Hanani, kuwa mwangalizi wa Yerusalemu akisaidiana na Hanania, jemadari wa ngome, kwa maana alikuwa mtu mwaminifu na mwenye kumcha Mungu kuliko wengi. Nikawaambia, Yasifunguliwe malango ya Yerusalemu kabla jua halijachomoza; na kabla walinzi hawajaondoka waifunge milango, mkaikaze; kisha wekeni walinzi wa zamu wa hao wakaao Yerusalemu, kila mtu na zamu yake, na kila mtu kuielekea nyumba yake. Basi mji ulikuwa wa nafasi nyingi, tena mkubwa; lakini watu waliomo walikuwa wachache, na nyumba zilikuwa hazijajengwa.
Nehemia 7:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, hapo ukuta ulipojengwa, na milango nimekwisha kuisimamisha, na mabawabu, na waimbaji, na Walawi, wamewekwa, ndipo nilimwagiza ndugu yangu, Hanani, pamoja na yule Hanania, jemadari wa ngome, kuwa na amri juu ya Yerusalemu; kwa maana alikuwa mtu mwaminifu huyo, na mwenye kumcha Mungu kuliko wengi. Nikawaambia, Yasifunguliwe malango ya Yerusalemu kabla halijachomoza jua; nao walinzi wangali wakisimama bado, waifunge milango, mkaikaze; kisha wekeni walinzi wa zamu wa hao wakaao Yerusalemu, kila mtu na zamu yake, na kila mtu kuielekea nyumba yake. Basi mji ulikuwa wa nafasi nyingi, tena mkubwa; lakini watu waliomo walikuwa haba, wala nyumba hazijajengwa.
Nehemia 7:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya ukuta kukamilika kujengwa upya na nikaweka milango, mabawabu wa lango, waimbaji, na Walawi waliteuliwa. Nikamweka Hanani ndugu yangu kuwa kiongozi wa Yerusalemu, pamoja na Hanania jemadari wa ngome, kwa kuwa alikuwa mtu mwadilifu na mwenye kumcha Mungu kuliko watu wengine. Nikawaambia, “Malango ya Yerusalemu yasifunguliwe hadi jua litakapokuwa limepanda. Walinzi wa malango wakiwa bado kwenye zamu, waamuru wafunge milango na waweke makomeo. Pia wateueni wenyeji wa Yerusalemu wawe walinzi, kila mmoja kwenye lindo lake, na wengine karibu na nyumba zao wenyewe.” Mji ulikuwa mkubwa, tena wenye nafasi nyingi, lakini walikuwepo watu wachache ndani yake, nazo nyumba zilikuwa bado ni magofu.