Nehemia 6:5-9
Nehemia 6:5-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Mara ya tano, Sanbalati akanitumia barua ya hadhara kwa njia ya mjumbe wake. Na barua yenyewe iliandikwa ifuatavyo: “Kuna habari zilizoenezwa miongoni mwa mataifa jirani, na Geshemu anathibitisha habari hizi, kuwa wewe pamoja na Wayahudi wenzako mnakusudia kuasi. Hii ndiyo sababu mnaujenga upya ukuta. Kulingana na habari hizo, wewe unakusudia kuwa mfalme wao. Ili kuthibitisha wazo lako, umejiwekea manabii mjini Yerusalemu ili watangaze kuwa ‘Kuna mfalme katika nchi ya Yuda’. Taarifa hii ataarifiwa mfalme Artashasta. Hivyo nashauri wewe na mimi tukutane na kuzungumzia jambo hili.” Nami nikampelekea ujumbe: “Hakuna jambo kama hilo. Habari hizo umezibuni wewe mwenyewe.” Walifanya hivyo ili kututisha wakifikiri: “Hawataendelea na kazi, kwa hiyo, hakuna litakalotendeka.” Nikamwomba Mungu wangu nikisema, “Lakini sasa, ee Mungu, nakuomba unipe nguvu.”
Nehemia 6:5-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumishi wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake; nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mnakusudia kuasi; ndiyo sababu unaujenga huo ukuta; nawe unataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo. Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu kwa kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa mfalme ataarifiwa mambo haya, Basi sasa, njoo ili tushauriane. Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni. Kwani hao wote walitaka kutuogofya, wakisema, Kwa kuwa mikono yao italegea katika kazi, kazi isifanyike. Lakini sasa Ee Mungu, itie nguvu mikono yangu.
Nehemia 6:5-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake; nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo. Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja. Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni. Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.
Nehemia 6:5-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe ule ule, naye alikuwa amechukua mkononi mwake barua isiyofungwa, iliyokuwa imeandikwa: “Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa, naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnapanga njama ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kufuatana na taarifa hizi, karibuni utakuwa mfalme wao, na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme. Basi njoo, tufanye shauri pamoja.” Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika. Unalitunga tu kwenye kichwa chako.” Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri hivi: “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.” Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”