Nehemia 6:1-9
Nehemia 6:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Sanbalati, Tobia, Geshemu, Mwarabu na adui zetu wengine, waliposikia kuwa tumemaliza ujenzi wa ukuta na kwamba hakuna mapengo yoyote (ingawa tulikuwa bado hatujaweka milango ya malango), Sanbalati na Geshemu walituma ujumbe kwangu wakisema, “Na tukutane kwenye kijiji kimojawapo cha tambarare ya Ono.” Lakini walikusudia kunidhuru. Basi, nikawapelekea wajumbe, nikisema, “Kazi ninayoifanya ni muhimu sana. Hivyo siwezi kuja kwenu ili kazi isije ikasimama.” Waliendelea kunitaka niende kwao mara nne, lakini nikawapa jibu lilelile. Mara ya tano, Sanbalati akanitumia barua ya hadhara kwa njia ya mjumbe wake. Na barua yenyewe iliandikwa ifuatavyo: “Kuna habari zilizoenezwa miongoni mwa mataifa jirani, na Geshemu anathibitisha habari hizi, kuwa wewe pamoja na Wayahudi wenzako mnakusudia kuasi. Hii ndiyo sababu mnaujenga upya ukuta. Kulingana na habari hizo, wewe unakusudia kuwa mfalme wao. Ili kuthibitisha wazo lako, umejiwekea manabii mjini Yerusalemu ili watangaze kuwa ‘Kuna mfalme katika nchi ya Yuda’. Taarifa hii ataarifiwa mfalme Artashasta. Hivyo nashauri wewe na mimi tukutane na kuzungumzia jambo hili.” Nami nikampelekea ujumbe: “Hakuna jambo kama hilo. Habari hizo umezibuni wewe mwenyewe.” Walifanya hivyo ili kututisha wakifikiri: “Hawataendelea na kazi, kwa hiyo, hakuna litakalotendeka.” Nikamwomba Mungu wangu nikisema, “Lakini sasa, ee Mungu, nakuomba unipe nguvu.”
Nehemia 6:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakubakia mapengo ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango); Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Lakini wakakusudia kunifanyia mabaya. Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, siwezi kushuka, kwa nini niwashukie na hapo kazi isimame? Nao wakaniletea mwito huo mara nne; nikawajibu maneno yale yale. Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumishi wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake; nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mnakusudia kuasi; ndiyo sababu unaujenga huo ukuta; nawe unataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo. Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu kwa kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa mfalme ataarifiwa mambo haya, Basi sasa, njoo ili tushauriane. Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni. Kwani hao wote walitaka kutuogofya, wakisema, Kwa kuwa mikono yao italegea katika kazi, kazi isifanyike. Lakini sasa Ee Mungu, itie nguvu mikono yangu.
Nehemia 6:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango); Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya. Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie? Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale. Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake; nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo. Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja. Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni. Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.
Nehemia 6:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Habari zilipofika kwa Sanbalati, Tobia, Geshemu Mwarabu, na adui zetu wengine kwamba nimejenga tena ukuta na hakuna nafasi iliyobakia ndani yake, ingawa hata wakati huo sikuwa nimeweka milango kwenye malango, Sanbalati na Geshemu wakanitumia ujumbe huu: “Njoo, tukutane katika mojawapo ya vijiji katika nchi tambarare ya Ono.” Lakini walikuwa wakikusudia kunidhuru. Kwa hiyo niliwatuma wajumbe kwao na majibu haya: “Kazi ninayoifanya ni kubwa sana, siwezi kuja. Kwa nini niiache kazi isimame nije kwenu?” Walinitumia ujumbe huo huo mara nne, na kila mara nikawapa jibu lile lile. Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe ule ule, naye alikuwa amechukua mkononi mwake barua isiyofungwa, iliyokuwa imeandikwa: “Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa, naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnapanga njama ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kufuatana na taarifa hizi, karibuni utakuwa mfalme wao, na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme. Basi njoo, tufanye shauri pamoja.” Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika. Unalitunga tu kwenye kichwa chako.” Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri hivi: “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.” Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”