Nehemia 2:1-20
Nehemia 2:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Katika mwezi wa Nisani, katika mwaka wa ishirini wa utawala wa mfalme Artashasta, wakati divai ilipokuwa mbele yake, nilichukua divai na kumpelekea mkononi mwake. Kamwe sikuwahi kuwa mwenye huzuni mbele yake. Mfalme Artashasta akaniuliza, “Je, mbona unaonekana kuwa mwenye huzuni, ingawa huonekani kuwa mgonjwa? Naona una huzuni sana moyoni mwako!” Ndipo nilipoogopa sana. Nikamjibu, “Ee mfalme, udumu milele! Kwa nini nisiwe mwenye huzuni wakati mji wa Yerusalemu yalimo makaburi ya babu zangu uko tupu na malango yake yameteketezwa kwa moto?” Ndipo mfalme Artashasta akanijibu, “Sasa unaomba nini?” Nikamwomba Mungu wa mbinguni. Halafu nikamwambia mfalme, “Ee mfalme, ikiwa unapendezwa nami na ikiwa nimepata upendeleo mbele yako, nakuomba unitume Yuda ili niende kuujenga upya mji ambamo yamo makaburi ya babu zangu.” Mfalme akaniuliza (malkia akiwa karibu naye), “Utakuwa huko kwa muda gani na utarudi lini hapa?” Ombi langu akalikubali nami nikamjulisha wakati nitakaporudi. Nikamjibu, “Ee mfalme ikiwa unapendezwa nami, naomba nipewe barua ili nizipeleke kwa watawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate ili waniruhusu nipite hadi nchini Yuda. Pia nakuomba barua iandikwe kwa Asafu mtunzaji wa msitu wa kifalme ili anipatie mbao za kutengenezea miimo ya malango ya ngome ya hekalu, ukuta wa mji na nyumba yangu nitakamokaa.” Mfalme akakubali ombi langu kwa kuwa Mungu, kwa wema wake, alikuwa pamoja nami. Nilipowafikia wakuu wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, niliwapa barua za mfalme. Mfalme alikuwa amenituma pamoja na maofisa wa jeshi na wapandafarasi. Lakini Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, Mwamoni, mtumishi wake, waliposikia kuwa nimekuja ili kushughulikia hali njema ya watu wa Israeli, hawakufurahia kabisa jambo hilo. Hivyo nikafika Yerusalemu, nikakaa huko kwa siku tatu. Kisha niliondoka usiku, mimi pamoja na watu wachache; sikumwambia mtu yeyote yale ambayo Mungu alikuwa ameyaweka moyoni mwangu kwa ajili ya mji wa Yerusalemu. Lakini siku moja usiku, niliondoka na kuwachukua watu wachache tu. Sikuchukua mnyama yeyote isipokuwa punda niliyempanda mimi mwenyewe. Nikatoka nikipitia Lango la Bondeni katika njia ielekeayo kwenye Kisima cha Joka na Lango la Mavi; nikazikagua kuta za mji wa Yerusalemu ambazo zilikuwa zimebomolewa pamoja na malango yake ambayo yalikuwa yameteketezwa kwa moto. Halafu, nikaenda kwenye Lango la Chemchemi na kwenye Bwawa la Mfalme. Lakini yule punda niliyempanda hakuweza kupita. Wakati huo wa usiku, nikapitia bondeni na kukagua ukuta wa mji. Nilirudi nikapitia Lango la Bondeni. Maofisa hawakujua mahali nilipokuwa nimekwenda wala nimefanya nini. Tena nilikuwa sijawaambia Wayahudi, makuhani, viongozi, wakuu wala wale watu ambao wangeifanya kazi ya kuujenga upya mji. Kisha nikawaambia, “Bila shaka mnaliona tatizo letu kuwa mji wa Yerusalemu ni magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Basi, na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu ili tusiaibishwe zaidi.” Nikawaeleza jinsi Mungu alivyokuwa pamoja nami akinitendea kwa wema wake. Nikawaeleza pia maneno ambayo mfalme alikuwa ameniambia. Wao walipoyasikia hayo, wakasema, “Haya, na tuanze kazi ya ujenzi.” Hivyo wakajiandaa kwa kazi hiyo njema. Lakini Sanbalati, Mhoroni, Tobia, Mwamoni mtumishi wake, na Geshemu, Mwarabu, waliposikia, wakatucheka na kutuzomea wakisema, “Ni kitu gani hiki mnachotenda? Je, mnataka kumwasi mfalme?” Nikawajibu, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha katika kazi hii, nasi tulio watumishi wake tutaanza ujenzi. Lakini nyinyi hamna fungu wala haki wala kumbukumbu katika mji wa Yerusalemu.”
Nehemia 2:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wowote. Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana. Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto? Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni. Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unitume mpaka Yuda, niende katika mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga. Mfalme akaniuliza, (malkia akiwa ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunituma; nami nikampa muda. Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa watawala walio ng'ambo ya Mto, ili wanikubalie kupita hadi nifike Yuda; nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengenezea boriti kwa malango ya ngome ya hekalu, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakapoishi mimi. Naye mfalme akanipa, maana mkono mwema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu. Ndipo nikafika kwa watawala wa mkoa walio ng'ambo ya Mto, nikawapa nyaraka hizo za mfalme. Naye mfalme alikuwa ametuma maofisa wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami. Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli. Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu. Kisha nikaondoka usiku, mimi pamoja na watu wachache; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe. Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kwenye kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto. Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama niliyemganda. Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo. Wala maofisa hawakujua nilikokwenda, wala niliyotenda; tena nilikuwa sijawaambia Wayahudi, makuhani, wakuu, maofisa, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo. Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena. Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema. Lakini Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Ninyi mtaasi juu ya mfalme? Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu.
Nehemia 2:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote. Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana. Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto? Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni. Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga. Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda. Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda; nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu. Ndipo nikafika kwa maliwali walio ng’ambo ya Mto, nikawapa hizo nyaraka za mfalme. Naye mfalme alikuwa amepeleka maakida wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami. Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli. Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu. Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe. Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto. Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama aliyekuwa chini yangu. Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo. Wala mashehe hawakujua nilikokwenda, wala nilivyotenda; wala sijawaambia Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala mashehe, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo. Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena. Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema. Lakini waliposikia Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Mtaasi ninyi juu ya mfalme? Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu.
Nehemia 2:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa utawala wa Mfalme Artashasta, wakati divai ilipoletwa kwake, niliichukua na kumpa mfalme. Sikuwahi kuonekana mwenye huzuni mbele yake kabla ya hapo. Basi mfalme akaniuliza, “Kwa nini uso wako unaonekana una huzuni wakati wewe si mgonjwa? Jambo hili si kitu kingine bali ni huzuni ya moyo.” Niliogopa sana, lakini nikamwambia mfalme, “Mfalme na aishi milele! Kwa nini uso wangu usiwe na huzuni wakati mji walipozikwa baba zangu umebaki magofu, na malango yake yameteketezwa kwa moto?” Mfalme akaniambia, “Je, haja yako ni nini?” Ndipo nikaomba kwa Mungu wa mbinguni, na nikamjibu mfalme, “Ikimpendeza mfalme, na kama mtumishi wako amepata kibali machoni pake, anitume kule mji wa Yuda, mahali baba zangu walipozikwa, ili niweze kuujenga upya.” Kisha mfalme, huku malkia akiwa ameketi karibu naye, akaniuliza, “Safari yako itachukua muda gani, nawe utarudi lini?” Ilimpendeza mfalme kunituma, kwa hiyo nikapanga muda. Pia nikamwambia, “Ikimpendeza mfalme, naomba nipewe barua kwa watawala wa Ngʼambo ya Frati, ili wanipe ulinzi hadi nifike Yuda. Naomba nipewe barua nipeleke kwa Asafu, mtunzaji wa msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengeneza boriti kwa ajili ya malango ya ngome ya Hekalu, na ukuta wa mji, na makao yangu nitakayoishi.” Kwa kuwa mkono wenye neema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu, mfalme akanijalia ombi langu. Basi nilienda kwa watawala wa Ngʼambo ya Frati na kuwapa barua za mfalme. Pia mfalme alikuwa ametuma maafisa wa jeshi na askari wapanda farasi pamoja nami. Sanbalati Mhoroni na Tobia afisa Mwamoni waliposikia kuhusu jambo hili, waliudhika sana kwamba amekuja mtu kuinua ustawi wa Waisraeli. Nilienda Yerusalemu, na baada ya kukaa huko siku tatu, nikaondoka wakati wa usiku pamoja na watu wachache. Sikuwa nimemwambia mtu yeyote kile ambacho Mungu wangu alikuwa ameweka moyoni mwangu kufanya kwa ajili ya Yerusalemu. Hapakuwa na mnyama yeyote nami isipokuwa yule niliyekuwa nimempanda. Nikatoka nje usiku kupitia Lango la Bondeni, kuelekea Kisima cha Joka na Lango la Samadi, nikikagua kuta za Yerusalemu zilizokuwa zimebomolewa, na malango yake yaliyokuwa yameteketezwa kwa moto. Kisha nikaelekea hadi Lango la Chemchemi na Bwawa la Mfalme, lakini hapakuwa na nafasi ya kutosha mnyama wangu kupita, kwa hiyo nikapandia bondeni usiku nikikagua ukuta. Mwishoni nikarudi na kuingia tena kupitia Lango la Bondeni. Maafisa hawakujua nilikoenda wala nilichokuwa nikifanya, kwa sababu nilikuwa bado sijasema lolote kwa Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala maafisa, wala mtu yeyote ambaye angefanya kazi. Ndipo nilipowaambia, “Mnaona taabu tuliyo nayo: Yerusalemu imebaki magofu na malango yake yameteketezwa kwa moto. Njooni tujenge upya ukuta wa Yerusalemu, nasi hatutakuwa tena katika aibu hii.” Pia niliwaambia kuhusu mkono wenye neema wa Mungu wangu uliokuwa juu yangu, na kile mfalme alichokuwa ameniambia. Wakajibu, “Haya! Tuanze kujenga tena.” Kwa hiyo wakaanza kazi hii njema. Lakini Sanbalati Mhoroni, Tobia afisa Mwamoni, na Geshemu Mwarabu waliposikia kuhusu jambo hili, walitudhihaki na kutucheka. Wakauliza, “Ni nini hiki mnachokifanya? Je, mnaasi dhidi ya mfalme?” Nikawajibu kwa kusema, “Mungu wa mbinguni atatufanikisha. Sisi watumishi wake tutaanza kujenga upya, lakini ninyi hamna sehemu wala dai lolote, wala kumbukumbu la haki katika Yerusalemu.”