Nehemia 12:1-47
Nehemia 12:1-47 Biblia Habari Njema (BHN)
Ifuatayo ni orodha ya makuhani na Walawi waliorudi kutoka uhamishoni pamoja na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na kuhani mkuu Yeshua. Makuhani: Seraya, Yeremia, Ezra, Amaria, Maluki, Hatushi, Shekania, Rehumu, Meremothi, Ido, Ginethoni, Abiya, Miyamini, Maadia, Bilga, Shemaya, Yoyaribu, Yedaya, Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya. Hao walikuwa ni wakuu wa makuhani na ndugu zao wakati wa Yeshua. Walawi: Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda na Matania, ambaye alihusika na usimamizi wa nyimbo za shukrani akishirikiana na ndugu zake. Nao Bakbukia na Uno rafiki zao, walisimama ibadani mkabala nao. Yeshua alimzaa Yoyakimu, Yoyakimu alimzaa Eliashibu, Eliashibu alimzaa Yoyada, Yoyada alimzaa Yonathani na Yonathani akamzaa Yadua. Yoyakimu alipokuwa kuhani mkuu, makuhani wafuatao walikuwa wakuu wa koo zao: Wa Seraya, Meraya; wa Yeremia, Hanania; wa Ezra, Mehulamu; wa Amaria, Yehohanani; wa Maluki, Yonathani; wa Shebania, Yosefu; wa Harimu, Adna; wa Merayothi, Helkai; wa Ido, Zekaria; wa Ginethoni, Meshulamu; wa Abiya, Zikri; ukoo wa Miniamini; wa Moadia, Piltai; wa Bilga, Shamua; wa Shemaya, Yehonathani; wa Yoaribu, Matenai; wa Yedaya, Uzi; wa Salai, Kalai; wa Amoki, Eberi; wa Hilkia, Heshabia; na wa ukoo wa Yedaya, Nethaneli. Wakati wa Eliashibu, Yoyada, Yohanani na Yadua wakuu wa jamaa za Walawi, waliorodheshwa; vilevile wakati wa utawala wa mfalme Dario wakuu wa jamaa za makuhani waliorodheshwa. Wakuu wa jamaa za ukoo wa Lawi waliorodheshwa katika kitabu cha Kumbukumbu mpaka wakati wa Yohanani mjukuu wa Eliashibu. Viongozi wa Walawi: Hashabia, Sherebia, Yeshua mwana wa Kadmieli walisimama mkabala na ndugu zao; walipangwa kuimba nyimbo za kusifu na kushukuru, kufuatana na amri ya mfalme Daudi, mtu wa Mungu. Mabawabu walikuwa: Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni na Akubu; pia hao walikuwa walinzi wa ghala. Watu hao waliishi wakati wa Yoyakimu, mwana wa Yeshua mwana wa Yosadaki na pia wakati wa Nehemia aliyekuwa mtawala wa mkoa; na hata wakati wa Ezra kuhani na mwandishi. Kisha wakati wa kuweka wakfu ukuta wa Yerusalemu Walawi walitafutwa kila mahali walipokaa ili kuja Yerusalemu kusherehekea kwa furaha pamoja na shukrani na nyimbo, wakitumia matoazi, vinubi na zeze. Wazawa wa waimbaji wakakusanyika kutoka viunga vya Yerusalemu na vijiji vya Wanetofathi, pia kutoka Beth-gilgali, eneo la Geba na Azmawethi, kwa sababu waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kandokando ya Yerusalemu. Makuhani na Walawi walijitakasa, pia waliwatakasa watu, malango na ukuta. Niliwakusanya viongozi wote wa Yuda kwenye ukuta na kutenga waimbaji katika makundi mawili makubwa yaliyoimba nyimbo za shukrani wakiwa katika maandamano. Kundi moja lilielekea upande wa kulia wa ukuta hadi kwenye Lango la Takataka. Waimbaji hao walifuatiwa na Hoshaya akiwa pamoja na nusu ya viongozi wa Yuda. Pamoja naye walikwenda Azaria, Ezra, Meshulamu, Yuda, Benyamini, Shemaya na Yeremia. Wazawa wafuatao wa makuhani walikuwa na tarumbeta: Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya aliyekuwa mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu. Ndugu zake wafuatao waliimba kwa ala za muziki za mfalme Daudi, mtu wa Mungu, yaani Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, walitanguliwa na Ezra mwandishi. Kwenye Lango la Chemchemi walipanda ngazi kuelekea mji wa Daudi, wakaipita Ikulu ya Daudi, na kuelekea nyuma kwenye ukuta hadi kwenye Lango la Maji, mashariki ya mji. Kundi lingine lililoimba nyimbo za shukrani lilielekea upande wa kushoto juu ya ukuta. Mimi nilifuatana na kundi hili pamoja na nusu ya watu. Tulipitia Mnara wa Tanuri hadi kwenye Ukuta Mpana. Na kutoka hapo, tulipitia Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, Mnara wa Mia Moja mpaka kwenye Lango la Kondoo. Tulimalizia maandamano yetu kwenye Lango la Gereza. Hivyo, makundi yote mawili yaliyokuwa yanaimba nyimbo za shukrani yalisimama katika nyumba ya Mungu, pamoja nami na nusu ya viongozi; hata na makuhani waliokuwa na tarumbeta: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Eliehoenai, Zekaria na Hanania. Hao walifuatwa na Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Waimbaji waliimba wakiongozwa na Yezrahia. Siku hiyo, watu walitoa tambiko nyingi na kufurahi kwani Mungu aliwafanya wawe na furaha kubwa. Pia wanawake na watoto, wote walifurahi. Vigelegele vya furaha toka mjini Yerusalemu vilisikika mbali. Wakati huo walichaguliwa watu wa kutunza vyumba vya ghala ambamo matoleo kwa ajili ya hekalu yalitunzwa, malimbuko ya kwanza, zaka na kuyakusanya kutoka mashamba ya miji, kwa ajili ya makuhani na Walawi kama ilivyotakiwa na sheria. Watu wote waliwafurahia makuhani na Walawi waliohudumu, kwa sababu walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, kama waimbaji walivyoimba hata walinzi wa malango kulingana na agizo la mfalme Daudi na Mfalme Solomoni mwanawe. Tangu wakati wa mfalme Daudi na Asafu kulikuweko kiongozi wa waimbaji, na kulikuwako nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu. Watu wote wa Israeli, tangu wakati wa Zerubabeli na Nehemia, walitoa matoleo ya kila siku ambayo yaliwatunza waimbaji walinda malango. Zaidi ya yote, watu wa Israeli walitoa matoleo kwa ajili ya Walawi, nao Walawi wakatenga sehemu kwa ajili ya wazawa wa Aroni.
Nehemia 12:1-47 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, hawa ndio makuhani na Walawi waliopanda na Zerubabeli, mwana wa Shealueli, na Yoshua; Seraya, Yeremia, Ezra; Amaria, Maluki, Hatushi; Shekania, Harimu, Meremothi; Ido, Ginethoni, Abia; Miyamini, Maazia, Bilgai; Shemaya, Yoyaribu, Yedaya; Salu, Amoki, Hilkia, Yedaya. Hawa walikuwa wakuu wa makuhani na ndugu zao siku za Yoshua. Tena Walawi; Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, na Matania, aliyekuwa juu ya shukrani, yeye na ndugu zake. Tena Bakbukia na Uno, washiriki wenzao walisimama mkabala wao. Naye Yoshua akamzaa Yoyakimu, Yoyakimu akamzaa Eliashibu, Eliashibu akamzaa Yoyada, Yoyada akamzaa Yohana, Yohana akamzaa Yadua. Na siku za Yoyakimu wakawako makuhani, wakuu wa mbari za mababa; wa Seraya, Meraya; wa Yeremia, Hanania; wa Ezra, Meshulamu; wa Amaria, Yehohanani; wa Maluki, Yonathani; wa Shekania, Yusufu; wa Harimu, Adna; wa Meremothi, Helkai; wa Ido, Zekaria; wa Ginethoni, Meshulamu; wa Abia, Zikri; wa Miyamini; wa Maazia, Piltai; wa Bilgai, Shamua; wa Shemaya, Yehonathani; wa Yoyaribu, Matenai; wa Yedaya, Uzi; wa Salu, Kalai; wa Amoki, Eberi; wa Hilkia, Hashabia; wa Yedaya, Nethaneli. Walawi siku za Eliashibu, na Yoyada, na Yohana, na Yadua, wameorodheshwa wakuu wa mbari za mababa; tena na makuhani; hata siku za kumiliki kwake Dario, Mwajemi. Wana wa Lawi, wakuu wa mbari za mababa, wameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu hadi siku za Yohana mwana wa Eliashibu. Nao wakuu wa Walawi; Hashabia, Sherebia, Yeshua, Binui, Kadmieli, na ndugu zao kuwaelekea, ili kusifu na kushukuru, kama amri ya Daudi, mtu wa Mungu, zamu kwa zamu. Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni, na Akubu, walikuwa mabawabu, wa kulinda nyumba za hazina katika malango. Hao walikuwapo siku za Yoyakimu, mwana ya Yoshua, mwana wa Yosadaki, na siku za Nehemia, mtawala, na Ezra, kuhani na mwandishi. Basi, walipouweka wakfu ukuta wa Yerusalemu wakawatafuta Walawi katika mahali pao pote, ili kuwaleta Yerusalemu, ili waweze kusherehekea kuweka wakfu pamoja na furaha, na kwa shukrani, na kwa kuimba, kwa matoazi, vinanda na vinubi. Waimbaji wakakusanyika kutoka uwanda na viunga vya Yerusalemu, na kutoka vijiji vya Wanetofathi; tena kutoka Beth-gilgali, na toka mashamba ya Geba na Azmawethi; kwa maana waimbaji hao walikuwa wamejijengea vijiji katika viunga vya Yerusalemu. Makuhani na Walawi wakajitakasa, nao wakawatakasa watu, na malango, na ukuta. Ndipo nikawapandisha viongozi wa Yuda juu ya ukuta, nikawatenga makundi mawili makubwa ya hao walioandamana na kushukuru, liende upande wa kulia ukutani kuliendea lango la jaa; na baada yao wakaenda Hoshaya, na nusu ya wakuu wa Yuda, na Azaria, na Ezra, na Meshulamu, na Yuda, na Benyamini, na Shemaya, na Yeremia, na baadhi ya makuhani wenye baragumu; Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu; na ndugu zake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda, na Hanani, wenye vinanda vya Daudi mtu wa Mungu; Ezra, mwandishi, akawatangulia; na kwa lango la chemchemi, wakienda moja kwa moja mbele yao, wakapanda madaraja ya mji wa Daudi, uinukapo ukuta, juu ya nyumba ya Daudi, mpaka lango la maji upande wa mashariki. Na kundi la pili wao wenye kushukuru wakaenda kuwalaki, na mimi nikafuata nyuma yao, pamoja na nusu ya watu, ukutani juu ya mnara wa tanuri, mpaka ule ukuta mpana; na juu ya lango la Efraimu, na kupita lango la kale, na lango la samaki, na mnara wa Hananeli, na mnara wa Hamea, mpaka lango la kondoo; nao wakasimama hapo langoni pa gereza. Ndivyo walivyosimama makundi mawili yao walioshukuru nyumbani mwa Mungu, na mimi, na nusu ya viongozi pamoja nami; na makuhani, Eliakimu, Maaseya, Miyamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania, wenye baragumu; na Maaseya, na Shemaya, na Eleazari, na Uzi, na Yehohanani, na Malkiya, na Elamu, na Ezeri. Waimbaji wakaimba kwa sauti kuu, akiwa Yezrahia msimamizi wao. Wakatoa dhabihu nyingi siku ile, wakafurahi; kwa kuwa Mungu amewafurahisha furaha kuu; na wanawake pia na watoto wakafurahi; hata ikasikika mbali sana furaha hiyo ya Yerusalemu. Na siku hiyo watu wakaagizwa juu ya vyumba vya hazina, kwa sadaka za kuinuliwa, na kwa malimbuko, na kwa zaka, ili kuzikusanya, kwa kadiri ya mashamba ya miji, sehemu zilizoamriwa katika torati za makuhani, na Walawi; kwa maana Yuda waliwafurahia makuhani na Walawi waliotumika. Wakauangalia ulinzi wa Mungu wao, na ulinzi wa kutakasika, na hao waimbaji na mabawabu vile vile, sawasawa na amri ya Daudi, na ya Sulemani mwanawe. Kwa kuwa siku za Daudi zamani, Asafu alikuwa mkuu wa waimbaji, na juu ya nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu. Na Israeli wote, siku za Zerubabeli, na siku za Nehemia, walitoa sehemu za waimbaji na mabawabu, kama ilivyohusika kila siku; nao wakawatakasia Walawi; na Walawi wakawatakasia wana wa Haruni.
Nehemia 12:1-47 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, hawa ndio makuhani na Walawi waliopanda na Zerubabeli, mwana wa Shealueli, na Yoshua; Seraya, Yeremia, Ezra; Amaria, Maluki, Hatushi; Shekania, Harimu, Meremothi; Ido, Ginethoni, Abia; Miyamini, Maazia, Bilgai; Shemaya, Yoyaribu, Yedaya; Salu, Amoki, Hilkia, Yedaya. Hawa walikuwa wakuu wa makuhani na ndugu zao siku za Yoshua. Tena Walawi; Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, na Matania, aliyekuwa juu ya shukrani, yeye na ndugu zake. Tena Bakbukia na Uno, ndugu zao, kuwaelekea kwa zamu. Naye Yoshua akamzaa Yoyakimu, Yoyakimu akamzaa Eliashibu, Eliashibu akamzaa Yoyada, Yoyada akamzaa Yohana, Yohana akamzaa Yadua. Na siku za Yoyakimu wakawako makuhani, wakuu wa mbari za mababa; wa Seraya, Meraya; wa Yeremia, Hanania; wa Ezra, Meshulamu; wa Amaria, Yehohanani; wa Maluki, Yonathani; wa Shekania, Yusufu; wa Harimu, Adna; wa Meremothi, Helkai; wa Ido, Zekaria; wa Ginethoni, Meshulamu; wa Abia, Zikri; wa Miyamini; wa Maazia, Piltai; wa Bilgai, Shamua; wa Shemaya, Yehonathani; wa Yoyaribu, Matenai; wa Yedaya, Uzi; wa Salu, Kalai; wa Amoki, Eberi; wa Hilkia, Hashabia; wa Yedaya, Nethaneli. Walawi siku za Eliashibu, na Yoyada, na Yohana, na Yadua, wameandikwa wakuu wa mbari za mababa; tena na makuhani; hata siku za kumiliki kwake Dario, Mwajemi. Wana wa Lawi, wakuu wa mbari za mababa, wameandikwa katika kitabu cha tarehe, hata siku za Yohana mwana wa Eliashibu. Nao wakuu wa Walawi; Hashabia, Sherebia, Yeshua, Binui, Kadmieli, na ndugu zao kuwaelekea, ili kusifu na kushukuru, kama amri ya Daudi, mtu wa Mungu, zamu kwa zamu. Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni, na Akubu, walikuwa mabawabu, wa kulinda nyumba za hazina penye malango. Hao walikuwapo siku za Yoyakimu, mwana ya Yoshua, mwana wa Yosadaki, na siku za Nehemia, liwali, na Ezra, kuhani, mwandishi. Basi, walipouweka wakfu ukuta wa Yerusalemu wakawatafuta Walawi katika mahali pao pote, ili kuwaleta Yerusalemu, wapate kufanya wakfu pamoja na furaha, na kwa shukrani, na kwa kuimba, kwa matoazi, vinanda na vinubi. Waimbaji wakakusanyika kutoka uwanda na viunga vya Yerusalemu, na kutoka vijiji vya Wanetofathi; tena toka Beth-gilgali, na toka mashamba ya Geba na Azmawethi; kwa maana waimbaji hao walikuwa wamejijengea vijiji katika viunga vya Yerusalemu. Makuhani na Walawi wakajitakasa, nao wakawatakasa watu, na malango, na ukuta. Ndipo nikawapandisha wakuu wa Yuda juu ya ukuta, nikawaagiza mikutano mikubwa miwili ya hao walioshukuru, na kuandamana; mmoja uende kwa kuume ukutani kuliendea lango la jaa; na baada yao wakaenda Hoshaya, na nusu ya wakuu wa Yuda, na Azaria, na Ezra, na Meshulamu, na Yuda, na Benyamini, na Shemaya, na Yeremia, na baadhi ya makuhani wenye baragumu; Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu; na ndugu zake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda, na Hanani, wenye vinanda vya Daudi mtu wa Mungu; Ezra, mwandishi, akawatangulia; na kwa lango la chemchemi, wakienda moja kwa moja mbele yao, wakapanda madaraja ya mji wa Daudi, uinukapo ukuta, juu ya nyumba ya Daudi, mpaka lango la maji upande wa mashariki. Na mkutano wa pili wao wenye kushukuru wakaenda kuwalaki, na mimi nikafuata nyuma yao, pamoja na nusu ya watu, ukutani juu ya mnara wa tanuu, mpaka ule ukuta mpana; na juu ya lango la Efraimu, na kupita lango la kale, na lango la samaki, na mnara wa Hananeli, na mnara wa Hamea, mpaka lango la kondoo; nao wakasimama hapo langoni pa gereza. Ndivyo walivyosimama mikutano miwili yao walioshukuru nyumbani mwa Mungu, na mimi, na nusu ya mashehe pamoja nami; na makuhani, Eliakimu, Maaseya, Miyamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania, wenye baragumu; na Maaseya, na Shemaya, na Eleazari, na Uzi, na Yehohanani, na Malkiya, na Elamu, na Ezeri. Waimbaji wakaimba kwa sauti kuu, wenye Yezrahia kuwa msimamizi wao. Wakatoa dhabihu nyingi siku ile, wakafurahi; kwa kuwa Mungu amewafurahisha furaha kuu; na wanawake pia na watoto wakafurahi; hata ikasikiwa mbali sana furaha hiyo ya Yerusalemu. Na siku hiyo watu wakaagizwa juu ya vyumba vya hazina, kwa sadaka za kuinuliwa, na kwa malimbuko, na kwa zaka, ili kuzikusanya, kwa kadiri ya mashamba ya miji, sehemu zilizoamriwa katika torati za makuhani, na Walawi; kwa maana Yuda waliwafurahia makuhani na Walawi waliotumika. Wakauangalia ulinzi wa Mungu wao, na ulinzi wa kutakasika, na hao waimbaji na mabawabu vile vile, sawasawa na amri ya Daudi, na ya Sulemani mwanawe. Kwa kuwa siku za Daudi zamani, Asafu alikuwa mkuu wa waimbaji, na juu ya nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu. Na Israeli wote, siku za Zerubabeli, na siku za Nehemia, walitoa sehemu za waimbaji na mabawabu, kama ilivyohusika kila siku; nao wakawatakasia Walawi; na Walawi wakawatakasia wana wa Haruni.
Nehemia 12:1-47 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wafuatao walikuwa makuhani na Walawi ambao walirudi na Zerubabeli mwana wa Shealtieli pamoja na Yeshua: Seraya, Yeremia, Ezra, Amaria, Maluki, Hatushi, Shekania, Rehumu, Meremothi, Ido, Ginethoni, Abiya, Miyamini, Moadia, Bilga, Shemaya, Yoyaribu, Yedaya, Salu, Amoki, Hilkia na Yedaya. Hawa walikuwa viongozi wa makuhani na wenzao wakati wa Yeshua. Walawi walikuwa Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, na pia Matania, ambaye pamoja na wenzake, alikuwa kiongozi wa nyimbo za shukrani. Bakbukia na Uni, wenzao, walisimama mkabala nao wakati wa ibada. Yeshua alikuwa baba wa Yoyakimu, Yoyakimu alikuwa baba wa Eliashibu, Eliashibu alikuwa baba wa Yoyada, Yoyada alikuwa baba wa Yonathani, na Yonathani alikuwa baba wa Yadua. Katika siku za Yoyakimu, kulikuwa na wakuu wa jamaa za kikuhani: wa jamaa ya Seraya, Meraya; wa jamaa ya Yeremia, Hanania; wa jamaa ya Ezra, Meshulamu; wa jamaa ya Amaria, Yehohanani; wa jamaa ya Maluki, Yonathani; wa jamaa ya Shebania, Yusufu; wa jamaa ya Harimu, Adna; wa jamaa ya Meremothi, Helkai; wa jamaa ya Ido, Zekaria; wa jamaa ya Ginethoni, Meshulamu; wa jamaa ya Abiya, Zikri; wa jamaa ya Miyamini na ya Maazia, Piltai; wa jamaa ya Bilgai, Shamua; wa jamaa ya Shemaya, Yehonathani; wa jamaa ya Yoyaribu, Matenai; wa jamaa ya Yedaya, Uzi; wa jamaa ya Salu, Kalai; wa jamaa ya Amoki, Eberi; wa jamaa ya Hilkia, Hashabia; wa jamaa ya Yedaya, Nethaneli. Wakuu wa jamaa za Walawi katika siku za Eliashibu, Yoyada, Yohanani na Yadua, pia wale jamaa za makuhani, waliandikishwa wakati wa utawala wa Dario Mwajemi. Wakuu wa jamaa miongoni mwa wazao wa Lawi hadi wakati wa Yohanani mwana wa Eliashibu waliandikishwa katika kitabu cha kumbukumbu. Viongozi wa Walawi walikuwa: Hashabia, Sherebia, Yeshua mwana wa Kadmieli na wenzao, waliosimama mkabala nao kusifu na kushukuru, sehemu moja ikipokezana na nyingine kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mabawabu waliokuwa wakilinda kwenye malango ya ghala ni: Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni na Akubu. Walihudumu siku za Yoyakimu mwana wa Yeshua, mwana wa Yosadaki, na katika siku za mtawala Nehemia, na za Ezra kuhani na mwandishi. Wakati wa kuwekwa wakfu ukuta wa Yerusalemu, Walawi walitafutwa kule walikokuwa wakiishi, nao wakaletwa Yerusalemu kuadhimisha kwa shangwe kuweka wakfu kwa nyimbo za shukrani na kwa uimbaji wakitumia matoazi, vinubi na zeze. Pia waimbaji walikusanywa pamoja kutoka maeneo yaliyozunguka Yerusalemu, kutoka vijiji vya Wanetofathi, kutoka Beth-Gilgali, na kutoka eneo la Geba na Azmawethi, kwa kuwa waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kuzunguka Yerusalemu. Makuhani na Walawi walipokuwa wamekwisha kujitakasa kulingana na desturi, waliwatakasa watu, malango na ukuta. Niliwaagiza viongozi wa Yuda wapande juu ya ukuta. Pia niliagiza makundi mawili makubwa ya waimbaji waimbe nyimbo za kumshukuru Mungu. Kundi moja lilipanda juu ya ukuta upande wa kuume, kuelekea Lango la Samadi. Hoshaya na nusu ya viongozi wa Yuda wakawafuata, pamoja na Azaria, Ezra, Meshulamu, Yuda, Benyamini, Shemaya, Yeremia, pamoja na baadhi ya makuhani wenye tarumbeta, na pia walikuwa na Zekaria mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu, pamoja na wenzake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, wakiwa na vyombo vya uimbaji, kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mwandishi Ezra aliongoza maandamano. Kwenye Lango la Chemchemi waliendelea moja kwa moja mpaka kwenye ngazi za Mji wa Daudi, kwenye mwinuko wa ukuta, na kupitia juu ya nyumba ya Daudi mpaka kwenye Lango la Maji upande wa mashariki. Kundi la pili la waimbaji lilielekea upande wa kushoto. Niliwafuata juu ya ukuta, pamoja na nusu ya watu kupitia Mnara wa Tanuru hadi kwenye Ukuta Mpana, juu ya Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, na Mnara wa Mia, hadi kwenye Lango la Kondoo. Walipofika kwenye Lango la Ulinzi wakasimama. Kisha yale makundi mawili ya waimbaji yaliyoshukuru yakachukua nafasi zao katika nyumba ya Mungu. Nami pia nikafanya hivyo, pamoja na nusu ya maafisa, na makuhani wafuatao: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania wakiwa na tarumbeta zao, na pia Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Makundi haya yaliimba chini ya uongozi wa Yezrahia. Siku hiyo watu walitoa dhabihu nyingi, wakishangilia kwa sababu Mungu aliwapa furaha kuu. Wanawake na watoto walishangilia pia. Sauti ya kushangilia huko Yerusalemu iliweza kusikika mbali sana. Wakati huo watu walichaguliwa kuwa wasimamizi wa vyumba vya ghala kwa ajili ya matoleo, malimbuko na zaka. Kutoka yale mashamba yaliyozunguka miji walipaswa walete kwenye ghala mafungu kama sheria ilivyoamuru kwa ajili ya makuhani na Walawi, kwa kuwa Yuda alifurahishwa na huduma ya makuhani na Walawi. Walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, nao waimbaji na walinzi wa lango wakafanya hivyo pia, kufuatana na amri za Daudi na Sulemani mwanawe. Muda mrefu uliopita, katika siku za Daudi na Asafu, kulikuwa na viongozi wa waimbaji na wa nyimbo za sifa na za kumshukuru Mungu. Kwa hiyo katika siku za Zerubabeli na za Nehemia, Israeli wote walitoa mafungu kila siku kwa ajili ya waimbaji na mabawabu. Pia walitenga fungu kwa ajili ya Walawi wengine, nao Walawi walitenga fungu kwa ajili ya wazao wa Haruni.