Nehemia 1:1-4
Nehemia 1:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
Lifuatalo ni simulizi la Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa, nilipokuwa katika mji mkuu wa Susa, katika mwezi wa Kislevu wa mwaka wa ishirini, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akaja pamoja na baadhi ya watu toka nchini Yuda. Nikawauliza kuhusu Wayahudi wenzetu waliosalimika, yaani ambao hawakuhamishiwa Babuloni na kuhusu mji wa Yerusalemu. Wao wakaniambia, “Wayahudi waliosalimika na kubaki katika mkoa ule, wako katika taabu na aibu. Ukuta wa mji wa Yerusalemu umebomolewa na malango yake yameteketea.” Niliposikia hayo nilikaa chini na kulia, nikaomboleza kwa siku kadhaa. Nikafunga na kumwomba Mungu wa mbinguni
Nehemia 1:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kislevu, mwaka wa ishirini, nilipokuwapo Shushani ngomeni, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliosalimika, ambao hawakuchukuliwa uhamishoni na habari za Yerusalemu. Wakaniambia, Watu waliosalimika, waliosalia huko katika mkoa ule, wamo katika hali ya dhiki kubwa na aibu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto. Hapo niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadhaa; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni
Nehemia 1:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisleu, mwaka wa ishirini, nilipokuwapo Shushani ngomeni, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu. Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto. Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni
Nehemia 1:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia: Katika mwezi wa Kislevu katika mwaka wa ishirini, wakati nilikuwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi wale walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu. Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni, wale ambao wamerudi kwenye lile jimbo, wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.” Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni.