Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Nahumu 3:1-19

Nahumu 3:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wako mji wa mauaji! Umejaa udanganyifu mtupu na nyara tele, usiokoma kamwe kuteka nyara. Sikia! Mlio wa mjeledi, mrindimo wa magurudumu, vishindo vya farasi na ngurumo za magari! Wapandafarasi wanashambulia, panga na mikuki inametameta; waliouawa hawana idadi, maiti wengi sana; watu wanajikwaa juu ya maiti! Ninewi! Wewe umekuwa kama malaya. Umewashawishi watu, ewe binti wa uchawi, uliyeyafanya mataifa kuwa watumwa kwa umalaya wako, na watu wa mataifa kwa uchawi wako. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema nitapambana nawe; nitalipandisha vazi lako hadi kichwani, niyaache mataifa yauone uchi wako, tawala ziikodolee macho aibu yako. Nitakutupia uchafu, na kukutendea kwa dharau, na kukufanya uwe kioja kwa watu. Kisha wote watakaokuona watakukimbia wakisema, “Ninewi umeangamizwa, ni nani atakayeuombolezea? Nani atakayekufariji?” Je, wewe Ninewi, ni bora kuliko Thebesi, mji uliojengwa kando ya mto Nili? Thebesi ulizungukwa na maji, bahari ilikuwa boma lake, maji yalikuwa ukuta wake! Kushi ilikuwa nguvu yake; nayo Misri pia, tena bila kikomo; watu wa Puti na Libia waliusaidia! Hata hivyo, ulichukuliwa mateka, watu wake wakapelekwa uhamishoni. Hata watoto wake walipondwapondwa katika pembe ya kila barabara; watu wake mashuhuri walinadiwa, wakuu wake wote walifungwa minyororo. Ninewi, nawe pia utalewa; utamkimbia adui na kujaribu kujificha. Ngome zako zote ni za tini za mwanzo; zikitikiswa zinamwangukia mlaji kinywani. Tazama askari wako: Wao ni waoga kama wanawake. Milango ya nchi yako ni wazi mbele ya adui zako; moto umeyateketeza kabisa makomeo yake. Tekeni maji muwe tayari kuzingirwa; imarisheni ngome zenu. Pondeni udongo kwa kuukanyagakanyaga, tayarisheni tanuri ya kuchomea matofali! Lakini huko pia moto utawateketezeni, upanga utawakatilia mbali; utawamaliza kama nzige walavyo. Ongezekeni kama nzige, naam, ongezekeni kama panzi! Wafanyabiashara wako waliongezeka kuliko nyota; lakini sasa wametoweka kama panzi warukavyo. Wakuu wako ni kama panzi, maofisa wako kama kundi la nzige; wakati wa baridi wanakaa kwenye kuta, lakini jua lichomozapo, huruka, wala hakuna ajuaye walikokwenda. Ewe mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wamelala, waheshimiwa wako wamesinzia. Watu wako wametawanyika milimani, wala hakuna yeyote wa kuwakusanya. Hakuna wa kuyapa nafuu majeraha yako, vidonda vyako ni vya kifo. Wote wanaosikia habari zako wanashangilia. Maana ni nani aliyeuepa ukatili wako usio na kikomo?

Shirikisha
Soma Nahumu 3

Nahumu 3:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang'anyi; mateka hayaondoki. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kuparapara, na magari ya vita yenye kurukaruka; mpanda farasi akipanda, na upanga ukimetameta, na mkuki ukimeremeta; na wingi wa waliouawa, na rundo kubwa la mizoga; mizoga isiyo na mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao. Kwa sababu ya wingi wa ukahaba wa yule kahaba mzuri, yule bibi wa mambo ya uchawi, auzaye mataifa kwa ukahaba wake, na jamaa za watu kwa uchawi wake. Tazama, mimi ni juu yako, asema BWANA wa majeshi; nami nitayainua marinda yako mbele ya uso wako; nami nitawaonesha mataifa uchi wako, na falme aibu yako. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji? Je! Wewe u mwema kuliko No-amoni, uliowekwa kati ya mito, uliozungukwa na maji; ambao boma lake lilikuwa bahari, na bahari ilikuwa ukuta wake. Kushi na Misri walikuwa nguvu zake, nazo zilikuwa hazina mpaka; Puti na Walibya walikuwa wasaidizi wake. Hata hivyo alichukuliwa mbali, alikwenda utumwani; watoto wake wachanga walisetwa kwenye maachano ya njia kuu zote; watu wake wenye heshima wakapigiwa kura, na wakuu wake wote wakafungwa kwa minyororo. Tena utalewa, utafichwa; tena utatafuta ngome kwa sababu ya adui. Ngome zako zote zitakuwa kama mitini yenye tini zilizoiva kwanza; ikitikisika zaanguka katika kinywa chake alaye. Tazama, watu wako walio ndani yako ni wanawake; malango ya nchi yako yamekuwa wazi kabisa mbele ya adui zako; moto umeteketeza mapingo yako. Teka maji yawe tayari kwa kuzingirwa kwako; Zitie nguvu ngome zako; Ingia katika udongo, yakanyage matope, Itie nguvu tanuri ya kuokea matofali. Huko moto utakuteketeza; Upanga utakukatilia mbali; Utakumeza kama tunutu alavyo; Jifanye kuwa wengi kama tunutu! Jifanye kuwa wengi kama nzige! Umeongeza wafanya biashara wako kuwa wengi kuliko nyota za mbinguni; tunutu huharibu; kisha huruka juu na kwenda zake. Watu wako waliotiwa taji ni kama nzige, na majemadari wako ni kama makundi ya mapanzi, watuao katika vitalu siku ya baridi, lakini jua lipandapo huruka juu na kwenda zao, wala hapana ajuaye walikokwenda. Wachungaji wako wanalala usingizi, Ee mfalme wa Ashuru; watu wako wenye heshima wamepumzika; watu wako wametawanyika juu ya milima, wala hapana mtu wa kuwakusanya. Jeraha lako halipunguziki; donda lako haliponyeki; wote wasikiao habari zako wapiga makofi juu yako; kwa maana ni nani aliyewahi kuukwepa ukatili wako usio na mwisho?

Shirikisha
Soma Nahumu 3

Nahumu 3:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang’anyi; mateka hayaondoki. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka; mpanda farasi akipanda, na upanga ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao. Kwa sababu ya wingi wa ukahaba wa yule kahaba mzuri, yule bibi wa mambo ya uchawi, auzaye mataifa kwa ukahaba wake, na jamaa za watu kwa uchawi wake. Tazama, mimi ni juu yako, asema BWANA wa majeshi; nami nitafunua marinda yako mbele ya uso wako; nami nitawaonyesha mataifa uchi wako, na falme aibu yako. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji? Je! Wewe u mwema kuliko No-amoni, uliowekwa kati ya mito, uliozungukwa na maji; ambao boma lake lilikuwa bahari, na bahari ilikuwa ukuta wake. Kushi na Misri walikuwa nguvu zake, nazo zilikuwa hazina mpaka; Putu na Walibia walikuwa wasaidizi wake. Hata hivyo alichukuliwa mbali, alikwenda utumwani; watoto wake wachanga walisetwa kwenye maachano ya njia kuu zote; watu wake wenye heshima wakapigiwa kura, na wakuu wake wote wakafungwa kwa minyororo. Tena utalewa, utafichwa; tena utatafuta ngome kwa sababu ya adui. Ngome zako zote zitakuwa kama mitini yenye tini zilizoiva kwanza; ikitikisika zaanguka katika kinywa chake alaye. Tazama, watu wako walio ndani yako ni wanawake; malango ya nchi yako yamekuwa wazi kabisa mbele ya adui zako; moto umeteketeza mapingo yako. Teka maji yawe tayari kwa kuzingirwa kwako; Zitie nguvu ngome zako; Ingia katika udongo, yakanyage matope, Itie nguvu tanuru ya kuokea matofali. Huko moto utakuteketeza; Upanga utakukatilia mbali; Utakumeza kama tunutu alavyo; Jifanye kuwa wengi kama tunutu! Jifanye kuwa wengi kama nzige! Umeongeza wafanya biashara wako kuwa wengi kuliko nyota za mbinguni; tunutu huharibu; kisha huruka juu na kwenda zake. Watu wako waliotiwa taji ni kama nzige, na majemadari wako ni kama makundi ya mapanzi, watuao katika vitalu siku ya baridi, lakini jua lipandapo huruka juu na kwenda zao, na mahali pao walipo hapajulikani. Wachungaji wako wanalala usingizi, Ee mfalme wa Ashuru; watu wako wenye heshima wamepumzika; watu wako wametawanyika juu ya milima, wala hapana mtu wa kuwakusanya. Jeraha yako haipunguziki; jeraha yako ni nzito sana; wote wasikiao habari zako wapiga makofi juu yako; kwa maana ni nani ambaye uovu wako haukupita juu yake daima?

Shirikisha
Soma Nahumu 3

Nahumu 3:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ole wa mji unaomwaga damu, uliojaa uongo, uliojaa nyara, na usiokosa mateka. Kelele za mijeledi, vishindo vya magurudumu, farasi wanaoenda mbio na mshtuo wa magari ya vita! Wapanda farasi wanaenda mbio, panga zinametameta, na mikuki inangʼaa! Majeruhi wengi, malundo ya maiti, idadi ya miili isiyohesabika, watu wanajikwaa juu ya mizoga: haya yote kwa sababu ya wingi wa tamaa za kahaba, anayeshawishi, bibi mkuu wa mambo ya uchawi, anayewatia utumwani mataifa kwa ukahaba wake na pia jamaa za watu kwa ulozi wake. BWANA wa majeshi anasema, “Mimi ni kinyume na ninyi. Nitafunika uso wako kwa gauni lako. Nitaonesha mataifa uchi wako na falme aibu yako. Nitakutupia uchafu, nitakufanyia dharau na kukufanya kioja. Wote wanaokuona watakukimbia na kusema, ‘Ninawi inaangamia, nani atakayeomboleza kwa ajili yake?’ Nitampata wapi yeyote wa kukufariji?” Je, wewe ni bora kuliko No-Amoni, uliopo katika Mto Naili, uliozungukwa na maji? Mto ulikuwa kinga yake, nayo maji yalikuwa ukuta wake. Kushi na Misri walikuwa nguvu zake zisizo na mpaka; Putu na Libia walikuwa miongoni mwa wale walioungana naye. Hata hivyo alichukuliwa mateka na kwenda uhamishoni. Watoto wake wachanga walivunjwa vunjwa vipande kwenye mwanzo wa kila barabara. Kura zilipigwa kwa watu wake wenye heshima, na watu wake wote wakuu walifungwa kwa minyororo. Wewe pia utalewa; utaenda mafichoni na kutafuta kimbilio kutoka kwa adui. Ngome zako zote ni kama mitini yenye matunda yake ya kwanza yaliyoiva; wakati inapotikiswa, tini huanguka kwenye kinywa chake alaye. Tazama vikosi vyako: wote ni wanawake! Malango ya nchi yako yamekuwa wazi kwa adui zako; moto umeteketeza mapingo yake. Teka maji kwa ajili ya kuzingirwa kwako, imarisha ulinzi wako, Ufanyie udongo wa mfinyanzi kazi, yakanyage matope, karabati tanuru la kuchomea matofali! Huko moto utakuteketeza, huko upanga utakuangusha chini na kama vile panzi, watakumaliza. Ongezeka kama panzi, ongezeka kama nzige! Umeongeza idadi ya wafanyabiashara wako hata wamekuwa wengi kuliko nyota za angani, lakini kama nzige wanaacha nchi tupu kisha huruka na kwenda zake. Walinzi wako ni kama nzige, maafisa wako kama makundi ya nzige wanaotua kwenye kuta wakati wa siku ya baridi; lakini wakati jua linapotokea wanaruka kwenda zao, na hakuna anayejua wanakoenda. Ee mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wanasinzia; wakuu wako wanalala chini mavumbini kupumzika. Watu wako wametawanyika juu ya milima bila kuwa na mtu yeyote wa kuwakusanya. Hakuna kitu kinachoweza kuponya jeraha lako; jeraha lako ni la kukuua. Kila anayesikia habari zako, hupiga makofi kwa kuanguka kwako, kwa kuwa ni nani ambaye hajaguswa na ukatili wako usio na mwisho?

Shirikisha
Soma Nahumu 3