Marko 9:2-9
Marko 9:2-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane juu ya mlima mrefu peke yao. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, mavazi yake yakangaa, yakawa meupe sana, jinsi dobi yeyote duniani asingeweza kuyafanya meupe. Elia na Mose wakawatokea, wakazungumza na Yesu. Petro akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vizuri sisi kuwapo hapa. Basi, afadhali tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Yeye na wenzake waliogopa hata hakujua la kusema. Kisha likatokea wingu likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, msikilizeni.” Mara wanafunzi hao wakatazama tena, lakini hawakumwona mtu mwingine, ila Yesu peke yake pamoja nao. Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu aliwakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, mpaka Mwana wa Mtu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.
Marko 9:2-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimetameta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hadi Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.
Marko 9:2-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.
Marko 9:2-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao. Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko vile mtu yeyote duniani angeweza kuyangʼarisha. Musa na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Yesu. Petro akamwambia Yesu, “Rabi, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Eliya.” Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana. Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.” Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Yesu. Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoyaona, hadi Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.