Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 1:21-45

Marko 1:21-45 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika sunagogi, akaanza kufundisha. Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama waalimu wao wa sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka. Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, akapaza sauti, “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” Yesu akamkemea huyo pepo akisema, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu.” Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika eneo la Galilaya. Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao. Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili. Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia. Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo. Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango. Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani. Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali. Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta. Walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta.” Yesu akawaambia, “Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo.” Basi, akaenda kila mahali huko Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo. Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba: “Ukitaka, waweza kunitakasa!” Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, “Nataka! Takasika!” Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika. Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwambia, “Angalia usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

Shirikisha
Soma Marko 1

Marko 1:21-45 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea haraka kote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, akiugua homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa wagonjwa, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni mahali pengine, katika vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana nilikuja kwa ajili ya hilo. Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo. Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila nenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa ajili ya kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini waziwazi; bali alikaa nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila upande.

Shirikisha
Soma Marko 1

Marko 1:21-45 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya. Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo. Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni. Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua. Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko. Simoni na wenziwe wakamfuata; nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta. Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea. Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo. Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.

Shirikisha
Soma Marko 1

Marko 1:21-45 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Wakaenda hadi Kapernaumu. Mara ilipofika siku ya Sabato, Yesu akaingia sinagogi, akaanza kufundisha. Watu wakashangaa sana kwa mafundisho yake, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka, wala si kama walimu wa sheria. Wakati huo huo katika sinagogi lao palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye akapaza sauti akisema, “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ndiwe Aliye Mtakatifu wa Mungu!” Lakini Yesu akamkemea, akamwamuru, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Yule pepo mchafu akamgaragaza huyo mtu kwa nguvu, kisha akamtoka akipiga kelele kwa sauti kubwa. Watu wote wakashangaa, hata wakaulizana wao kwa wao, “Haya ni mambo gani? Ni mafundisho mapya, tena yenye mamlaka! Anaamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” Sifa zake zikaanza kuenea haraka katika eneo lote la karibu na Galilaya. Mara walipotoka katika sinagogi, walienda pamoja na Yakobo na Yohana hadi nyumbani mwa Simoni na Andrea. Mama mkwe wa Simoni alikuwa kitandani, ana homa, nao wakamweleza Yesu habari zake. Hivyo Yesu akamwendea, akamshika mkono na kumwinua. Kisha homa ikamwacha, naye akaanza kuwahudumia. Jioni ile baada ya jua kutua, watu wakamletea Yesu wagonjwa wote na waliopagawa na pepo wachafu. Mji wote ukakusanyika mbele ya nyumba hiyo. Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa ya aina mbalimbali. Akawatoa pepo wachafu wengi, lakini hakuwaacha hao pepo wachafu waseme, kwa sababu walimjua yeye ni nani. Alfajiri na mapema sana kulipokuwa bado kuna giza, Yesu akaamka, akaondoka, akaenda mahali pa faragha ili kuomba. Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta, nao walipomwona, wakapaza sauti, wakasema, “Kila mtu anakutafuta!” Yesu akawajibu, “Twendeni mahali pengine, kwenye vijiji jirani, ili niweze kuhubiri huko pia. Maana nilikuja kwa kusudi hili.” Kwa hiyo akazunguka Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo wachafu. Mtu mmoja mwenye ukoma alimjia Yesu, akapiga magoti, akimwomba, “Ukitaka, unaweza kunitakasa.” Yesu, akiwa amejawa na huruma, akaunyoosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara ukoma ukamtoka, naye akatakasika. Baada ya Yesu kumwonya vikali, akamruhusu aende zake mara moja; akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote habari hizi, bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka alizoagiza Musa kwa utakaso wako, ili kuwa ushuhuda kwao.” Lakini yule mtu akaenda akaanza kutangaza habari za kuponywa kwake waziwazi. Kwa hiyo, Yesu hakuweza tena kuingia katika miji waziwazi bali alikaa sehemu zisizo na watu. Hata hivyo watu wakamfuata huko kutoka kila upande.

Shirikisha
Soma Marko 1