Marko 1:1-9
Marko 1:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako.’ Sauti ya mtu anaita jangwani: ‘Mtayarishieni Bwana njia yake, nyosheni barabara zake.’” Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.” Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani.
Marko 1:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Yudea, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwituni. Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.
Marko 1:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake. Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu. Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.
Marko 1:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: “Tazama, nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako”: “sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.’” Yohana Mbatizaji alikuja akibatiza huko nyikani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi. Watu kutoka Yudea yote na sehemu zote za Yerusalemu walikuwa wakimwendea. Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Alikula nzige na asali ya mwitu. Naye alihubiri akisema, “Baada yangu atakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuinama na kulegeza kamba za viatu vyake. Mimi nawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.” Wakati huo Yesu akaja kutoka Nazareti ya Galilaya, naye akabatizwa na Yohana katika Mto Yordani.