Mika 7:1-20
Mika 7:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Ole wangu! Hali ilivyo ni kama baada ya mavuno; hakuna tini za mwanzoni ninazotamani. Ni kama wakati wa kuchuma zabibu hakuna hata shada moja la zabibu la kula! Hakuna mcha Mungu aliyebaki nchini, hakuna mtu yeyote mnyofu miongoni mwa watu. Kila mmoja anavizia kumwaga damu; kila mmoja anamwinda mwenzake amnase. Wote ni mabingwa wa kutenda maovu; viongozi na mahakimu hutaka rushwa. Wakubwa huonesha wazi nia zao mbaya, na kufanya hila kuzitekeleza. Mwema zaidi kati yao hutaabisha kama mbigili, aliye mnyofu zaidi ni kama ua wa miiba. Siku iliyongojewa ya adhabu yao imefika. Na sasa mahangaiko yamewakumba. Usimwamini mwenzako, wala usimtumainie rafiki yako. Chunga unachosema kwa mdomo wako, hata na mke wako wewe mwenyewe. Maana, mtoto wa kiume anamdharau baba yake; mtoto wa kike anashindana na mama yake, mke wa mwana anapingana na mama mkwe wake. Maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. Lakini mimi namtumainia Mwenyezi-Mungu, namtazamia Mungu mwenye kuniokoa; Mungu wangu atanisikiliza. Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; Nikiwa gizani, Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu. Kwa vile nimemkosea Mwenyezi-Mungu, sina budi kuvumilia ghadhabu yake, mpaka atakapotetea kisa changu na kunijalia haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaona akithibitisha haki. Hapo adui yangu ataona hayo naye atajaa aibu; maana aliniambia: “Wapi basi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako?” Mimi mwenyewe nitamwona adui akianguka; atakanyagwakanyagwa chini kama tope la njiani. Siku yaja ambapo kuta za mji wenu zitajengwa upya. Siku hiyo mipaka ya nchi yenu itapanuliwa. Siku hiyo ndugu zenu watawarudia, kutoka Ashuru na vijiji vya Misri, kutoka nchi ya Misri na eneo la Eufrate; kutoka sehemu za maji na sehemu za milima. Lakini nchi yote nyingine itakuwa jangwa, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Ee Mungu, uwachunge watu wako kwa fimbo yako, uwachunge hao walio kundi lako mwenyewe ambao wanaishi peke yao katika msitu wamezungukwa na ardhi yenye rutuba. Uwachunge kama ulivyofanya pale awali katika malisho ya Bashani na Gileadi. Kama wakati ulipotutoa nchini Misri, utuoneshe tena maajabu yako. Nao watu wa mataifa watakapoona hayo, watajaa fedheha hata kama wana nguvu. Watashikwa na bumbuazi na kukosa cha kusema na kuwa kama viziwi. Watatambaa mavumbini kama nyoka; naam, kama viumbe watambaao. Watatoka katika ngome zao huku wanatetemeka na kujaa hofu. Watakugeukia wewe Mungu wetu kwa hofu, wataogopa kwa sababu yako. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? Wewe wasamehe dhambi za watu wako waliobaki, wala huyaangalii makosa yao. Hasira yako haidumu milele, ila wapendelea zaidi kutuonesha fadhili zako. Utatuhurumia tena, ee Mwenyezi-Mungu; utafutilia mbali dhambi zetu, utazitupa zote katika vilindi vya bahari. Utaonesha uaminifu wako na rehema zako kwa wazawa wa Abrahamu na wa Yakobo, kama ulivyowaahidi wazee wetu tangu zamani.
Mika 7:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa joto, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao ni hodari kwa kutenda maovu; afisa na hakimu wanataka rushwa, mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu. Nitaivumilia ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea shutuma yangu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi BWANA, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu. Ni siku ya kujengwa kuta zako! Siku hiyo mpaka utasongezwa mbali. Siku hiyo watakujia kutoka Ashuru na miji ya Misri, na kutoka Misri mpaka huo Mto, na kutoka bahari hii mpaka bahari hii, na kutoka mlima huu mpaka mlima huu. Hata hivyo nchi itakuwa ukiwa kwa sababu ya hao wakaao ndani yake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao. Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, msituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonesha mambo ya ajabu. Mataifa wataona, na kuziaibikia nguvu zao zote; wataweka mikono yao juu ya vinywa vyao, masikio yao yatakuwa na uziwi. Watayaramba mavumbi kama nyoka, kama vitu vitambaavyo juu ya nchi watatoka katika mahali walimojificha, wakitetemeka; watakuja kwa BWANA, Mungu wetu, kwa hofu, nao wataogopa kwa sababu yako. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hadumishi hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Abrahamu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.
Mika 7:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa hari, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao inayashika mabaya wayatende kwa bidii; mtu mkuu aomba rushwa, kadhi yu tayari kuipokea; mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu. Nitaivumilia ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea teto langu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi BWANA, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu. Ni siku ya kujengwa kuta zako! Siku hiyo mpaka utasongezwa mbali. Siku hiyo watakujia kutoka Ashuru na miji ya Misri, na kutoka Misri mpaka huo Mto, na kutoka bahari hii mpaka bahari hii, na kutoka mlima huu mpaka mlima huu. Hata hivyo nchi itakuwa ukiwa kwa sababu ya hao wakaao ndani yake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao. Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu. Mataifa wataona, na kuzitahayarikia nguvu zao zote; wataweka mikono yao juu ya vinywa vyao, masikio yao yatakuwa na uziwi. Watayaramba mavumbi kama nyoka, kama vitu vitambaavyo juu ya nchi watatoka katika mahali walimojificha, wakitetemeka; watakuja kwa BWANA, Mungu wetu, kwa hofu, nao wataogopa kwa sababu yako. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.
Mika 7:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Taabu gani hii niliyo nayo! Nimefanana na yule akusanyaye matunda ya kiangazi, aokotaye masazo baada ya kuvunwa shamba la mizabibu; hakuna kishada chenye matunda ya kula, hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani. Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi; hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki. Watu wote wanavizia kumwaga damu, kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya, mtawala anadai zawadi, hakimu anapokea rushwa, wenye nguvu wanaamuru wanachotaka: wote wanapanga njama pamoja. Aliye mwema kupita wote kati yao ni kama mchongoma, anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao ni mbaya kuliko uzio wa miiba. Siku ya walinzi wako imewadia, siku Mungu atakayokutembelea. Sasa ni wakati wao wa kuchanganyikiwa. Usimtumaini jirani; usiweke matumaini kwa rafiki. Hata kwa yule alalaye kifuani mwako uwe mwangalifu kwa maneno yako. Kwa kuwa mwana humdharau baba yake, naye binti huinuka dhidi ya mama yake, mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake: adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa. Lakini mimi, namtazama BWANA kwa matumaini, namngoja Mungu Mwokozi wangu; Mungu wangu atanisikia mimi. Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu! Ingawa nimeanguka, nitainuka. Japo ninaketi gizani, BWANA atakuwa nuru yangu. Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake, nitabeba ghadhabu ya BWANA, hadi atakapotetea shauri langu na kuithibitisha haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaiona haki yake. Kisha adui yangu ataliona naye atafunikwa na aibu, yule aliyeniambia, “Yu wapi BWANA Mungu wako?” Macho yangu yataona kuanguka kwake, hata sasa atakanyagwa chini ya mguu kama tope barabarani. Siku ya kujenga kuta zako itawadia, siku ya kupanua mipaka yako. Siku hiyo watu watakuja kwako kutoka Ashuru na miji ya Misri, hata kutoka Misri hadi Mto Frati, na kutoka bahari hadi bahari, na kutoka mlima hadi mlima. Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao. Wachunge watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, ambalo linaishi peke yake msituni, katika maeneo ya malisho yenye rutuba. Waache walishe katika Bashani na Gileadi kama ilivyokuwa siku za kale. “Kama siku zile mlipotoka Misri, nitawaonesha maajabu yangu.” Mataifa yataona na kuaibika, waliondolewa nguvu zao zote. Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao na masikio yao yatakuwa na uziwi. Wataramba mavumbi kama nyoka, kama viumbe vinavyotambaa ardhini. Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka; watamgeukia BWANA Mungu wetu kwa hofu nao watakuogopa. Ni nani Mungu kama wewe, ambaye anaachilia dhambi na kusamehe makosa ya mabaki ya urithi wake? Wewe huwi na hasira milele, bali unafurahia kuonesha rehema. Utatuhurumia tena, utazikanyaga dhambi zetu chini ya nyayo zako, na kutupa maovu yetu yote katika vilindi vya bahari. Utakuwa wa kweli kwa Yakobo, nawe utamwonesha Abrahamu rehema, kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu siku za kale.