Mika 6:1-8
Mika 6:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikilizeni anachosema Mwenyezi-Mungu: “Wewe nabii, nenda ukailalamikie milima, navyo vilima visikie sauti yako.” Sikilizeni kesi ya Mwenyezi-Mungu enyi milima, sikilizeni enyi misingi ya kudumu ya dunia! Mwenyezi-Mungu anayo kesi dhidi ya watu wake. Yeye atatoa mashtaka dhidi ya Waisraeli. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wangu, nimewatendea nini? Nimewachosha kwa kitu gani? Nijibuni! Mimi niliwatoa nchini Misri; niliwakomboa kutoka utumwani; niliwapeni Mose, Aroni na Miriamu kuwaongoza. Enyi watu wangu, kumbukeni njama za Balaki mfalme wa Moabu, na jinsi Balaamu mwana wa Beori alivyomjibu. Kumbukeni yaliyotukia njiani kati ya Shitimu na Gilgali. Kumbukeni mtambue matendo yangu ya kuwaokoa!” Nimwendee Mwenyezi-Mungu na kitu gani, nipate kumwabudu Mungu aliye juu? Je, nimwendee na sadaka za kuteketezwa, nimtolee ndama wa mwaka mmoja? Je, Mwenyezi-Mungu atapendezwa nikimtolea maelfu ya kondoo madume, au mito elfu na elfu ya mafuta? Je, nimtolee mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, naam, mtoto wangu kwa ajili ya dhambi yangu? Mungu amekuonesha yaliyo mema, ewe mtu; anachotaka Mwenyezi-Mungu kwako ni hiki: Kutenda mambo ya haki, kupenda kuwa na huruma, na kuishi kwa unyenyekevu na Mungu wako.
Mika 6:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi sasa, sikieni asemavyo BWANA; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, shutuma ya BWANA, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana BWANA ana shutuma na watu wake, naye atahojiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa kitu gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nilikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami niliwatuma Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako. Enyi watu wangu, kumbukeni sasa alivyouliza Balaki, mfalme wa Moabu, na alivyojibu Balaamu, mwana wa Beori; kumbukeni yaliyotukia toka Shitimu hadi Gilgali, mpate kuyajua matendo ya haki ya BWANA. Nimwendee BWANA na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimwendee na sadaka za kuteketezwa, na ndama wa umri wa mwaka mmoja? Je! BWANA atapendezwa na maelfu ya kondoo dume, au na makumi elfu ya mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzawa wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!
Mika 6:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi sasa, sikieni asemavyo BWANA; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, mateto ya BWANA, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana BWANA ana mateto na watu wake, naye atahojiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa habari gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako. Enyi watu wangu, kumbukeni sasa alivyouliza Balaki, mfalme wa Moabu, na alivyojibu Balaamu, mwana wa Beori; kumbukeni toka Shitimu hata Gilgali, mpate kuyajua matendo ya haki ya BWANA. Nimkaribie BWANA na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!
Mika 6:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikiliza asemalo BWANA: “Simama, jitetee mbele ya milima; vilima na visikie lile unalotaka kusema. “Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya BWANA, sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia. Kwa kuwa BWANA ana shauri dhidi ya watu wake; anatoa mashtaka dhidi ya Israeli. “Watu wangu, nimewatendea nini? Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu. Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa. Nilimtuma Musa awaongoze, pia Haruni na Miriamu. Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu alivyofanya shauri na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu. Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu hadi Gilgali, ili mfahamu matendo ya haki ya BWANA.” Nimjie BWANA na kitu gani na kusujudu mbele za Mungu aliyetukuka? Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa, nije na ndama za mwaka mmoja? Je, BWANA atafurahishwa na kondoo dume elfu, au mito elfu kumi ya mafuta? Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, mtoto wangu mwenyewe kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu? Amekuonesha yaliyo mema, ee mwanadamu. BWANA anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.