Mika 5:2-5
Mika 5:2-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema, “Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha, wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda, lakini kwako kutatoka mtawala atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu. Asili yake ni ya zama za kale.” Hivyo Mungu atawaacha watu wake kwa maadui, mpaka yule mama mjamzito atakapojifungua. Kisha ndugu zake waliobakia, watarudi na kuungana na Waisraeli wenzao. Huyo mtawala atawachunga watu wake kwa nguvu ya Mwenyezi-Mungu, kwa fahari yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. Watu wake wataishi kwa usalama, maana atakuwa mkuu mpaka miisho ya dunia. Yeye ndiye atakayeleta amani.
Mika 5:2-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye asili yake imekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na uchungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA, kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hadi miisho ya dunia. Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtawaleta wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.
Mika 5:2-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za BWANA, kwa enzi ya jina la BWANA, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia. Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtaondokesha wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.
Mika 5:2-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Lakini wewe, Bethlehemu Efrata, ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda, kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli, ambaye asili yake ni kutoka zamani, kutoka milele.” Kwa hiyo Israeli utaachwa hadi mwanamke aliye na uchungu atakapozaa mwana, na ndugu zake wengine warudi kujiunga na Waisraeli. Atasimama na kulichunga kundi lake katika nguvu ya BWANA, katika utukufu wa jina la BWANA Mungu wake. Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia. Naye atakuwa amani yao.